MAELEZO BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBERI
KABWE DHIDI YA TUHUMA ZA RUSHWA HUSUSAN KUELEKEA KATIKA KUPITISHA BAJETI YA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
Zitto Kabwe
Ndugu Waandishi,
Nalazimika kukutana nanyi kutoa
maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi
kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa
nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma. Taarifa
hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote zimesambazwa kimkakati na
kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.
Nafahamu nabeba dhamana kubwa ya
uongozi, taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi
wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali
itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika zao. Hivyo, nawajibika
kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale
wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania wasio na
sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa.
Mkakati huo wa kuniunganisha na
baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa
njia zifuatazo:
1. Kumekuwa na kauli za
watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza na hususan kutoa taswira
kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa;
2. Kuna taarifa ambazo
zimeandikwa tena katika kurasa za mbele za baadhi ya vyombo vya habari
zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto sawa na popo nundu’’ zikiashiria
kwamba na mimi ni mla rushwa; na
3. Waandishi wa habari na jamii
kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini
Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi
ya Upinzani.
Ndugu Waandishi,
Naomba kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa
kwamba nina ushiriki katika masuala ya rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu
sekta ya Nishati na Madini:-
1. Mara baada ya bodi ya Wakurugenzi
ya Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti
wake Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma kutangaza kwamba imemsimamisha kazi
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nd. William Mhando ili kupisha uchunguzi wa
baadhi ya vitendo/mwenendo wake, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC)
ambayo mimi ni Mwenyekiti wake ilimuandikia Mhe. Spika kumuomba aridhie ili
Kamati iweze kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya
Serikali (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA)
kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua
kuchukuliwa;
2. Kamati ya POAC ninayoiongoza
ilimuomba Mhe. Spika kuwaita wahusika tajwa kwa kuwa zilikuwapo tetesi kuwa
kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa
kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa
sana. Isitoshe, Kamati kutaka kujiridhisha na hatua za Bodi ni sehemu ya
msingi ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za
Kudumu za Bunge na pia Shirika la TANESCO ni moja kati ya mashirika ambayo
yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na pia ufanisi wake kwa ujumla. Tumefanya
hivyo pia katika mashirika mengine, hili la TANESCO sio tukio la kipekee;
3. Kitendo hiki cha halali na kwa
mujibu wa Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu kimetafsiriwa kwa makusudi
na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa sisi au zaidi kwamba mimi nina
maslahi binafsi na TANESCO na hususan Mkurugenzi wake Injinia Mhando, ndio maana
tumetaka maelezo ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati ya POAC tumewaita pia Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma
(PPRA) kwa jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi!
4. Baada ya tukio hilo, nikiwa
hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa
wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake, Nd. Eliachim Maswi hapa
hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa
na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani!
5.
Nimejaribu kumtafuta kwa
simu Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake ili wanipe ufafanuzi juu ya mimi na
Kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizi bila mafanikio, hali ambayo
inaniondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi
huo. Najaribu sana kujizuia kutokuwa na mashaka na ushiriki wao huo
ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao katika jamii, lakini wameshindwa
kunidhihirishia tofauti.
Sasa naomba kutoa
ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa matukio hayo tajwa ambayo yanatumiwa na
baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti nimehusika na vitendo vya rushwa.
1.
Binafsi sijawahi kuwa na
mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua
ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika.
Ieleweke wazi kabisa kuwa, hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au
Kamati yetu imekataa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote.
Ambacho tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria,
hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi;
2.
Ni kwa sababu hiyo, na kwa
kujiamini kabisa nimeunga mkono suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa
zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
kwa kina;
3.
Nimekwenda mbali zaidi
kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina
kujiridhisha na tuhuma hizo;
4.
Natumia fursa hii pia
kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata
ukweli;
5.
Ninaahidi kushiriki
kikamilifu iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari
kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yeyote.
Napenda
niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja
kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba:-
1.
