Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dr. Jakaya Kikwete, Jumamosi 30 Juni 2012. Kuhusu wazamiaji, mgomo wa
madaktari na kipigo cha Dkt. Ulimboka
Ndugu Wananchi,
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha
kumaliza nusu ya kwanza ya mwaka 2012 salama. Kwa kutumia utaratibu wetu
wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili.
Jambo la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili
ni la mgomo wa madaktari.
Usafirishaji
Haramu wa Binadamu Nchini
Ndugu
Wananchi;
Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za
tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43 za watu
wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego,
Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja na maiti
hao, walipatikana watu 84 wakiwa hai lakini wote wakiwa
wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa
kuwasafirisha watu hao hadi Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa
Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika
Kituo cha Kati cha Polisi, Dodoma. Maiti 22 zilipelekwa
Dodoma na 21 zilipelekwa Morogoro kuhifadhiwa.
Taarifa
zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu hao ni raia
wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye Afrika ya Kusini
ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi Marekani na Ulaya. Kwa
mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza miezi mitano iliyopita. Mwezi
mmoja waliutumia Ethiopia na miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa
Arusha ambako walipakiwa kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini
ikaishia Chitego. Lori walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo
kusababisha vifo kwa kukosa hewa.
Tukio
la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si
la kwanza kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika kipindi cha takriban
miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji haramu kuingia
nchini. Kwa mfano, kati ya mwaka 2005 na hivi sasa jumla ya wahamiaji
haramu 19,683 wamekamatwa. Karibu wote wameshaondoshwa
nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500 tu magerezani
wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao. Wengi wa watu hao
wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na Bangladesh.
Wahamiaji
haramu wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo rasmi. Wapo
wanaotumia nchi kavu hasa kupitia mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na
Tanga. Na, wapo wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za Pemba, Unguja na
za mikoa ya ukanda wa Pwani ya Tanzania Bara yaani Tanga, Pwani, Lindi na
Mtwara.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji nchini kuhamia
bali wao ni wapita njia tu. Wanaelekea Afrika ya Kusini ambako
wameahidiwa kuwa watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na Ulaya.
Watu hao pia wamethibitisha kuwepo kwa watu maalum wanaojihusisha na usafiri
wao tangu nchi watokako na zote wanazopitia mpaka kule waendako. Aidha,
wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao ili wawasafirishe na hakika si kiwango
kidogo. Kwa jumla ni kwamba hili si suala la uhamiaji haramu bali ni la
biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
Ndugu
Wananchi;
Kufuatia
vyombo vyetu vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa ndipo
wasafirishaji walipobuni njia za kuwasafirisha kama mizigo. Makontena,
malori yaliyofunikwa nyuma na matenki ya mafuta na ya maji yamekuwa yanatumika
kwa ajili hiyo. Usafiri wa aina hiyo ndiyo uliosababisha vifo
vilivyotokea Dodoma tarehe 26 Juni, 2012 na vya watu 21 vilivyotokea
mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile vya watu 12 vilivyotokea
katika matukio mawili ya Mkoa wa Mbeya, mwezi Mei, 2012.
Ndugu
Wananchi;
Tarehe
27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini
kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara hii haramu na hasa mbinu
mpya inayotumiwa na wasafarishaji. Nilitoa pongezi kwa vyombo vya dola
kwa kazi nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli za biashara hii haramu hapa
nchini. Tulielewana kuwa waendelee kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la
kukomesha kabisa biashara hii.
Niliagiza
pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006 kushughulikia ujambazi sasa
kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili tatizo hili. Aidha, kwa pamoja
tulikubaliana kuwa nchi yetu ishirikiane na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi,
Msumbiji na Afrika ya Kusini kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa
sheria. Tayari nimeshaanza kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi
hizo kuhusu ushirikiano huo. Nashukuru wote wameafiki nchi zetu
zishirikiane kwa pamoja kuvunja mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii
haramu na inayodhalilisha utu wa mwanadamu.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya Chitego na Mkoka
kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu wameonesha uzalendo wa hali ya
juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya jambo lenyewe, lakini pia wameonesha utu
kwa kuwajali wageni waliokumbwa na janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa
wa Dodoma na Morogoro ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa
kulishughulikia tatizo hilo kwa umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana
na ushirikiano ulioonyeshwa na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika
kushughulikia suala hili.
Mgomo wa
Madaktari
Ndugu
Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa.
Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee
tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa unaendelea wakati ule
pamoja na kuelezea chimbuko la mgomo na hatua iliyokuwa imefikiwa, nilielezea
mazungumzo yangu na viongozi wa Chama cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa
Jumuiya ya Madaktari. Nilitoa taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha
mgomo na watarudi kwenye meza ya majadiliano na Serikali. Siku ile pia
nilielezea matumaini yangu kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi
yetu. Bahati mbaya matumaini yangu hayo hayakuwa na hivi sasa
tunashuhudia tena wagonjwa wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa sababu ya
kukosa huduma wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma tena.
Ndugu
Wananchi;
Kama
walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi kwenye
mazungumzo na Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu, Kitengo cha
Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini, Namba 6 ya
mwaka 2004. Chama cha Madaktari na Serikali walifika katika Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi (Commission for Mediation and Arbitration) kwa ajili ya
majadiliano. Kwa pamoja na kwa ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba
Tume hiyo iwape fursa ya kuzungumza wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo
wataenda kusajili makubaliano yao. Tume ikawakubalia. Ni vizuri
ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe 8 Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha
Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande
mbili.
Ndugu
Wananchi;
Kati
ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya
majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari. Katika mazungumzo
hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa. Mambo hayo ni haya
yafuatayo:
- Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya mshahara.
- Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.
- Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30 ya mshahara.
- Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara.
- Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari.
- Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa mwezi.
- Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
- Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
- Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
- Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
- Huduma za afya ziboreshwe nchini.
- Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Ndugu
Wananchi;
Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na
kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba.
La kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi
kazini. Serikali ilieleza kuwa upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa
Utumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali
fedha za kununulia magari au pikipiki, samani na matengenezo ya magari.
Ilikubaliwa kuwa madaktari waitumie fursa hiyo.
Jambo la
pili, ni kuhusu
madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya. Jambo hili lilikubaliwa na
Serikali na Wizara ya Afya imekwishachukua hatua za utekelezaji wake.
Jambo la
tatu, ni kuhusu
hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya
Afya. Kwa pamoja walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya mamlaka ya
Kamati yao ya pamoja, waziachie mamlaka husika za uteuzi. Uongozi wa juu
wa Wizara umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la
kustaajanisha hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja
walikataa kumuona. Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza
na Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya mafanikio
Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi
kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje. Walikubaliana mambo
mawili. Kwanza, kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe.
Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie maadili ya kazi zao na kukataa kutoa
rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi. Pili,
walikubaliana kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa
nchini. Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali.
Nililieleza hili mwezi Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge
baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu.
Tumeiongeza
sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006
hadi shilingi trilioni 1.2mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya
miundombinu na elimu. Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na
wataalamu wa afya. Kazi inaendelea katika hospitali za
Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali ya Muhimbili. Hospitali hiyo ilivyo
leo sivyo ilivyokuwa miaka sita nyuma. Na kazi inaendelea hasa katika
maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa nje. Matunda yake yanaanza kuonekana
kwa upande wa figo, moyo, kinywa na mipango inaendelea kwa upande wa ubongo na
mishipa ya fahamu. Tunaendelea kuimarisha mafunzo ya madaktari na
madaktari bingwa, yote kwa nia hiyo hiyo. Hivi sasa Chuo Kikuu cha
Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua wanafunzi wengi zaidi ya ilivyokuwa siku
za nyuma na makazi mapya ya chuo yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua wanafunzi
wengi zaid. Mwaka 2005 tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka
huu tunao 520.
Ndugu Wananchi;
Jambo la tano ambalo
pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari waliofukuzwa. Hawa ni
wale Internswaliokuwa wamerudishwa Wizarani kutoka Muhimbili na
kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na Lugalo. Hili ni
jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa wamerudi Muhimbili.
Jambo la sita ni
kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu kuboresha huduma
ya afya. Mapendekezo hayo yalihusu kutathmini sera na mpango wa afya ya
msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya bajeti ya Serikali,
kuwepo na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na kuboresha viwango vya ubora
wa madaktari na kadhalika. Serikali imeyaafiki mapendekezo hayo na
yatafanyiwa kazi.
Jambo la saba, ambalo
pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi wa
maiti. Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni. Hata hivyo, Serikali
imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi kufikia shilingi
100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa
wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi;
Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi
fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo. La kwanza ni suala
la kufanya kazi katika mazingira hatarishi. Serikali imekubali hoja ya
kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira
hatarishi. Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada zote za afya
watapatiwa chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na fedha
zimetengwa katika bajeti ya 2012/13.
Aidha, Serikali imeeleza dhamira ya
kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa watumishi wa umma wanaostahili.
Utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira
hatarishi ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike.
Madaktari wamekataa hili la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama
wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara
moja.
Jambo
la pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi.
Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za kuishi.
Aidha, imeeleza mpango ulioanza wa kujenga nyumba 700 za madaktari
kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi wa nyumba 90 unaendelea, 50 katika
mkoa wa Mtwara na 40 katika mkoa wa Rukwa.
Kwa maeneo ambayo madaktari
wanalipwa posho ya pango Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa
mujibu wa taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa
nyumba. Jambo hilo limekataliwa na Madakari na kutaka lazima walipwe asilimia
30 ya mshahara kama posho ya nyumba. Serikali kwa upande wake
imeona vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa wafanyakazi
wengine wote wa umma.
Jambo lingine ambalo
lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya kazi katika
mazingira magumu. Pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya
maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma hivyo hatua
zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali wajibu wa kuweka
utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika maeneo hayo. Kwa ajili
hiyo, Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu namna ya kuwasaidia watumishi
hao kupunguza makali ya maisha katika kila eneo badala ya kutegemea posho peke
yake.
Kuhusu posho, Serikali imeeleza
kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi
wa kuainisha mazingira husika, kutambua watumishi waliopo na gharama zake.
Madaktari hawajakubali kusubiri
zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa.
Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo
yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho kulingana na mazingira
halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo.
Ndugu Wananchi;
Mambo mawili hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili. Jambo la kwanza ni posho ya kuitwa kazini
(on call allowance). Kwanza sina budi kueleza kuwa Serikali imekubali
kuongeza posho hiyo. Tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi
10,000/= hadi shilingi 25,000/= kwa daktari bingwa
(Specialist), shilingi 20,000/= kwa dakari mwenye usajili wa
kudumu (Registrars) na shilingi 15,000/= kwa madaktari
waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns).
Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa.
Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza
walipwe asilimia 10 ya mshahara. Ugumu wa kukubali
pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini.
Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa
kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa. Hili haliwezi kuwa
sahihi kufanya. Linaweza kuwafanya baadhi ya madaktari kutokutimiza
wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale pale.
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu
mshahara wa kuanzia kazi wa daktari. Madaktari wanataka uwe shilingi
3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi.
Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia
15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote
wa umma katika mwaka huu wa fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao,
daktari ataanzia kati ya shilingi 1,100,000/= na 1,200,000/= kutegemea
kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na
wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu
Wananchi;
Huo
ndiyo mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na matokeo ya
mazungumzo yenyewe. Katika kikao cha sita kilichofanyika tarehe 30 Mei,
2012, upande wa Chama cha Madaktari ulisema kuwa kwa vile hoja ya nyongeza ya
mshahara haina mabadiliko hawakuona haja ya kuendelea na majadiliano mpaka
watakapowasiliana na wenzao. Waliahidi kutoa taarifa ndani ya wiki mbili.
Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi
ambaye ndiye kiongozi wa majadiliano kwa upande wa Serikali, kuwa Madaktari
wameikataa taarifa na ufafanuzi waliopewa kutoka Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu
Wananchi;
Baada
ya majibu yale ya madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na Madaktari
walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro umekosa usuluhishi
kama sheria inavyotaka. Kwa pamoja pande zote mbili zilikubaliana suala
hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi. Wakati pande zote
zinasuburi mgogoro huu kufikishwa ngazi hiyo ya juu, upande wa Madaktari
ukatangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia saa sita ya usiku tarehe 23 Juni,
2012. Hatua hiyo haikustahili kwani suala lenyewe halijafika mwisho wa kushughulikiwa
kwa mujibu wa Sheria za Mahusiano ya Kazi nchini.
Ndugu
Wananchi;
Tarehe
22 Juni, 2012, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu Kitengo cha
Kazi kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la muda
kufanywa. Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa mgomo
usitishwe. Juhudi za kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na viongozi
wengine wa MAT hazikufanikiwa, Ofisi ya MAT ilikuwa imefungwa na simu zote za
viongozi wa MAT zilikuwa zimezimwa. Hatimaye tarehe 25 Juni, 2012,
alipatikana na kupewa amri hiyo ya Mahakama. Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt.
Mkopi alifika Mahakamani ambapo alikana kuwa yeye hahusiki na kuitisha huo
mgomo lakini hakumtaja aliyehusika. Pamoja na rai hiyo, Jaji alimuamuru
Rais wa MAT akawatangazie wanachama wake kusitisha mgomo. Dkt.
Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi leo na mgomo umekuwa unaendelea kinyume cha
Sheria.
Ndugu
Wananchi;
Wagonjwa
wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali kisheria
ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari.
Viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika mgogoro na
Mahakama na waajiri wao isivyostahili. Ni vyema viongozi wa Madaktari na
madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia
kiongozi wao mkuu amekana Mahakamani kuwa hahusiki nao. Madaktari lazima
watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka hatarini. Mfanyakazi ana kinga
ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki mgomo unaokubalika kisheria.
Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia, hawana cha
kiwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha yao kwani
hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali.
Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa kuboresha
mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu kwa maelekezo ya
Ilani ya Chama Tawala (CCM). Tumeitekeleza kwa vitendo sera hiyo, hata
hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa nia yangu njema tu pekee haitoshi, lazima uwezo
wa kufanya hivyo uwepo. Kwa kulingana na uwezo uliopo, tumeendelea
kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi hatua kwa hatua tangu tuingie
madarakani. Tumefanya hivyo kwa jumla kwa wafanyakazi wote na kwa kada
mbalimbali za watumishi wa umma.
Miongoni
mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za Serikali ni madaktari na
watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya. Tena nadiriki kusema
madaktari tumewapa upendeleo mkubwa kuliko watumishi wengine wa umma.
Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na
Serikali kwa asilimia mia moja wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine
hawako hivyo.
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi 178,700/=,
mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=. Tuliendelea
kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi957,700/= wanazolipwa
sasa. Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma
nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata
shilingi 446,100/=.
Tunafanya
hivyo kwa kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii na
ukweli kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari
nchini. Lakini inaonekana juhudi zetu zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu
Wananchi;
Sina
budi kusisitiza kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo tulio nao
wa kulipa. Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa kuwalipa
mshahara wa kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na posho zote zile.
Tukifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi 7,700,000/=.
Kwa hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu
tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana
na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini
bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na kwenda kwa muajiri
anayeweza kumlipa kiasi hicho. Nasi tutamtakia kila la heri. Hana
sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa
mshahara huo. Isitoshe, hana sababu ya kuendelea kuwa na mgogoro na
mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka. Huna sababu ya kumpa
usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya kujieleza au kukuachisha kazi.
Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na kuzijibu. Kwa nini upate
usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali
ndani ya saa 24. Jiepushe na yote hayo kwa kujiondoa mwenyewe.
Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana jinsi bali kukuondoa kazini maana
unakwenda kinyume na sheria za kazi na maadili ya kazi ya udaktari.
Mamlaka
za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya hivyo kwa wote
wanaoendelea kugoma. Najua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna
manun’guniko ya kuonewa. Hivyo, mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya
hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na
huyo ajae awe na mahali pa kuishi. Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae
daktari ambae hayupo kazini na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi ya watumishi wa
umma wakiwemo madaktari iko wazi. Tumekuwa tunafanya hivyo, na
tutaendelea kufanya hivyo kulingana na uwezo wa kibajeti. Ni vyema
watumishi wa umma wakatambua kuwa hatuwezi kutumia fedha zote au kiasi kikubwa
mno cha pesa za umma kulipana mishahara. Tukifanya hivyo, Serikali
itashindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi ambao ndiyo wengi na wanastahili
kuhudumiwa. Hata hizo huduma za afya tunazosema ni duni tuziboreshe,
hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu kubwa ya pesa za Serikali kuwalipa
mishahara wafanyakazi.
Hivi
sasa matumizi ya mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya
Serikali. Kiwango hicho ni kikubwa mno. Uwiano mzuri ni kuwa na
matumizi ya mishahara yasiyozidi asilimia 35 ya bajeti na asilimia
65 zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya
wananchi na taifa. Sisi tumezidi kwa asilimia 13.
Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio wengi.
Suala la Dkt. Steven Ulimboka
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu,
napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote kuelezea masikitiko yangu makubwa
na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dkt. Steven
Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni, 2012. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila
na desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo. Nimeelekeza vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.
Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la
kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.
Natambua kuwa Serikali nayo inatajwa
katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo
kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo. Dkt. Ulimboka alikuwa
mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na Madkatari.
Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya
majadiliano haya. Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema
wamuache maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi
kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyoeleza, mazungumzo
yalienda vizuri na mafanikio makubwa yamepatikana. Yapo maeneo machache na hasa eneo la
mshahara ambalo hatukuweza kukubaliana. Hapo tulipofikia si pabaya na
tulikubaliana sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa. Kwa nini
Serikali imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa
amri ya kusitisha mgomo. Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na
mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo. Hivi
baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven Ulimboka kwa sababu
ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna mtu wa Serikali kafanya,
itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya
Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt. Steven Ulimboka na kumuombea apone haraka
ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa.
Kwa namna ya pekee namshukuru na kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa
huruma na upendo na kwa hatua alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba kumaliza kwa kuwasihi
madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini. Watanzania wenzenu wanateseka
na kupoteza maisha. Muwe na moyo wa huruma na upendo na msaada kwa wagonjwa
kama kiapo chenu kinavyowataka.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
No comments:
Post a Comment