Hotuba ya Ndg. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 31.Julai 2012
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndg. Jakaya Kikwete
Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kuomba radhi kwa
kutoa hotuba ya mwisho wa mwezi wa saba, leo tarehe 01 Agosti, 2012 badala ya
jana tarehe 31 Julai, 2012. Hii ni kwa sababu ya msiba uliotukuta katika
familia na mimi kwenda Lindi kushiriki maziko ya marehemu wetu. Tofauti
na miezi iliyopita leo, pamoja na hotuba ya kawaida ya mwisho wa mwezi nimetoa
fursa kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini kuniuliza maswali nami
kujibu. Kwa upande wangu nina mambo matatu ambayo
nitayazungumzia leo.
Ajali
ya Kuzama kwa Meli ya MV SKAGIT
Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ni ajali ya Meli ya
MV SKAGIT iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012. Meli hiyo ilikuwa na watu 290, wakiwemo mabaharia 9, abiria watu wazima 250 na watoto 31. Juhudi za
uokoaji zilianza mara baada ya taarifa ya kuzama kwa meli hiyo
kupatikana. Maofisa na askari wa JWTZ, Polisi na KMKM walishiriki pamoja
na meli na watu binafsi katika uokoaji. Waokoaji walifanikiwa kuwapata
ndugu zetu 146 wakiwa hai na maiti 126 hadi tarehe 27 Julai, 2012. Kwa maana
hiyo basi, watu 18 hawajulikani walipo na inahofiwa kuwa nao pia hawako
hai. Huenda wamezama pamoja na meli au walizama baharini lakini miili yao
haikuweza kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kurudia
kutoa mkono wa rambirambi na pole nyingi kwa wale wote waliopoteza ndugu, jamaa
na marafiki katika ajali ile. Nampongeza sana Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na
viongozi wenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kazi kubwa na
nzuri waliofanya kuongoza juhudi za uokoaji pamoja na huduma walizotoa kwa
waliokolewa, waliojeruhiwa na waliofariki. Kwa wale ambao walikuwa
wenyeji wa Unguja na Pemba, SMZ ilitoa sanda na usafirishaji wa maiti mpaka
makwao kwa mazishi. Kwa wale wasiokuwa na ndugu Serikali ilibeba jukumu
la kuwazika kule Kama, Kusini Unguja.
Natoa pongezi za pekee kwa wale wote
walioshiriki katika uokoaji kwani juhudi zao ziliwezesha ndugu zetu wengi
kusalimika na maiti nyingi kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Kutokea kwa ajali ile kumetonesha
jeraha la huzuni, majonzi na mashaka makubwa yaliyolipata taifa letu miezi 11
iliyopita kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander. Katika
mkutano maalum wa Baraza la Usalama wa Taifa niliouitisha tarehe 20 Julai, 2012
kuzungumzia ajali ya MV SKAGIT tulifanya mapitio ya utekelezaji wa maagizo yetu
ya mkutano wa tarehe 11 Septemba, 2011 kufuatia ajali ya MV Spice
Islander. Kwa ujumla tumeridhika kuwa utekelezaji umekuwa mzuri kwa
upande wa mamlaka zinazohusika na usafirishaji majini yaani SUMATRA, Zanzibar
Maritime Authority na mamlaka za Bandari za nchi zetu mbili.
Ushirikiano baina ya mamlaka hizo sasa ni mzuri kwa mambo yote muhimu ambayo
Baraza liliagiza wafanye hivyo. Pamoja na hayo Baraza limetaka
ushirikiano huo uzidishwe na kuimarishwa.
Kwa mfano, Baraza limefurahishwa na
kupongeza kitendo cha mamlaka hizo kutumia Dar es Salaam Maritime
Institute kwa ushauri kuhusu ubora wa meli na huduma za usafirishaji
majini. Baraza limeagiza vyombo hivyo viwe na hadidu za rejea zinazofanana
kwa vigezo vya ubora ili nchi yetu iwe na viwango vinavyofanana vya ubora
wa meli na huduma za usafirishaji baharini kwa pande zetu mbili za
Muungano. Bahari ni moja na vyombo vinahudumia watu wale wale, kuwa na
vigezo tofauti vya ubora wa meli na viwango vya huduma ni jambo lisilostahili
kuwepo tena, ni la hatari. Baraza pia limeagiza pawepo na ukomo wa umri
wa meli zilizokwishatumika zinazoruhusiwa kutumika hapa nchini.
Aidha, Baraza limerudia kuagiza
pawepo na usimamizi makini zaidi kuhusu upakiaji wa mizigo na abiria.
Mamlaka husika, yaani SUMATRA, ZMA na maofisa wa bandari wahakikishe kuwa
uwezo wa meli uliohakikiwa na kutambuliwa unaheshimiwa ipasavyo. Pia,
meli zikaguliwe mara kwa mara na vigezo vifanane.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na hayo, Baraza la Usalama wa
Taifa limeona kuwa wakati umefika kwa Serikali yetu kuwa na Coast Guards, yaani
kikosi maalum cha uokoaji na usalama majini. Aidha, Baraza limetaka hatua
za makusudi zichukuliwe kuimarisha KMKM na Police Marines. Mwisho, Baraza
lilipongeza uamuzi wa SMZ wa kuunda Tume ya kuchunguza ajali ile kama
ilivyofanya wakati wa ajali ya MV Spice Islander.
Utafutaji
na Uchimbaji Gesi Nchini
Ndugu Wananchi,
Jambo la pili ninalopenda kulizungumzia
leo ni kuhusu maendeleo ya sekta ya gesi asili nchini. Juhudi za kutafuta
mafuta nchini zilianza mwaka 1952 na mwaka 1954 wakati kampuni ya BP ilichimba
kisima cha kwanza kule Mafia. Bahati mbaya kisima hicho hakikuzaa matunda
yaliyotarajiwa na juhudi za utafutaji mafuta zikafifia kabisa mwanzoni mwa
miaka ya 1960. Miaka kumi baadae, juhudi hizo zilianza upya na kuendelea
kwa kiwango na kasi za namna mbalimbali hadi sasa. Katika miaka ya hivi
karibuni juhudi zimekuwa kubwa na kuhusisha makampuni kadhaa ya kimataifa
yakiwemo makubwa na madogo.
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka 1954, mpaka sasa visima 61vimechimbwa, kati ya hivyo, gesi asili
imegunduliwa katika visima 22, visima 14 vya nchi kavu na maeneo ya maji mafupi na
visima 8 vya bahari ya kina kirefu. Hatujabahatika
kupata mafuta lakini tumefanikiwa kupata gesi asili katika maeneo kadhaa
baharini na nchi kavu katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo
kutokana na visima vilivyochimbwa mpaka sasa, akiba ya gesi asili iliyopo
nchini inakadiriwa kuwa kati ya futi za ujazo trilioni 25.4 – 28.9.
Yapo matumaini makubwa ya gesi nyingi zaidi kugundulika katika miaka michache
ijayo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba shughuli za utafutaji mafuta na
hasa gesi baharini zilizoanza mwaka 2004 kukiwa na kampuni moja sasa zipo 18. Baada ya ugunduzi wa kwanza wa gesi mwaka 2010,
shughuli za utafutaji sasa zimepamba moto na zimekuwa na mafanikio.
Naamini gesi nyingi zaidi itaendelea kupatikana.
Fursa
za Maendeleo
Ndugu Wananchi;
Kwa kiasi cha gesi asili
kilichokwishagunduliwa na kwa matumaini yaliyopo ya gesi zaidi kupatikana
kunaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi za kutumainiwa duniani kwa upatikanaji wa
gesi asili miaka michache ijayo. Hali hiyo inaipa nchi yetu fursa kubwa ya
kuweza kujiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii muda si mrefu kutoka
sasa.
Gesi asili ni rasilimali inayoweza
kutumika kuzalisha mbolea na hivyo kusaidia katika kuendeleza kilimo nchini kwa
kurahisisha upatikanaji wake na kuwa ya bei nafuu. Gesi asili inaweza
kutumika kuzalisha umeme na hivyo kuiwezesha nchi kupata umeme wa kutosha na
kuwepo ziada ya kuuza nje. Hivi sasa, katika gridi ya taifa megawati 350 za umeme zinatokana na gesi asili na
hata lengo letu la kuzalisha megawati 3,500 ifikapo
maka 2015 tunategemea zaidi gesi asili kuwezesha hilo kutimia. Ujenzi wa
bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam una shabaha hiyo.
Ndugu Wananchi;
Vile vile, gesi asili inaweza
kutumika kutoa nishati viwandani badala ya kutumia mafuta na hivyo kupunguza
gharama za uzalishaji. Watu majumbani wanaweza kutumia gesi asili kupikia
hivyo kupunguza matumizi ya umeme, mafuta, mkaa na kuni. Inapunguza
gharama za maisha na kusaidia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa
miti. Ni kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana TPDC inatekeleza
mradi wa kutengeneza gridi ya mabomba ya kusambaza gesi majumbani katika jiji
la Dar es Salaam.
Jambo lingine muhimu kuhusu
rasilimali hii ni kwamba tukiuza nje gesi nchi yetu itapata mapato mengi tena
ya fedha za kigeni. Kwa vile gesi ni nyingi mapato ya Serikali
yataongezeka sana, hivyo kuijengea uwezo wa kutimiza majukumu yake vizuri zaidi.
Kama matumizi yatakuwa mazuri, gesi asili itakuwa kichocheo kikubwa cha kukuza
uchumi wa nchi. Maendeleo ya haraka yatapatikana na hivyo kusaidia
kuwaondoa wananchi wengi kutoka katika lindi la umaskini tulionao sasa.
Changamoto
Muhimu
Ndugu Wananchi;
Pamoja na ukweli kwamba kuwa na gesi
asili nyingi kunaipa nchi yetu fursa kubwa ya kujiletea maendeleo, zipo pia
changamoto zake. Hatuna budi kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi ili gesi
iweze kunufaisha ipasavyo nchi yetu na watu wake. Changamoto zipo nyingi lakini
kubwa zipo za namna tatu.
Changamoto ya kwanza ni ile ya
kujenga uwezo wetu wenyewe wa kudhibiti shughuli zinazofanywa na makampuni ya
mafuta ili tuhakikishe kuwa tunapata malipo yanayostahili. Inatulazimu
tuwe na wataalamu wetu wazalendo wa fani za taaluma zihusuzo gesi kama vile
uhandisi, kemia, jiofizikia, uhasibu, ukaguzi na sheria. Tusipojenga
uwezo wetu wenyewe kwenye maeneo hayo kuna hatari ya kudhulumiwa na kupata
hasara. Pengine ipo haja ya kuwa na chombo maalum kwa ajili hiyo kama
tulivyofanya kwa mafanikio kwa upande wa dhahabu.
Changamoto ya pili ni ile ya kupata
Watanzania wengi wenye ujuzi na taaluma zinazohitajika na soko la ajira la
sekta ya gesi. Tusipofanya hivyo makampuni yataajiri watu hao kutoka nje
na hivyo kufanya Watanzania kutokunufaika na fursa za ajira zilizopo.
