Kigogo wa polisi atoboa siri kipigo
cha Dk. Ulimboka. Alazwa
Muhilmbili, awaomba madaktari wasimdhuru
na Betty Kangonga na
Abdallah Khamis
MKUU wa Upelelezi wa Kituo cha
Polisi Kawe (OC CID), David Mapunda, ametoa siri ya kutekwa, kupigwa na kuteswa
kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
OC CID huyo ambaye kwa sasa
amelazwa katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi)
alilazimika kutoboa siri ya kipigo cha Dk. Ulimboka ili aweze kupata matibabu
ya majeraha ya ajali ya kugongwa na gari aliyoipata juzi.
Dk. Ulimboka alipookotwa na
wasamaria wema katika msitu wa Pande na kufikishwa katika kituo cha polisi
Bunju, kilicho chini ya kituo cha Kawe, OC CID huyo anadaiwa kutoa amri ya Dk.
Ulimboka kukaa zaidi ya saa tatu ili asipate matibabu ya haraka.
Vyanzo vyetu vya habari
vililiambia gazeti hili kuwa mara baada ya kugongwa na gari juzi, kigogo huyo
wa polisi alijitahidi sana kukwepa kwenda Muhimbili lakini alijikuta akiishia
mikononi mwa madaktari wa taasisi hiyo ya mifupa ya Moi, hivyo aliingiwa hofu
ya kutotendewa haki ya matibabu.
Kabla ya kufikishwa Muhimbili,
askari huyo alikwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Lugalo na Aghakan, lakini
alijikuta anatakiwa kufika Kitengo cha Mifupa cha Moi, Muhimbili, ambako hadi
sasa bado anaendelea na matibabu.
Kwa mujibu wa habari hizo kutokana
na hofu ya kususiwa na madaktari, polisi huyo alilazimika kuwapigia magoti na
kueleza mengi kuhusu kipigo cha Dk. Ulimboka na kwamba yeye hahusiki na sakata
hilo.
Mtoa habari wetu alisema kuwa OC
CID huyo mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo akiwa na maumivu makali,
alisema hahusiki na kipigo cha Dk. Ulimboka na hata siku ya tukio hakuwepo.
Katika hali isiyo ya kawaida,
kigogo huyo alijitetea huku akiwa na maumivu makali ya majereha aliyopata.
“Mimi sijahusika kabisa na kutekwa
kwa Ulimboka. Jamani msinidhuru. Tena siku hiyo mimi sikuwepo,’ alikaririwa OC
CID akisema.
Habari zaidi zinasema kuwa askari
huyo aliendelea kueleza mengi na hata alipotakiwa kuchomwa sindano, alionyesha
woga na kuuliza anachomwa sindano gani.
Ili kuhakikisha anatibiwa vizuri,
kumekuwa na doria za kila mara ndani na sehemu mbali mbali za wodi za MOI hali
iliyowafanya madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kulalamikia hali hiyo.
Mbali ya OC CID huyo kuingiwa na
hofu ya kulipiziwa kisasi, hofu hiyo pia imewakumba ndugu zake kwani hawana amani
na matibabu ya ndugu yao.
Tanzania Daima Jumatano ilipofika
katika hospitali Muhimbili, ilishuhudia kuwapo kwa askari polisi wakilinda
doria, huku OC CID akiwa amelazwa chumba cha peke yake akiendelea kutibiwa.
Akizungumza na gazeti hili jana,
mmoja wa madaktari wa Muhimbili ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema
Mapunda alifikishwa hospitalini hapo juzi akiwa katika hali mbaya na mara baada
ya kufikishwa aliomba msamaha kwamba hakuhusika kumteka Dk. Ulimboka.
“Ni kweli jamaa alipokelewa lakini
tulishangaa kwani alikuwa akiongea kwa kuweweseka kwamba hajahusika na tukio la
kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka na akawa anaomba tusimdhuru,” alisema daktari
huyo.
Kwa mujibu wa daktari huyo,
kilichowashangaza zaidi ni ulinzi mkali wa polisi aliowekewa mgonjwa huyo huku
kukiwa na watu wanaofuatilia kila anayeingia katika wodi namba D aliyolazwa.
Afisa Uhusiano wa Moi, Jumaa
Almasi, alisema mgonjwa huyo alifikishwa hospitalini hapo wiki iliyopita akiwa
amepata majeraha mwilini baada ya kugongwa na gari.
Kuhusu mgonjwa huyo kumtaja Dk.
Ulimboka, Almasi, alisema hawezi kuzungumzia tukio hilo kwani hakuwepo wakati
akifikishwa hospitalini hapo.
Kwa Upande wake, Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kupata ajali kwa OC-CID
Mapunda na kuongeza kuwa ajali hiyo aliipata wakati akitekeleza majukumu yake.
Alisema hakuna uhusiano wowote wa
tukio la kutekwa Ulimboka na ajali hiyo.
Tangu tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka serikali
kupitia maafisa wake wa usalama wamekuwa wakihusishwa kwa namna moja au
nyingine.
Kuhusishwa huko kwa serikali
hususan jeshi la polisi kunafuatia matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na afisa
upelelezi kutoka kituo cha Selanda Bridge katika eneo la Muhimbili, matamshi ya
kutatanisha ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova
pamoja na kukamatwa kwa mtu aliyedaiwa kuungama kanisani kuwa ndiye aliyemteka
na kumtesa Dk. Ulimboka.
No comments:
Post a Comment