Mimi Zitto Zuberi Kabwe
sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima
nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa,
na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii
pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo;
2.
Nafarijika na salam mbali
mbali zinazotolewa kunifariji na kusisitiza kuwa nisilegeze kamba katika
mapambano haya, nimepokea ujumbe mwingi kwa simu, sms, tweeter na hata facebook
na niko pamoja nanyi Watanzania wenzangu kamwe sitarudi nyuma hadi kieleweke. Naamini katika
nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha mahitaji/haja ya kila mmoja wetu lakini
si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya watanzania wenzetu;
3. Napenda
kuweka rekodi sawa kwa Watanzania kwamba nimekuwa Mbunge hiki ni kipindi cha
pili, Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) huu ni
takriban mwaka wa saba sasa, Kamati yangu inasimamia mashirika 259 ya Umma na
si TANESCO peke yake. Mchango wa Kamati hii katika Bunge na kwa ustawi wa
Mashirika ya Umma ni bayana na haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa
upotevu mkubwa wa mali za umma na kuokoa fedha za umma kutokana na umakini
wake. Tumefanya hivyo CHC hivi karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine
mengi. Kote huko uadilifu na uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa. Inatuwia
vigumu kuona kuwa tunahojiwa katika suala hili la TANESCO. Hapa pana kitendawili.
4. Zipo hoja pandikizi za kutaka Kamati
ya POAC ivunjwe na haswa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia
mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa Kamati hii
imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi. Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC
isihusishwe na tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama
mimi na sio kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma
hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari kunusuru Kamati
ya POAC na maslahi ya taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti iwapo itathibitika
pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi.
5. Nafahamu pia kuwa kuna wanasiasa
hasa wa Upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia
kutaka kuidhoofisha. Lakini hawajui kuwa anaepanga wajumbe wa Kamati ni Spika
wa Bunge.
6. Msishangae pia kuja baadae kubaini
kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio
vinara wa kupokea rushwa.
7. Ni lazima tufike mahali kama
viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa
hadharani tuseme bila kuogopa. Hili ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi.
Kusimamia ufuatiliaji wa utaratibu ni jukumu letu kama Kamati ya POAC na ndio
sababu ya msingi ya kuanzishwa kwa mamlaka kama CAG na PPRA. Haiwezekani, tuwe
na set ya kanuni kwa kundi fulani na nyingine kwa makundi mengine, au kuhukumu
ufuataji wa taratibu kwa kuangalia sura ya mtu usoni
Mwisho
Kumejengeka tabia hivi sasa ya
kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na uzalendo. Kumeanzishwa kiwanda
kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na fitna zenye lengo la
kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na wananchi kwa kutumia vyombo vya habari
na nguvu ya fedha. Naamini mbinu hizi chafu, kama nyingine nyingi
zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa.
Naamini katika kweli na kweli daima
huniweka huru. Naamini kuwa mwale mdogo wa mwanga wa mshumaa hufukuza kiza. Kwa
imani hiyo, sitasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu hata nitakapobaki peke
yangu katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea rasilimali za taifa
zinufaishe watanzania wote.
Daima nitaongozwa na busara ya
Hayati Shabaan Robert isemayo, ‘Msema kweli huchukiwa na marafiki zake,
nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao kudumu na
marafiki zao siku zote, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo,
nikajitenga na furaha ya kweli itakayotokea pale uwongo utakapojitenga”.
Ahsanteni sana.
Chanzo: http://zittokabwe.wordpress.com/
1 comment:
Jenerali Mstahafu Robert Mboma alikuwa kwanza mkuu wa Jeshi la anga akiwa Meja Jenerali. Alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Tanzania (JWTZ) akapandishwa cheo ni kuwa Jenerali. Hivyo mpaka anastahafu jeshini cheo chake ni JENERALIA na sio Meja Jenerali. Zitto hapa umechemsha!
Post a Comment