Dr. Nkosazana Dlamini-Zuma
Kiswahili chazidi kupaa Umoja wa
Afrika
Umoja
wa Afrika umeitaja Lugha ya Kiswahili kuwa ndiyo lugha kubwa na rasmi Afrika na
ndio Lugha inayofundishwa zaidi katika Vyuo Vikuu mbalimbali duniani kutoka
Afrika.
Hayo
yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma
wakati akifungua Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika
mjini Addis Ababa, Ethiopia leo tarehe 30 Januari, 2013.
Dkt.
Zuma katika hotuba yake ya kusisimua ambayo ilielezea maendeleo yaliyofikiwa
Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, changamoto mbalimbali
zinazolikabili Bara hili na matarajio alisema kwamba katika kipindi hiki ni
muhimu kuitumia Lugha ya Kiswahili kuiunganisha Afrika.
“Wajukuu
zetu waliona ni kichekesho tulivyokuwa tukihangaika na tafsiri za Lugha
za Kiingereza, Kifaransa na Kireno wakati wa mikutano ya AU, na vile
tulivyokuwa tukizozana kwamba chapisho la Kiingereza halifanani na lile la
Kifaransa au Kiarabu, sasa tunayo Lugha yetu pamoja na hizo lugha nyingine huo
ndio ustaarabu wa sasa” alisema Dkt. Dlamini-Zuma.
Akizungumzia
maendeleo yaliyofikiwa Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Mhe. Dkt.
Dlamini-Zuma alisema kuwa Afrika sasa imepiga hatua kubwa katika
maendeleo ambapo kwa sasa Afrika ndio msafirishaji mkubwa wa chakula nje na pia
imekuwa kituo cha viwanda na kituo cha maarifa na hivyo kuleta manufaa kwa
maliasili zilizopo ikiwemo mazao ya kilimo kama kichocheo cha mapinduzi ya
viwanda.
“Rafiki
zangu, kwa hakika Afrika imepiga hatua kubwa katika maendeleo, kutoka
usafirishaji wa malighafi katika kipindi kilichopita na kuwa msafirishaji mkuu
wa chakula nje, hii itasaidia maliasili iliyopo Afrika kubaki na kuwa kichocheo
cha mapinduzi ya viwanda” alisema Dkt. Dlamini-Zuma. Aidha aliongeza kuwa,
Kampuni nyingi za Afrika kuanzia zile za madini, fedha, chakula, vinywaji,
utalii, madawa, uvuvi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni miongoni mwa
zinazoongoza duniani katika sekta hizo.
Dkt.
Dlamini-Zuma alieleza kuwa Afrika sasa ni ya tatu duniani kiuchumi. Hata hivyo
alisisitiza bado kuna umuhimu kwa nchi za Afrika kuchangia katika maendeleo.
Vile vile, alisema kwamba njia pekee ya kuleta amani ni kuwekeza kwa watu
hususan kuwawezesha vijana na wanawake. ‘Afrika inahitaji mapinduzi katika
ujuzi kwa kubadilisha mfumo wa elimu ili kuwaandaa vijana ambao ni wabunifu na
wenye mawazo ya ujasiriamali ili kuleta maendeleo katika Bara lao’ alisema Dkt.
Zuma.
Kuhusu hali ya
amani na usalama huko, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Dkt.
Dlamini-Zuma alielezea kusikitishwa kwake na hali katika nchi hizo na
kusisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta amani
ya kudumu katika nchi hizi.
"Tunavyouanza
mwaka 2014 mioyo yetu ipo na watu wa Sudan Kusini na wale wa Jamhuri ya
Afrika Kati hususan wanawake na watoto hivyo ni muhimu tufanye kazi kwa pamoja
ili nchi hizi zipate amani ya kudumu na kutimiza lengo letu la kuzima kabisa
mitutu ya bunduki katika Bara letu" alisisitiza Dkt. Dlamini-Zuma.
Aidha,
alimtangaza Bibi Binta Diop kuwa Mjumbe Maalum wa Amani na Usalama Afrika
ambaye atakuwa na jukumu la kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika katika
masuala ya kujenga amani na utatuzi wa migogoro.
Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika pia ulishuhudia ubadilishanaji wa
Uenyekiti wa Umoja wa Afrika kutoka kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe.
Hailemariam Dessalegn kwenda kwa Rais wa Mauritania, Mhe.
Mohamed Ould Abdel Aziz. Aidha, Mkutano huo ulimkaribisha Rais mpya wa
Madagascar, Mhe. Hery Rajaonarimampianina baada ya miaka minne ya kufutwa
uanachama wa AU.
Akitoa hotuba
yake kabla ya kukabidhi uenyekiti, Mhe. Dessalegn alizishukuru nchi zote za
Afrika kwa ushirikiano na kusisitiza umuhimu wa kuweka vipaumbele vya
maendeleo Barani Afrika katika Agenda ya Maendeleo ya Kimataifa baada ya mwaka
2015 na ile ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Ujumbe wa
Tanzania kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU uliongozwa na Mhe.
Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
ambaye alimwakilisha Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
No comments:
Post a Comment