Friday, July 06, 2012

Membe kutumbua ukweli wa meli za Iran zilizoandikishwa Zanzbar

Waziri wa mambo ya nchi za nje na uhusiano wa kimataifa; Bernard Membe.


Wakati suala la meli za Iran zinazopeperusha bendera ya Tanzania likitajwa kuwa moja ya sababu zinazoweza kuvuruga uhusiano wa Tanzania na Marekani, huku Mbunge wa Marekani akiwa amemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete ili aingilie kati suala hilo, leo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anatarajiwa kuweka wazi kila kitu. 

Membe ambaye alikuwa nje ya nchi, atakuwa na mkutano na waandishi wa habari leo pamoja na mambo mengine kuzungumzia kadhia hiyo hasa baada ya Mbunge Marekani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Howard Berman, kuweleza wazi kuwa kitendo cha kusajiliwa kwa meli za Iran na kupeperusha bendera ya Tanzania ni kuvunja vikwazo vya kiuchumi vya Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa msemaji wa wizara hiyo, Assa Mwambene, Waziri Membe atazungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake.

“Hilo suala mheshimiwa waziri mwenyewe atalitolea ufafanuzi kesho (leo) saa 5:00 asubuhi. Mimi sina ubavu wa kulielezea,” alisema Mwambene.

Katika barua ya Berman ya Juni 29, mwaka huu anasema kuwa anamwandikia Rais Kikwete kwa masikitiko kwamba Tanzania imeruhusu Kampuni ya Taifa ya Meli za Iran (NITC) kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye walau meli sita na zinatarajiwa kufikia 10 na zimesajiliwa nchini.

“Kwa kuruhusu meli hizo kuwa chini ya miliki ya NITC na kuendelea kusafirisha mafuta ghafi ya Iran, kitendo hiki kwa serikali yako kina madhara ya kuisaidia Serikali ya Iran kukwepa vikwazo vya Marekani na EU ili ipate mapato zaidi ya kugharimia mpango wake wa kutengeneza silaha za nyukilia na pia kusaidia ugaidi wa kimataifa,” imesema sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Rais Kikwete.

Kadhalika, alisema inasikitisha kuona kwamba serikali ya Tanzania imekiuka makubaliano ya pamoja ya jamii ya kimataifa ambayo inafanya kazi kwa pamoja kutumia njia za amani zikihusisha vikwazo vya kiuchumi ili kubadili tabia ya Iran ya kuhatarisha amani duniani.

“Kitendo cha kuruhusu meli za NITC kupeperusha bendera ya Tanzania inatia shaka hadhi ya Tanzania katika jamii ya kimataifa,” inasema barua hiyo.

Kwa maana hiyo, Berman amemuomba Rais Kikwete kuifuta usajili wa meli hizo zinazopeperusha bendera ya Tanzania, kwani kwa mujibu wa uamuzi wa Rais wa Marekani, Barrack Obama, wa 13608 ambayo aliusani Mei mosi mwaka huu unajumuisha nchi zote na mashirika yote katika ukiukaji wa vikwazo dhidi ya Iran kama watakuwa wanaisaidia nchi hiyo kukwepa vikwazo hivyo.”

Kadhalika, mbunge huyo ameonya kwamba endapo Tanzania itaamua kuziacha meli hizo kuwa na usajili nchini na kuendelea kupeperusha bendera ya Tanzania, basi wao katika Bunge la Marekani hawatakuwa na njia nyingine isipokuwa ni kutafakari kama bado mipango ya maendeleo baina ya Marekani na Tanzania kama bado inahitajika.

Meli zilizozua mgogoro huu zilisajiliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (Maritime Authority – ZMA) iliyoundwa kwa sheria No. 3 ya mwaka 2009 ambayo pamoja na kazi nyengine inasimamia utekelezaji wa Sheria ya usafiri wa Bahari Zanzibar ya mwaka 2006 (Zanzibar Maritime Transport Act 2006).

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa SMZ, Hamad Masoud Hamad, aliwasilisha taarifa yake kwa Baraza la Wawakilishi Julai 2, mwaka huu akithibitisha kusajiliwa kwa meli 10 za Iran Zanzibar ambazo zinapeperusha bendera ya Tanzania.

Alisema SMZ imetiliana mkataba na kampuni ya PHILTEX ya Dubai kufanya usajili wa meli za kimataifa (Open Registry). Usajili huu umekuwa ukifanyika tangu mwaka 2009 na mpaka sasa kupitia Wakala wake imesajili meli 399 ikiwa ni pamoja na meli za mafuta, makontena, za mizigo ya jumla na meli za abiria.

Alitaja meli hizo kuwa ni Daisy 81479 Daisy Shipping Co. Ltd Malta; Justice 164241 Justice Shipping Co. Ltd Cyprus; Magnolia 81479 Magnolia Shipping Co. Ltd Malta; Lantana 81479 Lantana Shipping Co. Ltd Malta; Leadership 164241 Leadership Shipping Co. Ltd Cyprus; Companion 164241 Companion Shipping Co. Ltd Malta; Camellia 81479 Camellia Shipping Co. Ltd Malta; Clove 81479 Clove shipping Co. Ltd Malta; Courage 163660 Courage Shipping Co. Ltd Cyprus; Freedom 163660 Freedom shipping Co. Ltd Cyprus na Valor 160930 valor Shipping Co. Ltd. Cyprus.

Waziri huyo alisema walimtaka wakala wao Philtex Corporation kuwaita wenye meli hizo na kuwataka kujieleza kuhusu uhusuiano wao na Serikali ya au makampuni ya mafuta ya Iran na walisema kuwa hawana uhusino uhusianao na Serikali au mamlaka yoyote nchini Iran na wameamua kuja kusajili meli Zanzibar kwa ridhaa.
    

No comments: