Monday, August 03, 2009

Tohara dhalili kwa wanawake



JUMAPILI iliyopita tulijuzana kuwa tohara za wanaume ni suala la usafi, afya na urijali; lakini je kwa wanawake?

Neno sahihi si tohara bali ukeketaji. Kweli kumtahiri mtoto dume husaidia kupunguza maradhi takilifu ya ngono mathalan Ukimwi, Kisonono, Herpes (uvimbe vimbe unaowasha) na saratani mbalimbali ikiwemo ile ya kizazi cha wanawake, na bahati nzuri, mada hiyo ikafafanuliwa fafanuliwa zaidi katika safu ya Daktari wa Mwananchi.

Mila ya ukeketaji tunaelezwa na wataalamu wa kisayansi na wapigania haki za wanawake ilianza enzi za watawala wa Faraoh nchini Misri zaidi ya miaka 3,000 iliyopita.

Haikuanzishwa na dini kama baadhi yetu tunavyoamini au kuelezwa. Maiti za mumiani zilizohifadhiwa zimeonyesha ukeketwaji wa wanawake ulikuwepo kabla ya Ukristo (miaka 2,000) na Uislamu kuanza miaka 1,400 iliyopita. Saudi Arabia mathalan penye chimbuko la Uislamu haifanyi tohara hii haramu kwa wanawake. Leo bado nchi 28 za Afrika, ikiwamo Tanzania zingali zinaendeleza mila hii potofu

Je, huwaje?

Kuna aina tatu za ukeketaji.

Kwanza inayojulikana zaidi ni kuondolewa kiungo kinachompa furaha mwanamke wakati wa kufanya mapenzi, yaani kinembe. Kiungo hicho maalumu kinapoondolewa husababisha matatizo mawili.

Mosi, kuharibika mshipa muhimu wa damu, hatua inayomletea bibiye maumivu maisha yake yote; pili anayekeketwa hasikii raha wakati akiwa na mumewe. Lengo la ukataji huu kimila ni furaha kwa mwanaume huku likimweka mke mtu jela la maisha; haoni faida (au hana haja) ya kutembea ovyo na mume mwingine.

Aina ya pili ni mbaya zaidi. Mabonde mawili yanayouzunguka uke wa mwanamke na yanayoupa uke sura huondolewa kabisa. Aina hii huharibu wajihi wa uke na kumwachia mwanamke kovu linalomkera humletea maumivu wakati wa kufanya mapenzi na mumewe, akivaa nguo za kubana au akiwa katika hedhi. Matokeo? Kujichukia na kutojithamini, shauri ya makovu (yanayogeuka kidonda mara kwa mara). Juu yake hupatwa maumivu makali wakati wa kujifungua.

Aina ya tatu na mbaya kuliko hizo juu ni kushonwa kabisa sehemu ya uke na kuacha njia ndogo tu (inayoenea kidole kidogo cha mkononi) kupitishia haja ndogo. Wanawake hawa hupata shida sana wakiwa hedhini kwa kuwa damu haipiti sawasawa na husababisha mgando ambao nimeelezwa uko kama ugali ugali unaorudia tumboni. Matokeo ni maradhi ya figo, ini na kusokotwa tumbo. Wasichana wengi wanaendelea kufa nchini na duniani kutokana na adha hii.

Idhilali ya mwisho.

Kina mama hawa wanapojifungua hubidi kupasuliwa kumpitisha mtoto; halafu kushonwa tena wakishamaliza uzazi. Nchi inayoongoza kwa tendo hili ni Sudan. Kule tumeelezwa wanawake huzibwa pia waume zao wanaposafiri ili wasifanye mapenzi nje; (kama mlango uliowekwa kofuli); halafu wakirudi wanakatwa tena. Mama mmoja aliyekimbilia Majuu kahadithia jinsi alivyokatwa zaidi ya mara tisa kwa kuwa kazaa idadi hiyo hiyo ya watoto.

Kwetu Tanzania ukeketaji ulipigwa marufuku kisheria na serikali ya Mwalimu Nyerere mwaka 1968 lakini hata baada ya kurekebishwa tena mwaka 1998 bado mikoa mingi inaendeleza mila hii potody—Mathalan, Kilimanjaro, Iringa, Dodoma, Tanga, Morogoro, Manyara, Arusha, Mara , Singida. Nimefahamishwa kuwa mkoa wa Mara unaongoza kupinga ukombozi huu. “Mara ni kipingamizi kikubwa sana maana kila tukijaribu kuanzisha harakati zinazuiwa na Wakurya ambao ni wakorofi katika hili.”

Sasa?

Mmoja wa wanawake aliyepitia madhila haya na ambaye kawa mpiganaji na mwanaharaki mkubwa wa vita dhidi ya ukeketaji wa wanawake ni Chiku Ali, mzaliwa wa Kijiji cha Samumba mkoa wa Singida; leo mkazi wa Bergen, Norway.

Chiku Ali alikeketwa akiwa na miaka mitano. Itikadi iliyoenea katika kabila lake la Wanyaturu ni kuwa wanawake waliokatwa walikuwa wasafi ilhali waliobakia, wachafu. Baadaye alipokuwa mtu mzima, Chiku aligundua kuwa kitendo hicho hakithaminiwi ulimwenguni kama alivyofundishwa au kulelewa na nyanya yake huko Singida.

Tangu mwaka 1993 Chiku amehusika na vyama mbalimbali vinavyosaidia maslahi ya mwanamke hususan tohara hii muflis. Kikundi cha wanawake Norway (Kvinner Fronten) kinachojaribu kuinua maisha ya wanawake hutoa msaada wa kifedha, kiasi cha Kronner 500,000 (shilingi milioni 60) kila mwaka kwa shirika la InterAfrican Committee lililo kama mwavuli unaosaidia kupambana na mila zinazodhalilisha watoto na wanawake barani Afrika. Mwavuli huu ulianzishwa mwaka 1984.

Anachofanya Chiku Ali ni kuwa sauti ya Waafrika huku Majuu akihakikisha kuwa misaada inatolewa kusaidia harakati mbalimbali za wanawake. Mbali na masuala ya tohara pia kaunganisha misaada kwa chama cha Kiwakkuki (Kikundi cha Wanawake Kilimanjaro Kupambana na Ukimwi) na kile cha wanawake wa Chole mkoa wa Mafia ambacho kimeshajenga kituo cha afya, mafunzo ya watu wazima na chekechea.

Anasema: “Mila hii imekita sana ndani ya fikra za wanajadi. Haiwezi kuondoka haraka; yabidi sote tusaidiane kuwaelimisha taratibu na kufafanua kwanini haina maana yeyote. Muda mwingi nafanya kazi hizi kwa kujitolea. Naamini kusaidia na kulinda maisha ya mwanamke kuliko kutajirika.”

Ukitaka kufahamu zaidi au kusaidiana na Chiku Ali amwandikie barua pepe :

Barua pepe: Chiku.Ali@bergen.kommune.no

Simu +47-9326211.

Makala hii kutoka Freddy Macha

Barua pepe: kilimanjaro1967@hotmail.com

Blogu: http://www.kitoto.wordpress.com

Simu : +44-7961 833040

No comments: