Sunday, May 23, 2010



F.C. Internazionale Milano ya Italia au kwa kifupi Inter wamekuwa mabingwa wa Ulaya jana (Champions League), baada ya kuwafunga Bayern Munich ya Ujerumani kwa magoli 2 - 0 kwenye fainali, uwanja wa Santiago Bernabeu, mjini Madrid, Hispania. Magoli yote hayo mawili yalifungwa na Mwajentina, Diego Milito. Mara ya mwisho Inter walichukua ubingwa huo, ilikuwa mwaka 1965.

Ushindi wa Inter unamfanya kocha Jose Maurinho "The Special One" kuweka historia, kwa kuwa kocha wa tatu kuchukua "Champions League" kwa vilabu viwili tofauti. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2004, alipoiwezesha Porto ya Ureno kuchukua Chapions League. Ameweka historia nchini Italia kuwa kocha wa kwanza kuchukua ubingwa wa Italia, kikapu cha Italia na Champions League katika msimu mmoja.

Maurinho anaungana na makocha Ernst Happel na Ottmar Hitzfeld waliomtangulia kwenye heshima hiyo kubwa ya soka duniani. Kwenye mechi ya jana, Maurinho amemshinda mwalimu wake kwenye mambo ya ukocha Louis van Gaal, Mholanzi kocha wa Bayern Munich. Van Gaal na Maurinho waliwahi kufanya kazi pamoja F.C. Barcelona, van Gaal akiwa kocha na Maurinho akiwa msaidizi wake.


 

No comments: