Wafanyakazi 30
wa TIGO watimuliwa kwa kuvujisha siri kwenye gazeti la MwanaHALISI
na Betty Kangonga (Tanzania Daima)
KUTEKWA, kupigwa na kuteswa kwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na
hatimaye kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kumeleta
kizaazaa katika kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Tanzania Daima Jumatano
limebaini.
Habari kutoka ndani ya kampuni hiyo
ya simu yenye mtandao mpana nchini, zinasema kuwa zaidi ya wafanyakazi 30
wamefukuzwa kazi na wengine wako kwenye uchunguzi wakituhumiwa kuvujisha
mawasilino ya siri ya simu za wateja kwa Gazeti la MwanaHalisi.
Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa
za mawasiliano za simu zinazodaiwa kuvujishwa na wafanyakazi hao, zilikuwa kati
ya Dk. Ulimboka, Afisa Usalama wa Ikulu na watu aliowasiliana nao kabla ya
kutekwa.
Rais Jakaya Kikwete amepata
kuliambia taifa mara mbili kwa njia ya televisheni, mwishoni mwa Juni na
alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari wiki iliyopita, kwamba serikali
yake haihusiki kuteka, kutesa na kumtupa daktari huyo porini.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda
amepata kuliambia Bunge kuwa, serikali yake haihusiki na utekaji, utesaji na
kuhoji, “...serikali imteke ili iweje?”
Hivi karibuni serikali ililifungia
Gazeti la MwanaHalisi baada ya kuandika habari iliyomtaja ofisa mmoja wa Idara
ya Usalama wa Taifa Ikulu (TISS), kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa kumteka,
kumpiga na kumtesa hadi kumjeruhi Dk. Ulimboka, ambaye kwa sasa anaendelea na
matibabu kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa habari hiyo ambayo
serikali inadai kuwa ni ya uchochezi, MwanaHalisi ilianika namba ya simu ya
ofisa huyo pamoja na watu wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo
linaloendelea kuchunguzwa na kamati maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi
wa Makosa ya Jinai (DCI).
Vyanzo vya habari kutoka kwa baadhi
ya wafanyakazi waliokumbwa na sekeseke hilo, zinasema kuwa waliofukuzwa wengi
ni wafanyakazi wa kitengo cha IT ambao wanadaiwa kuhusika kutoa taarifa za siri
ya mawasilino kati ya Dk. Ulimboka na watu wanaoaminika kuwa ni wabaya wake.
Mmoja wa wafanyakazi kutoka Kampuni
ya Tigo, aliliambia gazeti hili kuwa mbali na kutuhumiwa kutoa siri kwa Gazeti
la MwanaHalisi, wafanyakazi wengine wametimuliwa kwa madai ya kufanya
udanganyifu kwenye huduma za Tigo Pesa na kujipatia fedha.
“Kweli watu wengi wamefukuzwa
wakituhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, lakini wengine walikuwa
wakishirikiana na mawakala wa Tigo Pesa kuiibia kampuni.
“Kwa mfano mfanyakazi alikuwa
anakubaliana na wakala kumwingizia kiasi kama cha sh milioni moja, lakini
anaweza kuingiza hadi sh milioni 1.5 na kati ya hizo sh 500,000 ni mali yake,”
alisema mfanyakazi huyo.
Akizungumzia na Tanzania Daima
Jumatano, Mhariri Mkuu wa Gazeti la MwanaHalisi, Jabir Idrissa alishangazwa na
taarifa za Tigo kuwafukuza wafanyakazi wake kwa sababu ya habari iliyochapishwa
na gazeti lake.
“Chanzo chetu cha habari hakikutoka
kwa wafanyakazi wa Tigo. Kama wamefukuzwa kwa sababu ya MwanaHalisi, wamewaonea
bure. Kama Tigo ndio waliotupa taarifa na zile za Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), zilitoka wapi?” alihoji Jabir na kusisitiza wafanyakazi hao wameonewa
bure.
Ofisa Uhusiano wa Tigo, Edward
Shila, alipohojiwa kuzungumzia tukio hilo, hakukubali wala kukataa madai hayo
na kumtaka mwandishi kumtumia maswali kupitia e-mail yake ili aweze kuyatolea
majibu kiofisi.
“Kama una maswali naomba uniandikie
kupitia e-mail yangu ambayo nakutumia sasa hivi…maana siko tayari kutoa kauli
yoyote isiyokuwa ya kiofisi,” alisema.
Naye Omary Matulla ambaye
amejitambulisha kuwa ni ofisa wa kitengo cha kumbukumbu katika kampuni hiyo,
alikanusha kuwapo kwa taarifa za kufukuzwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema kuwa kila mfanyakazi ana
mipaka ya kufanya kazi katika kampuni hiyo, na pia ni wajibu wa kila mtumishi
kutunza siri kubwa.
“MwanaHalisi ana mbinu zake za
kupata habari wala haiwezekani kupata habari kupitia kampuni yetu na hata hivyo
jambo hilo si rahisi hata kidogo kutokea,” alikanusha Omary.
Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni
26, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa
kucha na kutolewa meno na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Tangu kutokea kwa tukio la kutekwa
kwa Dk. Ulimboka, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wanaharakati
wa kutetea haki za binadamu, wamekuwa wakiinyoshea kidole serikali kwamba ndiyo
iliyohusika.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi
mkoani Dar es Salaam, Suleiman Kova, hivi karibuni alitangaza kumfikisha
mahakamani mtu mmoja aliyedai kukiri kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka.
Kova aliwaambia waandishi wa habari
kuwa, polisi wamekamata mtu aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri
kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka.
Alidai kuwa mtuhumiwa alikwenda
kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar es Salaam.
Lakini hata hivyo, mchungaji wa
kanisa hilo, Josephat Gwajima alikana kauli ya Kova juu ya mtuhumiwa huyo,
akisema hajakwenda kutubu kwao.
No comments:
Post a Comment