Saturday, May 15, 2010


Wadau, hili la matumizi ya lugha ya kufundishia kwenye elimu ya juu nchini Tanzania, limeanza kujadiliwa toka karne ya 20. Hivi karibu kwenye karne hii ya 21 limezuka tena. Ngoja nitoe mchango wangu kwa uwezo wangu mdogo nilionao...

Nadhani, narudia tena nadhani wengi wanaopendelea Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia, hawaelewi kwa nini tunakazania Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia! 


Wanashindwa kutofautisha kujua Kiingereza kama lugha na ubora wa elimu, ukuaji wa kiuchumi na ongezeko la masoko ya biashara na kazi. Wao kwao vyote hivi ili vifanikiwe, lazima Kiingereza kitumike!

Sisi tunaotaka Kiswahili iwe lugha ya kufundishia, hatuna maana Kiingereza kifutwe kabisa au kisifundishwe! 

Hatuna maana ya kuwa baba na mama wasingumze Kiingereza na watoto wao majumbani kwao. 

Kiingereza kifundishwe, tena kianzie darasa la kwanza, ili watoto wakizoee mapema, lakini lugha ya kufundishia masomo mengine na iwe Kiswahili. Inawezekana nchi zingine na inawezekana Tanzania. Wenye uwezo wa kupeleka watoto wao kwenye shule za binafsi, rukhsa...

Hakuna ubishi kuwa Kiingereza ni lugha ya dunia...hapa hakuna ubishi hata kidogo. Lakini hakuna lugha inayochukua maneno mengi kutoka lugha zingine kama Kiingereza*

Kiswahili kinaweza kabisa kuwa lugha ya kutumia mashuleni na kikaenda sambamba kabisa na lugha ya Kiingereza, Kifaransa, Kihispania kama masomo mengine.

Kujua Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani kama lugha si vibaya hata kidogo. Ni ”advantage” kwa kweli, tena kubwa sanaaaa!!!!

Lakini mtu asinambie ubora wa elimu lazima ufundishwe kwa Kiingereza...Basi ingekuwa ubora wa elimu unatokana na kujua Kiingereza, nusu ya Waingereza wangekuwa wana shahada angalau za kwanza, robo yao wangekuwa na Ph.D, na wangekuwa wastaarabu, kusingekuwa na wabeba maboksi wa Kiingereza, wauaji wabakaji na mafisadi wa Kiingereza!!! Kiingereza ni kama lugha nyingine yoyote ile. Mtu yeyote anaweza kujifunza na kuizungumza, hata bila kufikia vidato vya juu.

Lazima tuwe na waalimu wazuri wa somo la Kiingereza. Waalimu watakaokuwa wanapigwa msasa wa lugha mara kwa mara. Watakaokuwa wanapewa motisha wa kwenda kuzuru hata Uingereza, Marekani, Australia, New Zealand hata Afrika Kusini, kuendeleza upeo wao wa lugha ya Kiingereza. Hapa ninaweza kuwa nina ndoto za alinacha, lakini hakuna binadamu asiye na ndoto ya maisha...!!!!

Mbinu za kufundisha lugha za kigeni zibadilishwe, ziende na wakati. Tusifundishwe kukariri tu kwa ajili ya mitihani, ukimaliza mitihani, baada ya muda mtu umesahau yote.

Watoto wetu wafundishwe kujadiliana tokea chekechea. Wafundishwe ”critical thinking”. Wapewe nafasi ya kuwa nao wanaweza kuzungumza na kujadili jambo na mwalimu, bila mwalimu kumkarapia mtoto kuwa hana adabu, kwa kujadili mada na mwalimu. Waalimu wetu wabadili itikadi na kukubali kuwa wakati mwingine ukiwa huna jibu, unaweza kumwambia mwanafunzi...ngoja nitakupa jibu kamili nitakapocheki ukweli wa swali lako...

