Friday, July 31, 2009

Ustaz Mohammed Yusuf:

kiongozi wa Boko Haram

auawa akiwa lupango

mjini Maiduguri




Ramani ya Naijeria na majimbo 37



Kiongozi wa kikundi kimoja cha Waislam wenye siasa kali nchini Naijeria, kiitwacho Boko Haram (maana yake “elimu ya magharibi ni haramu”), Ustaz Mohammed Yusuf ameuawa akiwa chini ya ulinzi wa polisi mjini Maiduguri. Hayo yalithibitishwa na Kamanda Isa Azare wa kamandi kuu ya polisi ya Maiduguri, alipoliambia shirika la habari la Reuters.



Fujo za Boko Haram zilianza Jumapili iliyopita kwenye jimbo la Bauchi, kabla ya kuenea kwenye majimbo mengine ya kaskazini mashariki ya Naijeria. Mapigano baina ya polisi wakishirikiana na jeshi la Naijeria na wafuasi wa Boko Haram, yamesababisha vifo vya watu zaidi ya mia sita. Juzi Jumatano jioni, askari jeshi walivamia ngome ya Boko Haram, na kuwauwa wafuasi wengi Boko Haram na kuwafanya wengine wakimbie. Jana Alhamisi, Mohammed Yusuf alikamatwa na jeshi.



Kwenye mkutano wa pamoja kati ya idara ya usalama ya Naijeria (State Security Service), idara ya usalama ya jeshi la Naijeria (Defence Intelligence Agency), idara ya polisi na shirika la ujasusi la nchi hiyo (National Intelligence Agency), Kanali Mohammed Yerima (Mkurugenzi mkuu wa usalama jeshini) alisema kuwa kikundi hicho kimekuweko tangu mwaka 1995. Kimekuwa na majina mbalimbali toka kuanzishwa, mojawapo likiwa Ahlulsunna wal’jama’ah hijra. Jina la Boko Haram lilianza kutumika mwaka 2002 na Ustaz Mohammed Yusuf mjini Maiduguri kwenye jimbo la Borno. Mwaka 2004 walihamia mji wa Kanamma kwenye jimbo la Yobe, walipoanzisha ngome yao wakaipa jina “Afghanistan”. Ndipo walipoanza kushambulia vituo vya polisi na kuua polisi kila walipopata nafasi. Boko Haram kimekuwa kikijulikana kama “Taliban wa Naijeria”



Kwenye jimbo la Bauchi, Boko Haram walikataa katakata kujumuika na watu wengine, wakiwemo Waislam wa kawaida. Baadhi ya wafuasi wao wanatoka kwenye nchi za jirani za Chad na Niger. Boko Haram hawataki elimu ya vitabu, sayansi na utamaduni wa nchi za magharibi. Na lengo lao ni kuiangusha serikali kuu ya Naijeria na kuanzisha sheria kali za kiislam kwenye majimbo yote 37 ya Naijeria.



Ustaz Mohammed Yusuf (39) alikuwa na elimu ya juu na ameacha wajane wanne.


1 comment:

Jamaldeen T. Bin Mazar E. Shariff Ibn Zenjibari said...

Huyu jamaa alikuwa anaishi maisha ya anasa sana. Alikuwa na Mercedes Benz na SUV kibao, halafu alikuwa anahubiri tofauti kwa waumini wake.

Umaskini kitu kibaya. Walikuwa wanamfuata kwa umaskini wao wa akili.

Nyerere alisema hakuna umaskini mbaya kuliko umaskini wa akili.