Mengi vs. Rostam:
Habari leo
Serikali imewakemea wafanyabiashara wawili maarufu nchini, Rostam Aziz na Reginald Mengi kwa kutumia vyombo vyao vya habari kwa maslahi yao binafsi. Imeelezwa kuwa malumbano ambayo wameyaanzisha yanahatarisha amani nchini. Sambamba na hilo, imewataka kuwasilisha vielelezo na madai yao kwa mamlaka husika ili hatua zinazofaa zichukuliwe na wananchi wapewe taarifa na vyombo hivyo. ..bofya na soma zaidi>>>>>
Mtanzania
SERIKALI imewaonya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, kuacha kutumia vyombo vya habari wanavyomiliki kwa ajili ya maslahi binafsi.Serikali pia imewataka wafanyabiashara hao kuacha mara moja malumbano kupitia vyombo vya habari na badala yake wawasilishe madai yao kwa mamlaka zinazohusika ili hatua zinazofaa zichukuliwe…bofya na soma zaidi>>>>>
Uhuru
SERIKALI imewataka Mbunge wa Igunga Rostam Aziz (CCM) na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi, kuacha malumbano kwa kuwa yanaweza kuchochea uvunjifu wa amani. Wameonywa kuwa, endapo wataendelea, serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria…bofya na soma zaidi>>>>
Mwananchi
KESI ya madai ya shilingi moja iliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Quality Group, Yusuf Manji, dhidi ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi itasikilizwa Juni 10 mwaka huu.Kesi hiyo iliyofunguliwa na Manji Aprili 28, mwaka huu, katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba…bofya na soma zaidi>>>>>
Nipashe
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, amekwamisha matumaini ya kushughulikia kansa ya ufisadi nchini, badala ya kutoa tamko alilosema ni la serikali akitaka watu wafunge mdomo kuhusu mafisadi papa waliotajwa na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi.
Katika tamko hilo lililosomwa mbele ya waandishi wa habari na Naibu Waziri wake, Joel Bendera, Mkuchika alisema kwamba kauli zilizoanzishwa na Mengi kwa kuwataja mafisadi papa watano na baadaye kujibiwa na mmojawapo, Rostam Aziz, zimewagawa wananchi na hivyo kuhatarisha amani nchini.
Mkuchika ambaye yuko jimboni Busanda kuendesha kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa ubunge, alisema kauli za ufisadi zimewagawa wananchi katika makundi mawili, moja likimuunga mkono Rostam na jingine Mengi, hivyo kwa upeo wa serikali ni hatari kwa usalama wa nchi.
“Serikali imebaini kuwa malumbano ya Mheshimiwa Rostam Aziz na Bwana Reginald Mengi yamewagawa wananchi katika makundi mawili; ya wale wanaunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rostam Aziz, na wale wanaounga mkono kauli ya Bwana Mengi,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Ingawa Mkuchika alikiri kwamba kila raia ana haki kikatiba kutoa maoni yake, alisisitiza ni lazima uhuru huo utumike kwa maslahi ya Taifa. Hata hivyo, hakufafanua maslahi ya taifa katika vita dhidi ya mafisadi ni yapi, ama kuwasaidia kuendelea kuibia nchi au kuwafichua ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Kadhalika, Mkuchika alisema serikali imebaini kuwepo matumizi mabaya ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Mengi kwa upande mmoja na Rostam kwa upande mwingine, na kwamba (matumizi) hayo yanalenga maslahi binafsi.
Hata hivyo, Bendera kwa niaba ya Mkuchika alipoulizwa maslahi binafsi ya Mengi katika kadhia hii ni nini hakueleza na badala yake alisema: “Hilo ndio tamko la serikali, someni mlielewe.”
“Serikali imebaini katika malumbano haya kumekuwepo na matumizi ‘mabaya’ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Bwana Mengi (televisheni, magazeti na redio) na Mheshimiwa Rostam Aziz (magazeti). Kila mmoja anatumia vyombo vya habari anavyomiliki kwa manufaa yake binafsi kinyume na maelekezo ya sera ya habari na utangazaji ya mwaka 2003,” imefafanua taarifa hiyo.
Hata hivyo, hakuna sehemu yoyote katika tamko hilo lenye kurasa nne, wala maelezo ya Bendera ambayo yalifafanua maslahi ya Mengi ama Rostam katika vita dhidi ya ufisadi.
Kadhalika, Bendera alipoulizwa uhalali wa kituo cha televisheni cha umma TBC1, kutangaza taarifa za mtuhumiwa wa ufisadi Rostam kupitia ‘kipindi maalumu’, alisema: “Hilo swali nendeni mkamuulize Mkurugenzi Tido (Mhando), mimi siwezi kujibu.”
TBC1 Mei 3, mwaka huu ilitoa kipindi maalum cha Rostam Aziz akimtuhumu Mengi kwamba ni fisadi nyangumi, huku akikwepa kuzungumzia kwa kina tuhuma za ufisadi dhidi yake. TBC1 ni mali ya umma na inaendeshwa pamoja na mambo mengine kwa kodi za wananchi.
Mbali na TBC1, pia magazeti ya umma ya Daily News na HabariLeo, nayo yalishabikia upande wa watuhumiwa watano wa ufisadi, ambao ni Rostam, Yusuf Manji, Subhash Patel, Jeetu Patel na Tanil Somayia.
Tamko la serikali wala halikutaja japo kwa mstari utendaji wa vyombo hivyo, na hata yale magazeti mengine yenye uhusiano na watuhumiwa hao ambayo yamekuwa yakikebehi wale wote walioko mstari wa mbele kupambana dhidi ya ufisadi.
Tamko hilo liliongeza, “serikali imeyatafakari malumbano ya wafanyabiashara hawa na kubaini kwamba yanalipeleka Taifa letu mahala pabaya…yana mwelekeo wa uvunjaji wa amani kama yataachwa yaendelee.”
Alipoulizwa sababu ya serikali kupitia wizara yake kuchelewa kutoa tamko hilo kama alivyofanya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, Bendera alijibu “serikali haikurupuki kutoa tamko.”
Mbali na Sophia, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni hivi karibuni, aliwataka wale wote wanaodhani wamekashifiwa katika tamko la Mengi juu ya mafisadi papa waende mahakamani. Alikuwa akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed.
Bendera pia alipoulizwa kwa nini serikali haikuchukua hatua kama hiyo wakati majina ya mafisadi yalipotangazwa mwaka juzi na Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Wilibrod Slaa, katika viwanja vya Mwembe Yanga Septemba 15, 2007, alisema “Mavi ya kale hayanuki, sisi tunazungumzia ya leo.”
Katika tamko hilo ambalo linafungua ukurasa mpya wa mapambano ya ufisadi nchini, serikali imesisitiza; “Kutokana na hali hiyo, serikali inawataka Rostam na Mengi kuacha mara moja malumbano kupitia vyombo vya habari, na badala yake wawasilishe madai na vielelezo vyao kwa mamlaka husika, ili hatua zinazofaa zichukuliwe na wananchi wapewe taarifa.”
Bendera alisema serikali haitakubali kusikia malumbano hayo wala vyombo vya habari vikichangia kuligawa Taifa katika makundi na kudumaza maendeleo.
Kadhalika, Waziri huyo hakufafanua maendeleo yanayodumazwa ni yapi, kwa kuwa katika malalamiko ya wananchi juu ya wizi wa rasilimali za umma, huduma za kijamii zimedumaa kutokana na fedha nyingi kuishia mifukoni mwa mafisadi.
Kwa mfano, katika wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jumla ya Sh bilioni 133 ziliibwa na mafisadi.
Fedha hizo kama zingeelekezwa kwenye shughuli za maendeleo kama ujenzi wa barabara, zina uwezo wa kujenga zaidi ya km 400 za lami.
Pia, tamko hilo lilielezea kusikitishwa na kile ilichokiita kuwa ni kitendo cha Mengi, kuzungumzia kesi ambazo ziko mahakamani.
“Sheria za nchi zinakataza mtu, watu kuzungumzia ama kujadili suala ambalo tayari lipo mahakamani, kwa kufanya hivyo Mengi amewahukumu watuhumiwa hao na kuwatia hatiani bila wao kupewa fursa ya kusikilizwa,” alisema.
Hata hivyo, tangu atangaze majina ya watuhumiwa wa ‘mafisadi papa’ Aprili 23, mwaka huu, mahakama yenye mamlaka ya kutafsiri sheria, haijatoa tamko linalohusu Mengi kuingilia mashauri yanayo kwenye mkondo wa sheria.
Kadhalika, katika kesi za EPA ambazo zipo mahakamani, kuna mlolongo mrefu wa makampuni mengine ambayo hayajafishwa huko kama Kagoda Agriculture Limited inayotuhumiwa kuchota zaidi ya Sh bilioni 40.
Hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa serikali anayetaka kuzungumzia Kagoda, na juhudi za vyombo vya habari kutoka kujua uchunguzi wa Kagoda zimegonga mwamba kila ofisi ikiwa ni pamoja na kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kukwepa.
Tamko la serikali pia liliwataka wahariri na wanahabari kuwa makini katika kutimiza wajibu wao kwa weledi na kuzingatia maadili ya kitaaluma, badala ya kuzingatia matakwa ya wamiliki wa vyombo wanavyovifanyia kazi.
Alisema serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wamiliki ambao hawatazingatia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na sheria ya utangazaji ya mwaka 2003 katika kutekeleza kazi zao.
Hata hivyo, serikali inayoendesha TBC1, Daily News na HabariLeo, hakusema katika tamko lake kwamba itachukua hatua gani juu watendaji wa vyombo hivyo ambao wameamua kumbeba Rostam Aziz na watuhumiwa wengine wa ufisadi. Waziri huyo, alisema pamoja na tamko hilo serikali inasisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi yanaendelea na kuwahimiza wananchi wenye taarifa kuziwasilisha katika vyombo vya dola.
Baada ya Mengi kuwataja hadharani Aprili 23, mwaka huu, ‘mafisadi papa’ watano, Rostam, Somaiya, Jeetu, Manji na Subash, mpaka sasa, ni Rostam, Manji na Subash tu wameibuka na kuibua madai mapya dhidi ya Mengi, huku wakishindwa kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwao.
No comments:
Post a Comment