Tunavyofundishwa nyumbani ni mbinu za kizamani sana za kufundishia. Kwetu ni mwalimu tu ndiye anayejua...mwanafunzi hujui kitu...mwanafunzi ni wa kufundishwa tu...si wa kujadili mada darasani na mwalimu. Ukifanya hivyo utakiona cha mtema kuni.

Iwekwe mikakati kuwafanya waalimu wote wa shule za msingi wajiendeleze na wafikie angalau kiwango cha diploma ya ufundishaji. Mishahara yao ifikie kiwango cha kumfanya mwalimu akae darasani na kufikria kufundisha na sio kufikiria mradi wa kuongeza kipato!

Kiingereza kama somo kiwe na vitabu vinavyokwenda na wakati. Wanafunzi wahamasishwe wazungumze Kiingereza kama somo. Mitihani ya kuzungumza Kiingereza ”oral exam” iwe ya mara kwa mara. Hii itawafanya wanafunzi wajilazimishe kukizungumza. Tena wanafunzi wa siku hizi wana bahati. Kuna vipindi vingi vya televisheni vya Kiingereza, wakae wasikilize. Kuna mitandao. Waiingie na kusoma.

Hapa Norway, kuwa mwalimu lazima uwe na shahada ya kwanza ya ualimu. Shule nyingi za msingi zina waalimu wenye mpaka shahada za uzamili. Sasa mwalimu huyu huwezi kumlinganisha kabisa na mwalimu wa shule ya msingi aliyemaliza darasa la saba na kwenda chuyo cha ualimu na kupata daraja C la kufundishia. Upeo wao ni tofauti kabisa tunataka, hatutaki...

Isitoshe mwalimu huyu mwenye daraja C mazingira anayofundishia ni duni. Mshahara haumfikishi hata wiki. Hao wanaobisha...wameshawahi kweli kufika Madongo Kuinama wakaona hali duni ya waalimu na shule zetu?

Hivi kweli akili zake atazielekeza kufundisha au atazielekeza kwenye kutafuta hela za kula? Huyu mwalimu unaweza kweli aache miradi yake ya kiuchumi ili aende akakae darasani wiki tatu kujinoa lugha na kuongeza upeo wake? Kwanza hata hiyo nafasi basi atapewa ya kujiendeleza....tunajua fika nchi yetu ilivyo...

Leo Tanzania kuna sehemu...mwalimu mkuu ndiye mwalimu wa kila somo na yuko pekee yake kwenye shule yenye wanafunzi 150.....

Huyu mwalimu hata kama anajua Kiingereza kumshinda Malkia Elizabeth, hawezi kabisa kukidhi haja za hawa wanafunzi wote alionao...

Shule zetu hazina vitabu, hazina nyenzo za kufundishia. Motisha wa waalimu mpaka wa wanafunzi ni mdogo mno...

Narudia: Inawezekana kabisa, wanafunzi waweze kutumia Kiingereza kama somo na huku Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia.

Wapenzi wa Kiingereza wanasema hivi:

”Watanzania tuboreshe Kiingereza chetu ni lazima tukazanie Kiingereza kama lugha ya kufundishia kwa sababu ni lugha ya dunia....Oh...mbona Jose Maurinho kocha wa Inter, Carlo Anchelloti wa Chelsea wanazungumza Kiingereza”...Mbona Wabrazil, Wachina, Wajapani, Wajerumani, n.k. wanajaza madarasa kujifunza Kiingereza? Hakuna ubaya wowote wa kujua lugha ya kigeni. Na ndivyo wanavyofanya hao wenzetu. Lakini hata siku moja huwezi kuwasikia wakisema:

Tuache Kijerumani, Kichina, Kijapani, Kikorea, Kireno kama lugha ya kufundishia na tuanze na Kiingereza.

Watu kama kina Maurinho, Ancelloti na wengineo, wanazungumza Kiingereza kwa sababu wako kwenye mazingira ambayo inawabidi wazungumze Kiingereza. Isitoshe wanapewa mwalimu na darasa ili waijue lugha... Halafu wanazungumza kile kinachoitwa ”Communicative Language” Yaani cha muhimu ni kuelewana kwenye mawasiliano....na siyo umahiri wa usanifu wa lugha...

Kama kweli tunataka tuzungumze Kiingereza kama Waingereza, basi tuache kabisa matumizi ya Kiswahili kwa nchi nzima kama lugha ya mawasiliano na tuanze kutumia mawasiliano yetu kwa Kiingereza kuanzia vijijini na mijini. Je, Watanzania tuko tayari kwa hili? Sidhani.

”Vinginevyo, kama tunazungumza Kiingereza darasani, halafu tukitoka nje ni Kiswahili, hakuna sababu kabisa ya kuendelea kukitumia Kiingereza kama ya kufundishia” alivyojisemea mwalimu wangu, mama Profesa Emeritus, Birgit Brock-Utne (wa Chuo kikuu Oslo)

Mimi ni mwalimu na  asili yangu ni Mtanzania, naishi na kufundisha hapa Norway. Nililetwa Norway nikiwa mdogo kabisa, sikuwa najua Kinorwejiani hata neno moja, sikuwa najua Kiingereza. Nimefundishwa Kinorwejiani nyumbani nilikokuwa nakaa na shuleni. Nimesoma kwa Kinorwejiani kama lugha ya kufundishia na Kiingereza kama somo la lugha. Nimeweza kumudu kukizungumza Kinorwejiani vizuri kwa kuwa nimekulia kwenye mazingira yanayozungumzwa lugha hii kila siku. Ujuani wangu wa Kiswahili ni juhudi zangu mwenyewe, na nimekisoma kama somo Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Trondheim (NTNU = Norges Teknisk-Naturvitenskapelige Universitetet - Norwegian University of Science and Technology)

Nimemaliza na naweza kuzungumza na kuandika Kiingereza sio kwa sababu nimesoma na Kiingereza kama lugha ya kufundishia, la hasha! Kiingereza kilikuwa ni kama somo la lugha.

Nimeajiriwa kufundisha sekondari sio kwa sababu ya kujua Kiingereza, hapana. Nimeajiriwa kwa sababu nazungumza Kinorwejiani na elimu yangu inakidhi kufundishia. Haya makaratasi sikuyapata kwa kufundishwa kwa Kiingereza, bali kwa Kinorwejiani. Makaratasi yangu haya haya niliyofundishwa kwa Kinorwejani, naweza kuyatumia kuyaombea kazi ya ualimu hata Uingereza, mradi tu kama nitaweza kuwadhihirishia kuwa naweza kazi.

Wewe ukija Norway na Kiingereza chako, watu watakusikiliza, halafu watakuuliza unajua kuzungumza Kinorwejiani? Hujui hupati kitu. Labda kwenye fani ya TEKNOHAMA wanakohitaji sana wataalamu.

Tusifanya mchezo na elimu... Tusifanye mchezo kabisa na elimu...wenzetu wanatumia mabilioni ya mapato yao ya taifa kwenye elimu. Shule ngapi Tanzania zina maktaba? Shule ngapi Tanzania kila darasa lina angalau kompyuta mbili? Shule ngapi Tanzania zina madarasa ya kompyuta? Shule ngapi za Tanzania zimefanyiwa ukarabati kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita? Angalau kupakwa rangi tu? Kama zipo kuta basi za kupaka rangi....

Elimu si lugha tu yakufundishia kama vile watu wengi wanavyofikiria, kuna vingi vinavyofanya elimu iwe bora.

Tanzania inatumia asilimia ngapi ya kipato cha taifa kwenye elimu ukilinganisha na matumizi ya JWTZ? Matumizi ya JWTZ na ulinzi ni maradufu na matumizi ya elimu.


Wajapani, Wakorea, Wajerumani, Wanorwejiani na wote wanaotumia lugha zao kama lugha za kufundishia, wanatoa pia kipaumbele lugha za kigeni kama Kiingereza na zinginezo. 

Hapa Norway wanafunzi wenye asili ya kuzungumza Kiswahili, wanaruhusiwa kufanya mitihani yao yote ya vidato kwa lugha ya Kiswahili kama sayansi jamii, hesabu, maarifa, n.k. kama wakitaka. Sio kuifanya kwa lugha ya Kiswahili, mitihani yenyewe inakuwa imetungwa kwa Kiswahili!!!!!

Nasema hivyo si porojo tu, huwa nasahihisha kati ya mitihani 8 hadi 13 kwa mwaka. 

Wanorwejiani wanafundishwa kwa lugha yao, pamoja na kuwa kila kukicha wanatohoa maneno mapya na kuifanya lugha yao kuendelea. Tuliosoma vyuo vikuu vya hapa tunajua kuwa mpaka leo, vitabu vingi vinavyotumika hapa Norway vyuoni ni vya Kiingereza. Hii haiwazui kabisa kuwafundisha wanafunzi wao kwa lugha ya Kinorwejiani, huku wakisoma vitabu kwa Kiingereza.


Lugha kama si yako, huhitaji kuizungumza kama mwenye asili ya lugha. Kinachotakiwa ni kile kinachoitwa, lugha ya mawasiliano (communicative language). Nikizungumza hata kama nikiboronga, la muhimu ni kama umenielewa. Watanzania wengi hatushindwi na hili la lugha ya mawasiliano.

Wanaosema: oh...Wakenya...oh..Wanaijeria...oh...Waafrika Kusini...hivi kweli umeshamsikiliza Mnaijeria anavyozungumza Kiingereza ukamwelewa moja kwa moja? Si wanazungumza kama wanazungumza Kiigbo, Kihausa, Kifulani, Kiyoruba n.k. ...kama hujasikia vizuri, kuanzia sasa wasikilize kwa makini.


Utafiti wa kisayansi, unaonyesha kuwa lugha yoyote ile inazidi kukua kwa kufundishwa na kutumika kwenye fani na nyanja zote za jamii.

Kwani hata kama hiyo lugha (mathalani Kiswahili) haina misamiati, ikiwa inafundishwa; vitengo, idara na taasisi zinazohusika zinalazimika kutohoa maneno mapya kila wakati ili lugha iweze kutumika kufundishia.

Tukisema kuwa ili Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia, lazima kijitosheleze kwanza kwenye sayansi na teknolojia, tunajidanganya wenyewe.

Sayansi na teknolojia haisimami kukisubiri Kiswahili kipate misamiati kwanza. Tena sayansi na teknolojia inakwenda kasi sasa kuliko wakati mwingine wowote ule. Muda unavyokwenda na kasi inazidi. Sasa Kiswahili hakitumiki halafu tunasema tungoje. Mambo mangapi yanabadilika kila siku kweli tutayafikia kama hakitumiki kwenye sayansi na teknolojia?

Kiingereza chenyewe kinakua kila siku kwa sababu ya kufundishwa na kutumika kwenye nyanja zote zikiwemo sayansi na teknolojia, kinakua pia kwa kuazima maneno toka lugha zingine**. Watu wanaosema Kiswahili hakijitoshelezi kama lugha ya kisayansi, hawa sijui huwa wanaishi dunia ipi au karne gani?

Miaka 10 tu iliyopita hakukuwa na neno kama iPhone, HTC, BlueBerry, Google, iPad, hata Kiingereza chenyewe inabidi kikimbie ili kuifikia sayansi na teknolojia na kwa Kiingereza inawezekana kwa kuwa kinatumika kwenye nyanja mbali mbali za kijamii, kuanzia mitaani hadi kwenye sayansi na teknolojia.
 
Mbona HIV na AIDS ilipoanza hakukuwa na neno VVU (Virusi Vya Ukimwi) na UKIMWI? Huu ni mfano kidogo tu. Ipo mingi. Wataalamu wa lugha walikaa na kuyatohoa. Sasa kwanini ishindikane kwa maneno mengine kama kweli tunataka kiwe cha kitaalamu na kisayansi?

Microsoft na Google wanajua kuna soko Afrika Mashariki na ya kati na wanajitahidi kweli...kuweka bidhaa zao kwa lugha ya Kiswahili, japo hawajafikia kiwango kikubwa na cha ufanisi mzuri, lakini wako njiani. Leo unaweza kufyonza ”apps” za Kiswahili na kuweka kwenye iPhone. Kwa nini? Kwa sababu, Apple na watafutaji masoko wanaona kuna soko kwa watumiaji wa Kiswahili na hata brauza yao (Apple) wameipa jina la Kiswahili, yaani Safari...

Kama hao ambao si watumiaji wa Kiswahili kila siku wanaona umuhimu wa Kiswahili, kwa nini sisi watumiaji wa Kiswahili kila siku tusilione hili?

Tusifanye  kama wakati flani tulipoambiwa kuwa:

"Lazima tuweke umeme Tanzania nzima ndipo tuwe na televisheni"

Mbona mpaka leo hakuna umeme kila kijiji? Tungesubiri mpaka kila kijiji kiwe na umeme, leo hii kweli tungekuwa na stesheni za televisheni Tanzania?

Hebu angalia ubora wa stesheni za televisheni miaka 10 iliopita nchini Tanzania na leo...tumetoka mbali, basi na Kiswahili ni hivyo hivyo, tusisubiri, wakati ni huu.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema:

”Kama Kiingereza ni Kiswahili cha dunia, basi Kiswahili ni Kiingereza cha Afrika” Mwalimu alikuwa na maana yake hapa.

Je, inawezekana?

Jibu: NDIYO!

Tusisahau kuwa lugha pia ni sehemu ya utamaduni, kiungo muhimu kwa utamaduni wa Mtanzania ni lugha ya Kiswahili. Kwani Tanzania tuna makabila takriban kama 128 hivi na kila kabila lina mila, desturi na utamaduni wake.

Tamati naishia hapa...

Tausi Usi Ame Makame
Sauda, Norway

6 comments:

Omari Guy Agallo Chichi said...

Tausi,

Swadakta!

Wee Tausi umeolewa? Manaake naona kichwa chako kinachemka kweli!

Kama hujaolewa au huna mshkaji. Mie nipo.

omyguyagallochichi@yahoo.co.uk

Naona utanifaa. Natafuta mwanamke atakayenichallenge kila siku kwenye mazungumzo na maisha

Weee Tausi kiboko!

Anonymous said...

Tausi,

wewe umetetea hoja zako kielimu. Sio kama wale wanaosema tu...bila kutetea hoja zao...

I salute you!

Keep it up!

Chidozie said...

Tausi...

Go girl....

Splendid, marvellous piece of writing on the use of Kiswahili as a lingua-franca...

Woooooo weeeeee !!!!!

Unajua umenishawishi hata mimi niliyekuwa mguu ndani, mguu nje...

Sasa nimepata mwanga angalau wa kwa nini Kiswahili kinaweza kuwa lugha ya kufundishia

Anonymous said...

Tausi mtoto wa Kitanga,

Upo?

Umeandika vizuri mno!

Anonymous said...

Asante dada yangu
bora urudi bongo uwe waziri wetu
wa utamaduni
pamoja na kukulia nje bado unawashida mawaziri , wabunge wengi ambao wamesoma bongo kuanzia msingi hadi manzese, lakini wakitoa hotuba wanachanganya na kiingereza ili tujue eti wasomi.
cha msingi anze rais mwenyewe kila akija ulaya atoe hotuba za kiswahili

Anonymous said...

Doh!

Kajiunge na siasa, upate uwaziri wa elimu...wizara hiyo inafaa mtu kama wewe.