Neno
la usiku:
CCM
na sifa ya mchawi!
Ndugu zangu,
Usiku wa saa sita umeingia tena hapa Iringa. Kabla sijaondoka kwenye meza ya kibarua changu nina neno fupi la usiku.
Naam, inasemwa, kuwa
mchawi mchukie, lakini, sifa yake mpe, anajua kuroga!
Majuzi hapa nilipokuwa
kwenye shughuli za kijamii kijijini Mahango, Madibira, kuna kitu kilichonifanya
nishangae, lakini, baada ya tafakuri nikauona ubunifu kwa aliyekitenda.
Nikiri, kuwa huko
nyuma nimefanya vikao kadhaa na Kamati ya Shule ya Mahango chini ya
Uenyekiti wa Bw. Victor Kadama ( Pichani). Sikupata kujua kuwa Victor
Kadama, mbali ya kuwa Mwenyekiti wa kamati ya Shule, pia ni Katibu Mwenezi wa
CCM, Kata ya Madibira. Ndio, Victor Kadama ndiye Nape Nnauye wa Madibira.
Maana, kwenye vikao vyetu
hakuwahi hata siku moja kuvaa nguo za rangi ya chama chake wala kofia. Lakini,
majuzi hapa tulipokuwa na mkusanyiko mkubwa wa wanakijiji kuwapokea wageni
kutoka Norwich, Uingereza waliokuja kuzindua mradi wa ujenzi wa
Maktaba ya Kijamii kijijini hapo, basi, kwa siku mbili mfululizo, nilimwona Bw.
Victor Kadama akiwa ametinga kofia ya chama chake, CCM.
Bw. Kadama kwa siku
zote mbili hakuongea hata neno moja kuhusu chama chake, lakini, kofia yake
ilikuwa inaongea. Kulikuwa na uwepo wa CCM kupitia kwa kofia ya Kadama.
Na hata wageni waipopangiwa ziara ya miguu kuona mazingira ya kijiji,
Victor Kadama na kofia yake haraka alichukua jukumu la kuongoza msafara.
Aliendelea kufanya ' kazi ya uenezi' wa Chama chake.
Kwa vyama vingine vya
siasa kuna ya kujifunza kutoka kwa CCM. Pamoja na dhambi zao zote, CCM bado
wana oganaizesheni inayoeleweka na yenye kufikia hadi ngazi za vitongoji.
Ni mtaji wao mkubwa kisiasa. Tofauti na vyama vingine, makada wa CCM
wanajipenyeza kila mahali, iwe kwenye kamati za shule au za kuchimba visima.
Ndio, hata, uwe na harusi ya mwanao, bado kuna makada wa CCM
watakaojipenyeza kwenye Kamati za harusi.
Naam, mchawi mchukie,
lakini sifa yake mpe, anajua kuroga, hakyamungu!
Maggid,
Iringa.
0788 111 765
No comments:
Post a Comment