Waswahili walisema
“Hakuna siri ya watu wawili”
Tumelipuana wenyewe!

Kituo cha luninga ya biashara hapa Norway TV 2 kimebainisha ubabaishaji wa kuchukua hela za ruzuku isivyo halali kwa baadhi ya vyama vya wageni hapa Oslo (Norway). Vyama vingi vya wageni hapa Norway pamoja na chama kikubwa kuliko vyote vya wageni hapa, Pakistan Welfare Society chenye makao yake makuu mjini Oslo, vimekuwa kwa muda mrefu vikipewa ruzuku za kuendeshea shughuli zao na Manispaa ya Oslo (Oslo Kommune), taasisi na vitengo vinavyohusika na wizara ya mambo ya nchi za nje ya hapa.
Moja ya vigezo vya kukubalika kupewa ruzuku ni kuwa orodha ya wanachama, namba zenye tarakimu kumi na moja za kitaifa (National identity number/fødselsnummer), anwani za wanachama na kuwa ankra inayoonyesha kuwa wanachama wanalipa ada za mwezi/mwaka. TV 2 imebaini kuwa, Pakistan Welfare Society (PWS) imekuwa na vyote hivyo, kinyume cha kanuni za sheria za kuendesha vyama vya kijamii.
Ada za mwezi/mwaka zimekuwa zikilipwa na PWS yenyewe, halafu wakipewa ruzuku, wanazirudisha kwenye chama, zilizobaki wanafanyia shughuli zao. Zingine zimejengea mahekalu nchini Pakistani. Pia imebainika kuwa asilimia 80 ya waliowaorodhesha kama wanachama wao, wamekataa kuwa si wanachama wa PWS walipoulizwa na TV2. PWS imefanya mchezo wa rafu wa kuchukua namba za kitaifa za hao waliowaorodhesha kama wanachama na anwani zao na kujaza kwenye fomu za maombi kama wanachama wao ili kutimiza vigezo vya kuombea ruzuku.
Kashfa hii inamhusisha, Khalid Mahmood ambaye anagombea ubunge kwa tiketi ya chama cha Labour (Arbeidepartiet), kwenye uchaguzi mkuu, utakaofanyika Jumatatu 14. Septemba mwaka huu. Khalid Mahmood, amekuwa akijishughulisha na PWS tangu miaka ya sabini. Na mpaka hivi majuzi jina lake lilikuwa limeorodheshwa kama katibu mkuu wa PWS.
TV 2 inabainisha kuwa mchezo huo wa rafu, hauchezwi na Pakistan Welfare Society pekee yake. Vyama vingi vya kijamii vya wageni vimekuwa vikicheza rafu za namna hii na vimekuwa vikiendeshwa kienyeji mno.
Serikali ya Manispaa ya Oslo (Oslo Kommune) imeamua kuvichunguza vyama vyote vya wageni vinavyopokea ruzuku za Manispaa. Uchunguzi huo, utaangalia orodha za wanachama kama ni halali au batili, ruzuku zinavyotumika na jinsi shughuli za vyama hivyo zinavyoendeshwa. Vyama vitakavyogundulika kuwa vimecheza rafu, viongozi wa hivyo vyama watawajibishwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Jinsi gani wamekuwa wakuwalipia hao “wanachama?”
Mtu mmoja anafanya kazi ya kutembea kwenye mabenki tofauti kwa nyakati mbali mbali na kumlipia mwanachama mmoja mmoja kwa siku na nyakati tofauti (hata wiki tofauti) ili ionekane kweli “mwanachama” amelipa ada yake kwa kutumia giro ya benki/posta yenye jina na maelezo kina (particulars) ya “mwanachama” mlengwa .
Bahati nzuri Chama Cha Watanzania Oslo, hakijawahi kucheza mchezo huu. Kwa miaka mingi sasa Chama Cha Watanzania Oslo kimeshindwa kuomba ruzuku kutoka Manispaa ya Oslo, taasisi na vitengo vinavyohusika kwa kukosa orodha ya wanachama iliyokamilika. Chama Cha Watanzania Oslo, hakina orodha ya wanachama wanaolipa ada, wala haina orodha ya wanachama na namba zao za kitaifa. Chama Cha Watanzania Oslo, kinajiendesha kwa nguvu zake zenyewe (nguvu za soda).
1 comment:
Nena Mkuu, nena te te eeh
Post a Comment