Monday, May 18, 2009

Rostam katika tope jipya


Rostam Aziz (RA)


Na Mwandishi Wetu
MwanaHALISI ~ Maslahi ya Taifa Mbele


TUHUMA mpya za ufisadi zimeibuka dhidi ya mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na kumzamisha katika tope jipya, MwanaHALISI limegundua.

Tuhuma hizo zinahusu gharama za kutoa bandarini tani 4,677.82 za mahindi kazi iliyofanywa na Rostam Aziz.

Kazi hiyo iligharimu Sh. 894,372,520 bila ya kuwapo mkataba kati ya Rostam na serikali.

Tuhuma hizo zimebainishwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

CAG anasema fedha hizo zililipwa kwa Kampuni ya Tanzania Packages Manufacturers (1998) Ltd, kupitia akaunti Na. 1010400548400 iliyoko Benki ya Standard Chartered, na mhusika ni Rostam Aziz.

Ofisi ya CAG anasema ununuzi huo wa mahindi tani 4,677.82 zenye thamani ya dola za Marekani 1,113,788.942 ni wa mashaka. Wakati huo dola moja ya Marekani ilikuwa Sh. 803.00. Rostam alizoa Sh. 894,372,520.

“Hata hivyo, malipo haya yalifanyika bila kuwapo mkataba kati ya Rostam Aziz na serikali. Vilevile hapakuwapo nyaraka muhimu za kuingiza mahindi nchini, kama ilivyodokezwa katika aya ya 3.1.1 ya taarifa hii (ya CAG), hivyo kutia mashaka kama kweli mahindi haya yalinunuliwa toka nje ya nchi,” inasema taarifa.

Taarifa hiyo ilikuwa inahusu utoaji wa zabuni na mikataba ya ununuzi wa tani 175,000 za mahindi kutoka nje ya nchi na msimamizi alikuwa Wizara ya Kilimo na Ushirika-Idara ya Usalama wa Chakula.

Taarifa ya CAG ilikuwa ikipelekwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), na imesainiwa na Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, E.K.Shuli.

Kwa mujibu wa aya hiyo, nyaraka muhimu za kuingiza mahindi ndani ya nchi, kama ilivyosainiwa chini ya kifungu 5.3 cha mkataba hazikuonyeshwa.

Nyaraka hizo ambazo hazikuwasilishwa ni pamoja na nakala tano za Ankara (invoice) zinazoonyesha aina ya mali iliyoagizwa, kiasi, bei na thamani ya mali.

Nyaraka nyingine ni nakala halisi za kuingiza mizigo nchini; nakala tano zenye orodha ya mali inayoingizwa nchini; cheti cha bima, cheti cha muuzaji mahindi kuthibitisha kuleta mali na cheti cha usafi wa mali.

Cheti kingine kilichokosekana ni kile cha ukaguzi wa ubora wa mali kutoka kwa mkaguzi wa ubora (viwango) wa nchi ambayo mali hiyo imeagizwa au kununuliwa.

“Kukosekana kwa nyaraka hizi muhimu za uingizaji mali nchini kunatia mashaka juu ya ubora wa mali iliyonunuliwa, na kama kweli mahindi yaliagizwa nje ya nchi na kampuni mbili,” inasema taarifa ya CAG.

Mikataba ya ununuzi wa mahindi ilikuwa baina ya serikali na kampuni mbili za EECO Traders Ltd ya Uingereza, ambayo ilitakiwa kuingiza tani 25,000 zenye thamani ya dola za Marekani 4,187,500 na M/S Andre & CIE ya Afrika Kusini, ambayo ilitakiwa kuingiza tani 100,000 zenye thamani ya dola za Marekani 19,075,500.

Majukumu ya mikataba hiyo miwili yalitekelezwa na Kampuni ya Tanzania Packages Manufacturers (1998) Ltd., na mhusika mkuu ni Rostam Aziz.

Malipo ya kampuni zote mbili yalifanywa kwa kampuni hiyo na anayetajwa kupokea malipo ni Rostam yuleyule.

Kubadilishwa kwa mfumo wa malipo kwa kampuni hiyo kulisababisha Barua ya Dhamana (LC) ya Sh. 2.995 bilioni iliyokuwa imefunguliwa katika NBC (1997) Ltd., tawi la City Drive kwa ajili ya EECO Traders Ltd., kuliingizia serikali hasara ya Sh. 29,329,728/25 ikiwa ni kamisheni ya benki kwa ajili ya kufungua LC hiyo.

Taarifa ya CAG kwa Bunge inasema, “Kitendo cha Kampuni ya Tanzania Packages Manufacturers (1998) Ltd., kuchukua majukumu ya kutekeleza mikataba hii bila kibali cha maandishi cha serikali, kinaleta mashaka katika ununuzi huo wa mahindi.”

Taarifa inasema kwa makosa hayo, serikali inapaswa kuidai EECO Traders Ltd., fidia ya hasara hiyo ya Sh. 29,329,728.82 iliyosababishwa na Rostam Aziz.

Mbali na hasara hiyo, ukaguzi wa mikataba na nyaraka zilizohusika kupokelea mahindi ulionyesha kuwa tani 1,662.985 hazikupokelewa.

Kufuatia kucheleweshwa kuletwa nchini kiasi hicho cha mahindi, wazabuni walipaswa kulipa fidia ya ucheleweshaji huo inayofikia jumla ya dola 745,993.

Taarifa ya CAG inaitaka wizara ya kilimo na ushirika ithibitishe iwapo tani 1,662.985 za mahindi zilizochelewa kupokelewa ziliingizwa nchini baadaye na thamani yake ielezwe.

“Wizara ithibitishe uhalali wa malipo haya kwa kuwasilisha mkataba wa ununuzi wa tani 4,677.82 za mahindi kati ya serikali na Rostam Aziz,” inasema taarifa ya CAG kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Tuhuma hizi zinakuja wakati serikali imetangaza kufunga mjadala juu ya tuhuma zinazomkabili
Rostam na Mengi mengine yakitarajiwa kuibuliwa.

No comments: