Wednesday, July 29, 2009

Waliofariki ajali ya

basi ya Tanga watajwa


MIILI ya abiria 13 kati ya 28 waliofariki dunia juzi jioni katika ajali ya basi la Kampuni ya Mohamed Trans, wametambuliwa.

Miili hiyo ni kati ya 27 iliyohamishiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo baada ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Magunga, kutokuwa na majokofu.

Moja kati ya miili hiyo ulitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zake ambao ni wakazi wa mji wa Mombo wilayani hapa.

Akizungumza katika eneo la tukio, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, James Kombe, aliwataja maiti waliotambuliwa kuwa ni Joseph Kamitee ambaye ni dereva wa pili wa basi la Mohamed Trans na dereva wa lori la Kampuni ya Simba Track, lililogongana na basi hilo, Ramadhani Kipsto.

Kwa mujibu wa Kamanda Kombe, wengine ni raia wawili wa Marekani, akiwamo Catheline Brooke Baxter mwenye paspoti namba 089355273 iliyotolewa New Orleans na Francis Kanyoike raia wa Kenya.

Wengine ni Hasan Ramadhani (35), Julius Molel (40), Mkandarasi Said (32), Ludovic Masele (48), Ainaini Marro (53), Wilsdom Mmasa (17), Ramadhani Shaban (21) na Baraka Shaban ambaye ni utingo wa lori.

Pia wamo Muhammed Said, Neema Robert (24), ambaye ni Ofisa Uhamiaji Namanga, Daniel Owin, (34), Mbaruju David Kasanda (35) na Hagiroli Utrikali, Mtanzania mwenye asili ya Kiasia.

Katika Hospitali ya Bombo, hadi tunaandika habari hizi, tayari maiti 13 zilikuwa zimeshatambuliwa na ndugu zao kati yao wanaume ni 11 na wanawake wawili.

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga aliyefika eneo la ajali na baadaye Hospitali ya Magunga, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Erasto Sima alisema majeruhi 14 walifikishwa kwa ajili ya matibabu ambapo wawili wamekimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya hali zao kuwa mbaya.

Aliwataja majeruhi waliokimbizwa Muhimbili kuwa ni Maria Kika, mkazi wa Moshi na Mary Erasnos, ambao wote wamepata majeraha vichwani.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Rashid Said alisema majeruhi ambao wataendelea kupata matibabu hospitalini hapo ni Erasmos Mathias, Nelson Giatu na Lugano Martin ambaye ni dereva wa kwanza aliyekuwa akiendesha basi hilo wakati likipata ajali.

Majeruhi wengine ambao walifikishwa hospitalini hapo na wanatarajia kupewa ruhusa ni Ahmed Abdallah (22) wa Nairobi, Abdallah Ademi (22) wa Nairobi, Peter Nyakua (43) wa Tarime, Mtunzi Selemani (32) wa Bukoba, Mary Erasmus (27) wa Babati, Hellen Alex 23 wa Nairobi, Jane Njeri (33) na Jenipher Mushi (29) wa Rombo, Tarakea.

Wengine ni Nelson Gitau (40) wa Himo, Jimmy Massawe (32) wa Machame na Ludovic Mcharo 20 wa Tanki la Maji Ilboru.

Akizungumza na wananchi waliofika eneo la ajali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Meja Jenerali Said Kalembo, aliwataka abiria waonapo madereva wanaendesha kwa mwendo wa kasi, kutoa taarifa polisi ili waweze kudhibitiwa.

“Nawapa mkono wa pole ndugu wa waliokufa katika ajali hii, ni janga kubwa limetukuta Tanga, lakini nawaomba abiria mkiendeshwa kwa kasi, toeni taarifa polisi,” alisema Kalembo.

Naye Kombe alieleza kukerwa kwake na mtindo wa madereva kuendesha kwa kasi wakati wamebeba roho za watu.

Dereva wa basi hilo, Samwel Paulo anashikiliwa na polisi mkoani hapa kutokana na ajali hiyo.

Kutoka Tanzania Daima


No comments: