Tuesday, July 24, 2012



“Tumegundua mtandao wa kuuza binadamu” – Jakaya Kikwete


na Christopher Nyenyembe, Mbeya

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa Tanzania kwa kushirikiana na nchi nyingine zimefanikiwa kugundua mtandao wa biashara haramu ya binadamu wanaosafirishwa kupitia mpaka wa Malawi kwenda nchi za Ulaya na kuuzwa kwa lengo la kupatiwa uraia na kazi.

Kikwete amedai kuwa kundi linalofanya biashara haramu ya binadamu limejikita kila nchi ambako huwapokea wananchi wa Ethiopia na Sudan Kusini na kuwapitisha kwenye njia za panya hadi Malawi.

Rais Kikwete alisema hayo juzi jioni Ikulu ndogo mjini hapa, alipokuwa akijibu baadhi ya maeneo ya taarifa ya mkoa huo iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ikihusu kuongezeka kwa kundi la wahamiaji haramu wanaopita katika mkoa huo kila wakati na kunaswa.

Kandoro alisema tatizo hilo linazidi kukua siku hadi siku huku kukiwa na idadi kubwa ya wahamiaji haramu kutoka Ethiopia wanaonaswa mara kwa mara na idara ya uhamiaji wakisafirishwa ndani ya malori na kuvushwa kwenye mpaka wa Kasumulu kuelekea nchi jirani ya Malawi ambako huko nako upo mtandao unaowapokea.

Akiizungumzia hali hiyo kwa kina, Kikwete alisema kuwa mtandao huo si kwamba ni wa wahamiaji haramu tu isipokuwa umegundulika kuwa unafanya bishara haramu ya binadamu, na kwamba kila anayefanikiwa kumvusha mtu mmoja hulipwa kati ya dola 10 na kuendelea.

“Hii biashara si ndogo kama mnavyofikiri; inawahusu watu wazito na wenye fedha ambao wakifanikiwa kuwafikisha watu huko Marekani, wanapatiwa uraia wa kuishi na kutafutiwa kazi za kufanya.

“Tulipowahoji tuliowakamata Dodoma wanasema hapa Tanzania wanapita tu na sisi hatuwezi kuruhusu wapite, tukiruhusu tutakuwa tunapingana na mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupiga vita biashara haramu ya binadamu,” alisema Rais Kikwete.

Hata hivyo alisema kuwa idara ya usalama inafanya kazi kubwa ili kubaini mianya inayotumiwa na wafanyakazi wasiokuwa waaminifu walioko mipakani ambao nao kwa namna moja au nyingine wanajihusisha na usafirishaji huo.

“Hivi ninapoongea na ninyi wengine wako hapa hapa wananisikiliza,wanapuuza ninachokisema kwa kuwa nao ni miongoni mwa watu wanaofanya biashara hiyo haramu.

“Hili tunalifanyia kazi na kama mna habari tumefanikiwa kumkamata mtu mmoja anayefanya biashara hiyo hali iliyotusaidia kutambua kwa undani mtandao mzima,” alisema Kikwete.

Hata hivyo, Kikwete aliwaomba wananchi mipakani wasaidie kuwafichua watu wanaofanya biashara hizo na kuacha kuwapokea na kuwahifadhi watu wasiowajua majumbani mwao ili waweze kupata chochote kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.

Alisema kuwa umaskini kwa kiasi kikubwa unawafanya watu wafikie mahali pa kuuzana ili tu mtu apate dola 10 kwa siku na kusisitiza kuwa wale watakaobainika wakijihusisha na biashara haramu za binadamu wenzao watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili Tanzania isiwe nchi inayolaumiwa kwa kosa hilo.

Aliiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo chini ya Mwenyekiti wake, Kandoro, kuhakikisha kuwa inafanya kazi ya ziada ili kukomesha biashara hiyo hasa katika mipaka ya Kasumulu na Tunduma na kwamba serikali imechukua hatua ya kuondoa vizuizi vya barabarani kwa kuwa vilikuwa vikiwanufaisha zaidi watumishi wa umma waliopewa kazi hiyo na kushauri mbinu zaidi za kiintelijensia zitumike.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: