Kuandika kwa
Profesa Joseph L. Mbele
NINAPENDA sana kuandika, hasa insha na uchambuzi wa fasihi. Lakini maandishi yangu mengi tangu zamani yamekuwa katika lugha ya kiIngereza. Hali hii imetokana na kwamba mimi ni mwalimu katika masomo ya kiIngereza. Karibu muda wote nasoma na kufundisha katika lugha hiyo. Tangu nilipoanza kujifunza kiIngereza, darasa la tatu, niliipenda lugha hiyo kuliko masomo yote. Hadi nilipoingia sekondari, hali ilikuwa hivyo. Nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilikuwa napenda kusoma na kuandika kiIngereza; kiSwahili nilikuwa sishughuliki nacho sana.
Lakini pole pole, tangu nilipokuwa Chuo Kikuu, nilianza kupata mwamko mpya. Rafiki yangu, ambaye sasa ni Profesa Mugyabuso Mulokozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alinibadilisha mawazo. Alikuwa ananishangaa kwa kuzama katika kiIngereza tu bila kujishughulisha na kiSwahili, hadi nikajitambua kuwa nilikuwa naendekeza kasumba. Kidogo kidogo nilianza kujishughulisha na utafiti katika fasihi ya kiSwahili na baadaye nikaanza kuandika makala kwa kiSwahili. Mulokozi alikuwa sambamba nami, kunihimiza kwa kila hatua niliyofikia. Nawajibika kumshukuru. Katika juhudi zote hizi, nimetambua uzuri na manufaa ya kuandika katika kiSwahili.
Pamoja na kuandika insha kwa kiSwahili, nimekuwa na ari ya kutafsiri tungo za kale za kiSwahili kwenda kiIngereza. Huu ni mtihani bora unaochangamsha sana akili. Katika kutafsiri, mtu unajipima ufahamu wako wa lugha mbili na tamaduni na falsafa zake, na unakumbana na matatizo ya tofauti zilizomo katika lugha, tamaduni na falsafa hizi. Lakini, unapata uzoefu muhimu.
Miezi michache iliyopita, nilipoombwa na Ndugu Maggid Mjengwa kuandika makala katika gazeti la “Kwanza Jamii,” nilikubali bila kusita. Niliona ni fursa nzuri ya kujipima uwezo wangu wa kuandika kwa kiSwahili na pia fursa ya kujipatia uzoefu zaidi katika uandishi huo. Kadiri siku zinavyopita, naona mategemeo yangu hayo yanafanikiwa.
Jambo linalonifurahisha zaidi ni kuwa kwa kuandika kwa kiSwahili, nawasiliana na waTanzania wengi, kuanzia mijini hadi vijijini. Baada ya kuandika makala yangu ya kwanza katika “Kwanza Jamii,” nilipata taarifa kutoka kijijini kwangu kuwa wanakijiji waliisoma makala ile. Kujua kwamba kwa kuandika katika “Kwanza Jamii,” nawasiliana na watu wa kijijini kwangu imekuwa ni changamoto na motisha kwangu. Mijadala inayofuatia makala hizi ni ishara ya kuwa ujumbe unawafikia wananchi. Mijadala hiyo inatupa mwanga kuhusu utata wa masuala mbali mbali.
Kuandika kiSwahili ni kuienzi lugha yetu hii ambayo ina historia ndefu iliyojaa tungo za thamani kubwa, kama vile “Utendi wa Tambuka,” “Utendi wa Mwana Kupona,” “Utendi wa Rasi ilGhuli,” na tungo nyingine nyingi za mabingwa kama Shaaban Robert. Lugha hii na fasihi yake ni hazina isiyo kifani, ambayo tunapaswa kujivunia.
Kiswahili, kama lugha nyingine yoyote, ina uwezo wa kuelezea kila kitu katika jamii yetu na dunia kwa ujumla. Kimuundo ni lugha yenye uwezo kama lugha nyingine yoyote. Kama lugha zingine, lugha ya kiSwahili ina haki ya kukopa maneno kutoka lugha nyingine inapohitajika. Kwa upande wangu, kama nilivyosema, kuandika kwa kiSwahil ni namna ya kujipima uwezo wangu, na pia namna ya kuthibitisha uwezo wa lugha hii.
Shaaban Robert alijivunia lugha ya kiSwahili na alikuwa hodari wa kuitumia kwa ufasaha na mvuto mkubwa. Kwa uandishi wake, aliitukuza lugha hii kwa namna ambayo haijawahi kuonekana, na wengi wamejaribu kufuata mfano wake. Mbali na kuitumia vizuri lugha ya kiSwahili, Shaaban Robert aliandika kuhusu uzuri wa lugha hii, akijivunia urithi wake.
Pamoja na kuipenda na kuienzi lugha ya kiSwahili, Shaaban Robert hakuwa mbaguzi.
Aliziheshimu lugha zingine pia na kutambua ubora wake. Heshima ilikuwa ni msingi mkubwa wa tabia na mtazamo wa Shaaban Robert kimaisha. Ingawa elimu yake ya shuleni haikuwa kubwa alijitahidi hata kuandika kwa kiIngereza. Alijituma pia katika kutafsiri maandishi kutoka katika kiIngereza kwenda katika kiSwahili. Shaaban Robert alimsifu sana Shakespeare, yule mwandishi maarufu sana wa zamani wa kiIngereza, akisema kuwa akili ya Shakespeare ilikuwa pana kama bahari, ambayo mawimbi yake yalitua kwenye fukwe za dunia yote.
Nashukuru kuwa nilipata mwanga wa kujiingiza katika utumiaji wa kiSwahili badala ya kujisahau katika kiIngereza tu. Ni mkondo ambao Mwalimu Nyerere alitaka tuufuate. Yeye aliienzi lugha ya kiSwahili kwa maneno na vitendo. Aliitumia vizuri katika maandishi na hotuba zake, na aliipa hadhi kama lugha ya Taifa. Alitafsiri maandishi ya kiIngereza kwa kiSwahili, kama vile tamthilia za Shakespeare. Alituachia mfano wa kuigwa.
Kuandika kiSwahili, kama vile ilivyo kuandika katika lugha nyingine yoyote, ni kazi inayohitaji jitihada na nidhamu. Kwa upande wangu, naona manufaa yake ni mengi, kwani inaniongezea uzoefu na pia kuniunganisha na jamii ya watumiaji wa kiSwahili
Joseph L. Mbele
1520 St. Olaf Avenue
Northfield MN 55057
Phone: 507 403 9756
http://www.josephmbele.blogspot.com
http://www.hapakwetu.blogspot.com
Makala hii imechapishwa kwenye Kwanza Jamii
No comments:
Post a Comment