Ndugu
Wananchi,
Kwa changamoto hizi mbili, jawabu
lipo kwenye elimu na mafunzo tunayotoa kwa vijana wetu katika shule, vyuo vya
ufundi na vyuo vya elimu ya juu. Kwanza kabisa lazima tuboreshe elimu ya
sayansi na hisabati katika shule zetu za msingi na sekondari. Katika vyuo
vya ufundi tutoe mafundi mchundo wa taaluma zinazohitajika na tasnia ya gesi na
mafuta. Hivyo hivyo kwa upande wa vyuo vikuu nako wafundishe wataalamu wa
fani zinazohitajika kama vile utafutaji wa gesi na mafuta, uendelezaji wa
mafuta na gesi, uchumi na biashara ya mafuta na gesi, uhasibu na ukaguzi wa
mafuta na gesi pamoja na sheria za mafuta na gesi na mikataba ya utafutaji na
uendelezaji wa mafuta na gesi.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa tayari
tumejipanga kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo. Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kinajiandaa kuanza kutoa mafunzo yaChemical and Environmental Lab
for Oil and Gas na fani yaExploration and Production
Software Technology katika mwaka huu wa masomo. Chuo cha Madini
Dodoma kitaanza kutoa mafunzo ya diploma ya Petroleum Geoscience kuanzia
Septemba mwaka huu. Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha
Nelson Mandela Arusha, na Chuo cha Teknolojia cha Mbeya na kile cha Dar es
Salaam pia wameanza kufundisha mitaala hiyo. Aidha, VETA Makao Makuu na
VETA Mtwara nao wanafundisha masomo yahusuyo gesi. Wizara ya Nishati na
Madini itawadhamini wanafunzi 50 kutoka
Mkoa wa Mtwara kwenda kupata mafunzo hayo ya gesi asili katika chuo cha VETA
Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Wizara ya Nishati na Madini pia inatekeleza mpango
mkakati wa kuwapata wataalamu wa sekta hiyo kati ya 40-50 kati ya sasa na mwaka
2016. Taaluma zinazotiliwa mkazo ni Petroleum Geoscience, Petroleum
Geophysics, Petroleum Geochemistry, Petroleum Engineering, Petroleum Modeling,
Oil and Gas economics, Oil and Gas Accounting and Auditing na Oil and gas Legal
Regimes and Contract Negotiations. Kwa upande wake, Serikali
itatoa upendeleo maalum kwa kulipia gharama zote za mafunzo ili tuweze kuwapata
wataalamu hawa mapema iwezekanavyo. Nawaomba vijana wetu wachangamkie fursa
hizi za masomo na watakapohitimu mafunzo wawe tayari kuitumikia nchi yetu kwa
bidii.
Kujenga Uwezo Wetu wa
Kutumia Mapato ya Gesi
Ndugu Wananchi,
Changamoto nyingine kubwa sana ni ile ya
kuhakikisha kuwa mapato yatokanayo na gesi yanatumika vizuri na kwa manufaa ya
taifa na watu wake. Lazima tuanze sasa kufikiria na kujipanga kwa ajili
hiyo. Si vyema tukangojea mpaka hapo mapato yatakapoanza kupatikana ndiyo
tufikirie na kutengeneza mfumo mzuri wa kusimamia na kutumia mapato yatokanayo
na gesi. Tutakuwa tumechelewa, watu laghai na waovu watakuwa wameanza
kunufaika hivyo watakuwa wagumu kutengeneza mfumo utakaowanyima fursa ya
kuliibia taifa.
Jambo hili ni muhimu sana kufanya kwani ipo mifano
hai ya nchi zenye rasilimali nyingi za mafuta na gesi lakini nchi na wananchi
wake hawanufaiki sawia. Mauzo yanafanyika na fedha nyingi kupatikana
lakini manufaa kwa nchi na watu wake ni madogo au hayapo kabisa.
Wanaonufaika ni viongozi na baadhi ya maofisa wa umma wanaohusika na usimamizi
wa shughuli zihusuzo rasilimali hizo. Na, hata sisi tunaweza kujikuta
katika hali hiyo kama tusipojipanga vizuri sasa ambayo badala ya rasilimali
kuwa baraka zinageuka kuwa balaa au hata laana.
Ndugu Wananchi;
Zipo nchi duniani ambazo zina usimamizi mzuri wa
mapato ya rasilimali za mafuta na gesi na kuleta baraka na neema kwa taifa na
watu wake. Nchi hizo zimeweza kuhifadhi na kutumia vizuri mapato yake
kukuza uchumi wa nchi kwa jumla na kuboresha upatikanaji wa huduma za kiuchumi
na kijamii kwa watu. Matokeo yake ni watu wa nchi hizo kuishi maisha
yaliyo bora kuliko walivyokuwa kabla ya kupatikana kwa rasilimali hizo.
