Anguko La
CCM Arumeru:
Tafsiri
Yangu
Ndugu zangu,
Unaweza kuwatawanya watu kwa mabomu , lakini kamwe, mabomu hayawezi kuitawanya mioyo ya watu yenye kutaka mabadiliko.
Habari kubwa usiku wa kuamkia leo ni anguko la CCM kule Arumeru Mashariki kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha Ubunge.
Tafsiri yangu;
Kuna wakati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alipata kutamka; " CCM
haina hati miliki ya kutawala". Mkapa aliusema ukweli wake ambao kwa
bahati mbaya hupata tabu kuusimamia. Na hakika, idadi ya Watanzania wenye
kutaka mabadiliko inazidi kuongezeka. Na katika siasa za nchi hii
ukiona wanawake watu wazima wanashiriki mikutano ya kampeni ya wapinzani, basi,
ujue ni ishara ya mabadiliko yanayokuja.
Na ukweli mwingine ni huu; vijana wengi zaidi wamekuwa mstari wa mbele katika kutaka mabadiliko hayo. Kimsingi Arumeru Mashariki wamechagua mabadiliko. Na si kwamba Chadema ni chama bora na makini sana, la hasha, Watanzania wengi zaidi vijana wanaonyesha kuichukia CCM. Miongoni mwao ni Wana-CCM. Kiukweli, mvuto wa Chama Cha Mapinduzi kwa Watanzania na hususan vijana unazidi kupungua.
Na ajabu ya matokeo ya Arumeru?
Katika hali isiyo ya kawaida, kuna Wana- CCM
waliyoyapokea kwa furaha matokeo ya chama chao kushindwa Arumeru. Tafsiri yake? Ni
kushamiri, si tu kwa makundi ndani ya chama hicho, bali, hofu ya kutokea kwa
mpasuko ndani ya chama hicho katika mbio za kuusaka Urais ifikapo mwaka 2015.
Kitakachotokea sasa ndani ya chama hicho ni ‘ Witch hunting’- kutafutana uchawi. Bila shaka, kuna maswali yatakayoulizwa. Moja kubwa ni hili; kimeshindwa chama au mgombea? Na msukumo wa swali hilo ni katika kumtafuta mchawi na kukitenganisha chama na mgombea katika ‘Anguko la Arumeru’. Huo utakuwa ni mwendelezo wa ‘ Vita vya Panzi’ ndani ya CCM. Lakini, katika siasa, kuna wanaoamini pia, kuwa wakati mwingine kuna lazima ya kuwepo kwa ‘ Vita vya Panzi’ ili kujitenganisha na kumbikumbi.
CCM ifanye nini?
Jibu; ifuate njia ya Dr Harrison Mwakyembe
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kata ya
Ipinda hivi majuzi Dr Mwakyembe alitoa kwa watu wake
kauli ya ‘ Kichifu’ na iliyojaa hekima na busara. Alisema; “ Mimi sikubaliani
na mtu yeyote anayesema kitu cha kwanza ni chama chako…. Hapana, mimi kitu
cha kwanza kwangu siyo CCM , cha kwanza mimi ni Mtanzania, cha pili
ndio tunaingia kwenye vyama. Mtu anayekimbilia chama kuwa cha kwanza hivi hicho
chama kingetokea wapi kama siyo taifa?”. ( Dr Harrison Mwakyembe, Nipashe,
Machi 31, 2012)
Na nilimwona na kumsikia Dr. Mwakyembe akiyasema hayo kwenye runinga. Umati ule uliomshangilia Dr Mwakyembe ulikuwa wa wananchi bila kujali itikadi zao. Kulikuwa na Wana -Chadema pia, na kiongozi wa Chadema alipewa kipaza sauti kuongea kumkaribisha ‘ Chifu Mwakyembe’ aliyerudi nyumbani na mtazamo mpya wa kizalendo.
Kuifuata njia ya Mwakyembe itawasaidia CCM kurudisha umaarufu wao. Maana, moja ya sababu za wananchi walio wengi kuichukia CCM ni hulka yake ya kuwabagua wapinzani na kuwaona ni watu wasiofaa kushiriki uongozi wa nchi.
WaTanzania wengi sasa wanatambua, kuwa si kweli wapinzani ni watu wabaya. Ni maadui. Kwamba watasababisha vita na vurugu. Wananchi wameona pia kazi njema inayofanywa na upinzani. Ghiliba hii ya CCM kuwachonganisha wapinzani kwa wananchi imepitwa na wakati. Badala yake, inachangia kupunguza kura za CCM.
Na CCM isipobadilika sasa, na Chadema ikabaki kama ilivyo sasa bila kusambaratika, basi, CCM itakuwa na wakati mgumu sana ifikapo 2015, maana, kuna ‘Jeshi kubwa’ la vijana linalojiandaa na kushiriki uchaguzi wa 2015. Jeshi hili linaundwa na vijana wengi wasio na ajira wala hakika ya maisha yao ya kesho. Wanaiona CCM kama sehemu ya matatizo yao. Wana kiu ya kumpata mkombozi.
Na wanafunzi hawa wa Shule za Kata wamegeuka kuwa ‘ agitators’ wazuri wa mabadiliko. Ikumbukwe, shule za kata ziko vijijini. Siku hizi hata waliokuwa wakiitwa ‘ wajinga’ wa vijijini wamepata walimu wa kuwafungua macho. Watoto wao wenyewe wanaosoma au waliomaliza shule za kata na kubaki vijijini kwa vile hata uwezo wa kujisomesha elimu ya juu hawana. Hawa hawana mapenzi na CCM.
Na katika vijana mia moja hii leo, utapata kazi kubwa kuwapata 20 wanaoipenda CCM. Huu ndio ukweli wa hali halisi. CCM ibadilike na kuwa chama cha kisasa kilicho tayari hata kuongoza nchi pamoja na wenzao wa upinzani. Yumkini jitihada za CCM kuangamiza upinzani zaweza kuwa na madhara makubwa endapo CCM itapata bahati mbaya ya kuondolewa madarakani 2015. Maana, anguko hilo laweza pia kumaanisha kifo cha chama hicho.
CCM haipaswi sasa kufikiria mikakati ya kuangamiza upinzani ili watawale daima. Dhana ya ’ CCM Daima’ ni ndoto iliyopitwa na wakati. Katika Tanzania ya sasa kuna wengi wenye kuombea kubaki hai na kushiriki kuzifuta ndoto kama hizo.
CCM ya sasa inapaswa kupanga mikakati ya
kuendelea kuongoza dola huku ikishirikiana hata na wapinzani. Ingawa hata huo
ni mtihani mgumu wenye kukihitaji chama hicho kuwa na watu makini zaidi badala
ya waendekeza fitina na majungu.
Na hii ni tafsiri yangu.
Maggid Mjengwa,
Iringa,
Tanzania
+255 788 111 765
+255 788 111 765
No comments:
Post a Comment