Aponea chupuchupu
kuchapwa viboko 40,
akataa kulipa faini!
Khartoum (Sudan): Mwandishi wa habari Bi. Lubna Hussein (miaka 34) aliyekamatwa Julai kwa kuvaa suruali hadharani, na kuhukumiwa na polisi wa maadili kuchapwa viboko 40, ameponea chupuchupu. Badala yake amehukumiwa kulipa faini ya Dala 200 za Kimarekani na mahakama. Hata hivyo Bi. Lubna amekataa kulipa na kusema yuko tayari kwenda jela kuliko kulipa faini.
Bi. Lubna alikamatwa na polisi wa maadili mjini Khartoum akiwa pamoja na wanawake wengine 12. Wanawake 10 walikubali kuchapwa viboko na kupigwa faini, lakini Bi. Lubna na wenzake wawili walikata rufani na kesi yao kupelekwa mahakamani.
Siku zote kesi hii ilipokuwa mahakamani, wanawake walikuwa wakiandamana huku wakiwa wamevaa suruali, kupinga kushtakiwa kwa Bi. Luban. Kesi hii iliamsha hamasa za wapenda haki za binadam duniani ilipojulikana.
Paragrafu 152 ya sheria za jinai za Sudan, inapendekeza adhabu ya viboko 40 kwa yeyote atakayeonekana hadharani na mavazi yasiyofaa kwa mujibu wa mila na desturi za Wasudani na ni kipengele hiki Bi. Lubna amekuwa akipigania kiondolewe kwenye sheria za Sudan.
No comments:
Post a Comment