TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
IKULU HAIJAWAZUIA MAWAZIRI KUSAFIRI…
Gazeti la kila siku la Mwananchi la leo, Ijumaa, Mei 21, 2010, limechapisha habari kwenye ukurasa wake wa kwanza chini ya kichwa cha habari, “Serikali Yahaha Uchaguzi Mkuu: Ikulu yazuia mawaziri kwenda nje, yawatuma mikoani kukutana na viongozi wa Dini na Tucta”.
Katika habari hiyo, gazeti hilo linadai kuwa Mawaziri wa Serikali wamezuiwa kusafiri nje ya nchi ili waende katika mikoa mbalimbali, ili wakutane na kuzungumza na viongozi wa dini na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kwa nia ya kuwashawishi viongozi hao kuiunga mkono Serikali.
Tunapenda kuwaarifu na kuwahakikishia wananchi kuwa habari hizo siyo za kweli. Ni uongo. Hakuna waziri yoyote wa Serikali aliyezuiliwa kusafiri nje ya nchi kikazi. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hajatoa agizo la kumzuia waziri yoyote kusafiri nje ama popote kikazi, Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Ali Mohamed Shein hajatoa agizo la namna hiyo, na wala Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda hajatoa agizo hilo.
Kwa hakika, hakuna haja wala hoja ya msingi kwa Serikali kuwatuma Mawaziri ama hata watu wengine wowote kwenda mikoani kuzungumza na viongozi wa kiroho ama wale wa TUCTA.
Kama wananchi watakavyokuwa wanakumbuka, mazungumzo kati ya viongozi wa dini na Serikali yamemalizika majuzi. Yalifanyika rasmi na hadharani pale Hoteli ya White Sands, mjini Dar es Salaam. Tena mazungumzo hayo yalikwenda vizuri na yamemalizika vizuri. Viongozi wa dini wamefurahi sana.
Mazungumzo yenyewe yalifungwa na Mheshimiwa Rais Kikwete, na viongozi wa roho walifurahi kiasi cha kwamba wamependekeza kuwa utaratibu wa kuwa na mazungumzo ya namna hiyo liwe ni jambo la kudumu na yafanyike kila mwaka.
Na Mheshimiwa Rais Kikwete amekubali pendekezo hilo ambako sasa itafanyika mikutano miwili kati ya viongozi wa kiroho na wale wa Serikali kila mwaka. Mkutano mmoja utakuwa kati ya Serikali na kila dhehebu, na ule wa pili utakuwa kama ule uliomalizika White Sands yaani kati ya Serikali na viongozi wote wa kiroho.
Hivyo, kwa sasa Serikali haina sababu ya kuwatuma mawaziri wake kwenda kuzungumza na viongozi wa dini wakati mkutano kati ya pande hizo mbili umemalizika majuzi tu, tena vizuri, kwa kushirikisha viongozi wa kiroho kutoka mikoa yote.
Aidha, mazungumzo kati ya Serikali na TUCTA pia yamemalizika. Mazungumzo hayo yalimalizika Mei 8, mwaka huu, 2010, mjini Dar es Salaam. Haya nayo yamemalizika vizuri na pande hizo mbili zimekubaliana. Lililobakia sasa ni Serikali kuyafanyia kazi makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo kupitia taratibu na michakato mbalimbali ya Kiserikali ukiwamo mchakato wa Bajeti.
Sasa, kama mazungumzo kati ya Serikali na TUCTA yamefanyika vizuri na pande hizo mbili zimekubaliana, Serikali ama Ikulu, ina sababu gani ya kutuma mawaziri kwenda kuzungumza na viongozi wa TUCTA mikoani? Wanazungumza nini tena?
Hivyo, kama tulivyosema hapo juu habari za gazeti la Mwananchi ni habari za uongo. Ni jambo la kusikitisha kuwa gazeti lenye heshima kama Mwananchi nalo limejipa madaraka na mamlaka ya kujenga hoja zisizokuwa sahihi na za uongo dhidi ya Serikali.
Mwananchi ni gazeti linaloheshimika katika jamii. Linapoamua kujiingiza katika shughuli ya kuandika habari za uongo na zisizokuwa sahihi, bila kwanza kuthibitisha habari hizo na mamlaka husika ambazo gazeti hilo linazituhumu, inakuwa ni jambo la hatari sana.
Tunapenda kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kujenga na kuimarisha, na kuchukua kila aina ya hatua kupanua na kuboresha uhuru wa habari na uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Lakini vile vile, Serikali inataraji kuwa vyombo vya habari na manahodha wake wataendelea kuheshimu uhuru huo kwa kuandika habari za kweli na zinazosimamia kwenye misingi ya kweli kweli ya uandishi wa habari ukiwamo weledi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment