Richmond funika kombe
mwanaharamu apite!
Salehe Mohamed, Tanzania Daima.
SINA haja ya kuanza kutoa hadithi ya kampuni 'hewa' ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, iliyokuwa ikivuna sh milioni 152 kwa siku kwa ajili ya kutupatie umeme wa dharura wakati nchi hii ya 'Wadanganyika' ilipotishiwa kuingia kiza totoro.
Lakini kubwa zaidi linalopaswa kuendelea kukumbukwa katika vichwa vya Wadanganyika hao ni namna kashfa hiyo ilivyowaondoa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na Ibrahim Msabaha (Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Lakini wakati Lowassa akitangaza kujiuzulu wadhifa wake, alisema hakuridhishwa na ripoti iliyotolewa na kamati teule ya Bunge iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza zabuni iliyoipa ushindi kampuni hiyo ambayo tuliambiwa ni hewa na ya kitapeli.
Lowassa alisema kamati haikumtendea haki ya msingi kwa kuwa haikumhoji 'natural justice' lakini alikwenda mbali zaidi pale alipodai kile kilichokuwamo kwenye ripoti kiliulenga 'uwaziri mkuu'
Binafsi niliyaona maneno ya kiongozi huyo kama ni ya mfa maji, lakini hivi sasa naanza kushawishika na kuamini kuwa ni kweli uwaziri mkuu ndiyo uliolengwa katika kashfa ile.
Kwa nini nisiamini hivyo wakati serikali hivi karibuni imetangaza kuwa hakuna hata mtendaji mmoja wa serikali aliyefanya makosa katika mchakato wa kutoa zabuni ya mabilioni ya walipa kodi kwa kampuni hewa ya Richmond?
Kama serikali imemuona mtu hakuwa makini (uzembe) katika utendaji wake wa kazi na kuisababishia nchi hasara ya mabilioni hilo si kosa? Ni kiasi gani cha fedha za walipa kodi zimepotea katika kipindi chote cha uhai wa Richmond?
Kuna tofauti gani kati ya kosa alilolifanya Hosea na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, ambaye amefikishwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya ofisi kwa kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 11?
Mimi si mtaalamu wa sheria lakini kwa utashi wangu na uzoefu wa kazi nilio nao unaniaminisha kuwa uzembe ni kosa linalomfukuzisha mtu kazi, na pia kumfunga sasa iweje watuhumiwa wa Richmond wasafishwe kiasi hiki?
Ni lini viongozi na watendaji wa serikali wataacha unafiki na majungu? Kama Richmond ilikuwa safi kwa nini serikali ilivunja mkataba pamoja na kusimamisha malipo kwa kampuni ya Dowans iliyorithi mikoba ya Richmond?
Hatuhitaji wasomi kutoka Chuo cha Harvard kulikosomeshwa watu kama Barack Obama au Chuo Kikuu cha Yale au Colombia – mavyuo hayo yote ya Marekani - kujua kuwa kilichofanywa na serikali au Bunge ni matumizi mabaya ya fedha za walipakodi kwa kuwa tume iliyoundwa ilitumia mamilioni ya wavuja jasho.
Nani anasema ukweli kati Bunge na Serikali, kwa nini vyombo hivi viwili vinafanya kazi kwa kukinzana tena hadharani kiasi cha kujishushia heshima mbele ya jamii.
Kama Bunge lilichunguza kashfa ya Richmond na kubaini upungufu pamoja na kutoa maazimio, ili yatekelezwe na serikali ambayo sasa imeonyesha wazi kutoyatekeleza nini hatima ya vyombo hivi viwili.
Kwa nini Bunge halionyeshi kukasirishwa au kuchukua hatua dhidi ya taarifa hiyo ya serikali, ambayo si jambo la kuficha limeliaibisha Bunge na kuonekana ni sehemu ya chuki na kulipiziana visasai.
Je, ni kweli Lowassa alionekana tishio kwa serikali ndiyo maana baada ya kujiuzulu kwake Richmond imeonekana safi? Kwa nini watu wasiamini maneno ya Lowassa kuwa yeye ndiye aliyelengwa kuondolewa madarakani na kuchafuliwa jina?
Nina hakika sakata hili la Richmond kwa kiasi kikubwa limeleta majeraha na chuki ndani Chama Cha Mapinduzi (CCM), bungeni, serikalini na katika jamii hususani watu waliokuwa wakituhumiwa kuhusika na hujuma hiyo.
Kwa nini Ninyamaze wakati naona tuendako si salama kwa vizazi vilivyopo na vijavyo? Kwa nini Bunge au serikali viwe uwanja wa mapambano ya mtu mmoja mmoja badala ya kuwa uwanja wa mapambano ya hoja zenye kuijenga jamii?
Sitanyamaza kutoa yangu ya moyoni hadi pale wabunge na watendaji wengine wa serikali, watakapobadili tabia zao na kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kujadili nani kafanya nini na yupo wapi!
Kwa hali inavyoelekea, si ajabu tukasikia Bunge limegeuka kuwa uwanja wa ngumi - si tayari tumeshaanza kusikia viongozi wakifananishwa na mbwa, wakitoa maneno ya 'ovyo ovyo', wengine wakifananishwa na nyoka wa mdimu na mengineyo.
Maneno ya namna hii mwisho wake ni kwa watu wazima kukunjana mashati na kupigana, si ajabu; mbona katika nchi za wenzetu tunaona wabunge na viongozi wanavyotwangana ngumi!
No comments:
Post a Comment