Saturday, May 08, 2010

Matukio tisa yaliyomdhalilisha Rais Kikwete 2006 - 2010


Katika kipindi cha Uongozi wa Rais Kikwete kuna matukio kadhaa yaliyotokea na kusababisha minong’ono ,mijadala kwenye vyombo vya haabri na hata sehemu mbalimbali ambapo watu hukaa na kujadili.Matukio haya mengine yamesababisha baadhi ya watu kuhamishwa maeneo yao ya kazi na wengine kupewa maonyo makali.Kubwa zaidi ni mengine kusababisha watu kujadili uwezo wa Rais na watendaji wake katika kuongoza Taifa hili . Yapo matukio mengi lakini makubwa ni nane kama ifuatavyo;


1. Kusaini kwa mbwembwe Sheria ya Gharama za Uchaguzi 2010 yenye vipengele tata vilivyochomekwa kinyemela.

Hivi karibuni Rais alisaini kwa mbwembwe sheria ya gharama za uchaguzi iliyopitishwa na Bunge mwanzoni mwa mwaka huu.Itakumbukwa kuwa sheria hii kabla na baada ya kuwa sheria ilipigiwa kelele sana na wanaharakati pamoja na vyama vya upinzani kuwa ni mbovu haifai.Rais bila kujua kilichomo aliisani kwa mbwembwe zote kwa kuwakaribisha watu toka kada mbalimbali wakiwemo mabalozi. Muda mfupi baadaye ikagundulika kuwa Sheria iliyosainiwa na Rais ilikuwa na vipengele ambavyo havikujadiliwa Bungeni. Wote tumeshuhudia sheria hii ikarudishwa tena bungeni ili kujadiliwa pamoja na kwamba ilishajadiliwa,hili tukio sio la kawaida wala la kupuuzia hasa ikizingatiwa kuwa sheria hii ni sheria nyeti sana. Tukio hili la kituko lilifanyika katika Viwanja vya Ikulu

2. Kujiuzulu kwa Waziri Mkuu-Edward Lowassa

Kwa kuwa Waziri Mkuu anateuliwa na Rais tena wakati mwingine bila kushauriana na mtu kitendo cha Lowassa kulazimika kujiuzulu baada ya kashfa ya Richmond ilikuwa ni pigo jingine kwa Rais. Hii inamaanisha kuwa Rais wetu hayuko makini katika teuzi zake ndio maana anateua watu ambao sio viongozi wasafi wasio na dhamira ya dhati ya kuongoza taifa hili. Hii ni aibu nyingine kwa Rais kwani mtendaji wake mkuu aliyempenda kuliko Mawaziri wote kumuangusha kwa utendaji wake mbovu hivyo kulazimisha kuvunjwa kwa baraza la Mawaziri na kumteua mtu mwigine ambaye hakuwahi kumfikiria kuwa Waziri Mkuu.

3. Mradi wa Malaria

Mtakumbuka kuwa Rais alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Mradi wa Malaria haikubaliki uliofanyika Leaders Club. Baada ya uzinduzi huu uliowashirikisha wanamuziki mbalimbali wa Bongo Fleva wa hapa nchini,mwanamuziki Joseph Mbilinyi(Sugu) aliwatuhumu baadhi ya wasaidizi wa Rais kumtumia Rais kutimiza maslahi binafsi za kibiashara amabpo wasaidizi hao walimpora mradi huu wenye thamani kubwa.Tukio hili lilikanushwa vikali na Ikulu lakini pamoja na hayo limeidhalilisha ikulu na hivyo kumdhalilisha Rais.

4. Gari la Kubeba Wagonjwa

Itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa mwaka huu Rais aligoma kukabidhi gari la la msaada la kubeba wagonjwa baada ya kutokea utata kuhusu halmashauri inayopaswakukabidhiwa gari hilo. Gari hilo lililotolewa msaada na Kampuni ya CMC Automobiles Limited lilipaswa kutolewa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido lakini cha ajabu alifika mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.Tukio hili lilitokea ndani ya Ikulu.

5. Kupokea Hundi yenye Utata

Rais alijikuta kwenye tukio jingine la aibu baada ya picha yake kuchapishwa katika vyombo mbalimbali vya habari ikimuonyesha akiwa anapokea hundi kutoka kwa maofisa wa juu wa benki ya Dunia. Kama mtakumbuka tulionyeshwa Rais akikabidhiwa hundi hiyo ambacho kiasi cha fedha kilichoandikwa kwa maneno,dola za Kimarekani laki mbili kilkuwa tofauti na kile kilichoandikwa kwa tarakimu dola 300,000. Hili lilikuwa ni tukio jingine la aibu kwa Ikulu na Rais wetu kwa ujumla.

6. Daraja la Lugoba

Itakumbukwa kuwa mwaka 2006, daraja la Lugoba ambalo linaunganisha mikoa ya Dares salaam,Tanga, Kilimanjaro na Arusha liliharibiwa na mvua na hivyo kuwa katika matengenezo.Rais alifanya ziara ya kutembelea daraja hilo lakini alipofika alishangazwa na kutokuwepo kwa Waziri mwenye dhamana kwa kipindi hicho ambapo alikuwa ni Basil Mramba ambaye alipaswa kuwemo kwenye ziara hivyo. Inasemekana kuwa Mramba alikuwa hana taarifa kuhusu ziara hivyo.

7. Uzinduzi wa Hotel ya Snow Crest -Arusha

Hivi karibuni Rais alipozindua hotel ya kimataifa ya Snow Crest Arusha iliyojengwa ka gharama ya shilingi bilioni 10 lakini baadaye hotel hiyo ilivunjwa na wakala wa Barabara Tanzania(Tanroads) kwa kuwa ilikuwa imejengwa ndani ya eneo la barabara..Hii pia ni aibu kwa Rais.

8. Sakata la Mahujaji

Mwaka 2007 Mahujaji walikwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kukosa ndege ya kuwapeleka Makka.Rais aliwahoji wasaidizi wake na kujibiwa kuwa tayari ndege imeshaandliwa kwaajili ya kuwasafirisha.Rais alishuhudia baadhi ya Mahujaji hao wakipandishwa kwenye ndege lakini baada ya yeye kuondoka Mahujaji hao walishushwa kwa madai kuwa ndege hiyo ilikuwa na hitilafu. Ilikuwa ni changa la macho kwa Rais.

9. Kuzidiwa Jukwaani/kwenye Mkutano Muhimu

Mwishoni mwa mwaka jana afya ya Rais ilitetereka mpaka kupelekea kushindwa kuhutubia mamia ya waumini wa Kanisa la AICT na wanachi wengine katika uwanja wa CCM Kirumba.Rais alibebwa na watu wa usalama wa Taifa na kupelekwa kwenye chumba cha kumpumzika. Rais pia alizidiwa na kupelekwa kwenye chumba cha mapumziko alipokuwa kwenye mkutano wa Sulivan uliofanyika jijini Arusha. Kwa nchi yeyote ile iliyoendelea Rais hapaswi kuzidiwa anapokuwa jukwaani au kwenye mkutano wowote.Rais ana dakatari anyelipwa vizuri hivyo anapaswa kujua afya ya Rais wakati wote.

Haya ni baadhi tu ya matukio ambayo kwa mtazamo wangu naona yalimdhalilisha Rais na hivyo kutufanya watu tuhoji utendaji wa Rais na Serikali yake kwa ujumla. Na mengine yanakuja kabla hatujaingia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Kutoka Jamii Forums

No comments: