Mchungaji Mnigeria anayetoa huduma za kiroho katika Kanisa la Christ International Church ‘CIC’ lililopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, Samwel Oluseyi Olufemi, ametimuliwa Bongo, Risasi Jumamosi limepenyezewa.
Ilidaiwa kwamba, jitihada za kumtafutia kibali cha ukazi Mtumishi huyo wa Mungu zilianza Februari 26, mwaka huu lakini Machi 30, Idara ya Uhamiaji ilimwandikia barua ya kumtaka kuondoka nchini.
Risasi Jumamosi lilifanikiwa kupata nakala ya barua hiyo iliyoonesha Mtumishi huyo kutakiwa awe ameondoka nchini ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba DN 427223/17 ilieleza kwamba, Idara ya Uhamiaji ilimnyima kibali cha ukazi Mchungaji Olufemu kufuatia kuwepo madai ya kutuhumiwa kuhamahama taasisi za kiroho tangu alipoingia nchini mwaka 2005, hali iliyotafsiriwa kuwa, inaweza kuleta mifarakano ya kidini na kusababisha kuvunjika kwa amani.
Barua hiyo iliyosainiwa na Bw. B.A Shayo kwa niaba ya Kamishina Mkuu wa huduma za uhamiaji ilimtaka kiongozi huyo kuondoka nchini ndani ya siku 30 tangu siku ya kuandikwa kwa barua hiyo.
Licha ya barua hiyo, Mchunga Kondoo huyo alisambaza vipeperushi vilivyoeleza kuwa, Aprili 2, mwaka huu angehubiri katika kanisa lake hali iliyotafsiriwa kuwa ni kukaidi agizo la serikali.
Katika kukusanya ‘data’ Jumapili ya Aprili 4, mwaka huu, Paparazi wetu alifika kanisani hapo na katika hali ya kushangaza, taarifa iliyotolewa na mtumishi wa Mungu, Moses Asajile ilieleza kuwa, Mchungaji Olufemu kasafiri kwenda Nigeria na atakuwepo huko kwa wiki mbili hivyo waumini wamuombee aende na kurudi salama.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilitafsiriwa na baadhi ya waumini kuwa ni sawa na kuwapotosha kwani ukweli ni kwamba, Mchungaji huyo alitakiwa kuondoka nchini mara moja kutokana na kukosa vigezo vya kupewa kibali cha ukazi.
Kutoka Global Publishers
No comments:
Post a Comment