Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kutoka kushito: Yoweri Museveni (Uganda), Mwai Kibaki (Kenya), Paul Kagame (Rwanda), Jakaya Kiwete (Tanzania) na Pierre Nkurunziza (Burundi)
Na Ashura Mohamed-Arusha
Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajiwa kukutana Arusha, Tanzania hii leo,
katika mkutano maalum utakaojadili pamoja na mambo mengine, mapendekezo ya
maombi ya nchi ya Sudan Kusini, kujiunga na jumuiya hiyo.
Nchi zote tano za Kenya, Uganda,
Tanzania,Rwanda na Burundi zinatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa siku moja
utakaofanyika katika hoteli ya Ngurdoto, nje kidogo ya mji wa Arusha.
Taarifa zilizopatikana toka ofisi ya
EAC,Idara ya Mawasiliano na Masuala ya Umma imesema mkutano huo pia unatarajiwa
kujadili agenda nyingine nne.
Maombi ya Sudani Kusini yatafikiriwa
ikiwa ni miezi karibu mitano baada ya maombi ya Jamhuri ya Sudani kukataliwa
kwa madai ya kutokidhi vigezo vilivyoanzisha mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Mkataba huo unaeleza wazi kwamba
nchi yoyote inayotaka kujiunga na EAC, sharti iwe imepakana na moja kati ya
nchi tano wanachama wa jumuiya hiyo.
Hata hivyo maombi ya Sudani Kusini
yanakuja wakati ambapo ipo katika hali ya uwezekano wa kuingia katika vita
kamili na jirani yake, Sudani Kaskazini, hoja ambayo huenda pia itatupiwa jicho
na kikao hicho cha Wakuu wa EAC.
Nchi hiyo mpya kabisa barani Afrika
na duniani kwa ujumla, ilipatikana Julai 1, 2011 baada ya mwongo mmoja wa vita
na Sudani Kaskazini.
Hoja nyingine ambazo zinatarajiwa
pia kujadilia katika mkutano huo ni pamoja na uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu mpya
wa EAC, atakayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, kuchukua nafasi iliyokuwa
inashikiliwa na Beatrice Kiraso wa Uganda ambaye kamaliza mkataba wake wa kazi
na pia kufikiria kumwongezea mkataba wa kazi, Naibu Katibu Mkuu,
anayeshughulikia Uzalishaji na Sekta ya Jamii, Jean Claude Nsengiyumva kutoka
Burundi.
Mkutano huo wa Wakuu wa EAC,
umetanguliwa na mkutano maalum wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa EAC
No comments:
Post a Comment