Lakini, hii imewezekana kutokana na usimamizi mzuri na matumizi mazuri ya
mapato yatokanayo na mafuta na gesi.
Tumeamua kujifunza kutoka nchi za wenzetu
waliofanikiwa ili na sisi tunufaike. Na sisi tunajiandaa kutengemeza Sera
ya Gesi Asili na kurekebisha Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta na
Sheria ya Menejimenti ya Mapato ya Serikali yatokanayo na gesi zitakazotoa
majibu hayo na kuliwezesha taifa kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa utafutaji
na uchimbaji wa gesi asili pamoja na usimamizi na matumizi mazuri ya mapato
yatokanayo na gesi hiyo. Wapo wenzetu kwa mfano, wanacho kitu
kinachoitwa Sovereign Funds ambapo
mapato yote huhifadhiwa na baadae hutolewa kwa utaratibu maalum.
Tunataka tujifunze kutoka kwao ili na sisi tutengeneze chombo chetu
cha namna hiyo ili tunufaike.
Ndugu Wananchi;
Mambo hayo tumeshaanza kuyafanyia kazi.
Katika mazungumzo yangu na baadhi ya wakuu wa nchi rafiki na mashirika ya
maendeleo ya kimataifa, nimewasilisha maombi ya kusaidiwa na kushirikiana kwa
mambo mawili. Kwanza kwa kuwawezesha Watanzania kupata mafunzo ya haraka
kwa wataalamu watakaosaidia kusimamia shughuli za utafutaji, uendelezaji na
biashara ya gesi asili nchini. Pili, watusaidie kupata watu wenye ujuzi
na uzoefu ili watushauri kuhusu namna ya kutengeneza mifumo bora ya
kusimamia na kutumia mapato ya gesi kwa mujibu wa mifano ya wenzetu
waliofanikiwa. Nafurahi kwamba maombi yetu yamepokelewa vizuri na nchi
zote na mashirika yote ya kimataifa tuliozungumza nao. Baada ya muda si
mrefu kazi itaanza.
Mgomo wa Walimu
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu na la mwisho ni mgomo
wa walimu. Pengine ni mapema kusema kwa vile kesho
Mahakama itaamua kuhusu shauri hilo. Lakini napenda kuwahakikishia walimu
kuwa tunawajali, tunawathamini na kutambua mchango wao muhimu kwa taifa
letu. Wakati wote tumekuwa tunashughulikia madai ya haki zao na
malimbikizo mbalimbali. Madai ya safari hii ni makubwa mno, yametuzidi
kimo. Athari za kuyatimiza yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali
kutumia asilimia 75kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa
Serikali na kubakiza asilimia 25 kwa
kuendeshea Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi.
Haitakuwa sawa. Ndiyo maana tumeshindwa kuelewana walipokataa rai hiyo na
wao kusisitiza kugoma.
Wakati tunaendelea kusubiri uamuzi
wa Mahakama, nina maombi mawili kwa walimu: Moja, wasiwalazimishe walimu
wasiotaka kugoma wafanye hivyo, wawaache waendelee na kazi. Pili,
wasitumie watoto isivyostahili kujenga hoja zao. Nawasihi warudi kwenye
meza ya mazungumzo.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu
naomba nitumie fursa hii kuwatakia Waislamu wote nchini kheri na baraka tele
kwa swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Wakati wote, mjiombee wenyewe kwa
Mwenyezi Mungu awajaalie toba na malipo mema katika mfungo huu. Mkumbuke
pia kuiombea nchi yetu amani, upendo na mafanikio mema.
Baada ya maneno hayo, naomba sasa niishie hapo.
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza. Sasa nipo tayari kujibu maswali ya
Wahariri kama yapo. Ndugu Wahariri
mliopo hapa, karibuni.
No comments:
Post a Comment