Friday, May 15, 2009

Migogoro ya Afrika imeleta

uhalifu Zanzibar


Moja ya silaha inayotumika sana kwenye migogoro mingi duniani na kwenye uhalifu ni bunduki ya aina ya AK-47 (Avtomat Kalashnikova obraztsa 1947 goda; "Kalashnikov's automatic rifle model of year 1947".  Aina hii asili yake ni Urusi. Nchi nyingi kama China, nchi za Ulaya ya Mashariki na hata baadhi ya nchi za Ulaya ya Magharibi, za Mashariki ya Kati, Latini Amerika, baadhi ya nchi za Kiafrika zimetengeneza bunduki hii kwa leseni. Aina nyingi za kufuatia AK-47 zimetengezwa duniani. Mbunifu wa AK–47 alikuwa Luteni Jenerali Mikhail Kalashnikov (Mhariri wa blogu)

 

  

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema migogoro inayozikabili nchi mbalimbali za Afrika, imesababisha silaha ndogo ndogo kuzagaa na kuanza kuathiri visiwa vya Unguja na Pemba.

 

Imesema hiyo inatokana na ongezeko la vitendo vya ujambazi nchini. Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Kiongozi, Ali Rajab, alipokuwa akifungua mkutano wa mtandao wa kushughulikia udhibiti wa kuzagaa silaha ndogo ndogo na nyepesi unaofanyika Zanzibar.

 

Mkutano huo umeandaliwa na Jumuiya ya Hururept–Rust ya kutoka Arusha. Alisema kutokana na wimbi la migogoro iliyosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe hasa katika maeneo ya ukanda wa Maziwa Makuu, umesababisha silaha ndogo ndogo kuzagaa na kuongezeka vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha.

 

Hata hivyo, alisema serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na matatizo hayo kwa kushirikiana na Jumuiya zisizokuwa za kiserikali ili kudhibiti uhalifu wa kutumia silaha.

 

Alisema serikali inakubali kushirikiana na Jumuiya za Asasi za Kiraia Zanzibar kukabiliana na tatizo hilo kwa kuunda mtandao maalum Zanzibar kufanikisha vita vya kudhibiti ueneaji wa silaha holela ambao umekuwa chanzo kikubwa cha uhalifu a kutumia silaha.

 

Aidha, alisema suala la kuzagaa silaha katika ukanda wa maziwa makuu lilikuwa ajenda kubwa katika jumuiya ya maendeleo ya Kusini (Sadc) na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wake.

 

Naye Mratibu wa Mkutano huo, Peter Mcomalla, alisema tatizo la kuzagaa silaha holela, limeathiri dunia kutokana na vitendo vya uhalifu kujitokeza katika mataifa mbalimbali hususan Afrika na kuwataka wananchi wa Zanzibar kutumia mtandao utakaoanzishwa kukabiliana na tatizo hilo.

Chanzo gazeti la Nipashe.

No comments: