Thursday, April 03, 2014

Hotuba ya kuwagawa Watanzania - Barua ya ZAWA UK kwa Rais Kikwete


Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
Ikulu
P O Box 9120
Dar es Salaam



Yah: Hotuba yako ya kuwagawa Watanzania



Mheshimiwa Rais,

Tumelazimika kuandika barua hii kwako kama kiongozi wa juu wa taifa letu ili kukuonesha namna ambavyo tumesikitishwa na matamshi yako wakati wa ufunguzi wa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma. Tukiwa sehemu ya jamii kubwa ya Kizanzibari tuishio nje ya nchi yetu, hotuba yako imetutia khofu kubwa kulenga kwake zaidi kwenye kuvunja na sio kujenga mustakbali mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hotuba yako Mheshimiwa Rais, haikuzingatia maslahi ya Muungano wetu kwa misingi ya umoja unaonendana na matakwa ya wananchi walio wengi.

Tunakuandikia barua hii kukuzindua kile ambacho tumekiona kinakwenda tafauti na akhlaki zako. Ukweli ni kwamba kwa muda wote wa kipindi chako cha utawala tumekuwa tukikutazama kama ni tarajio jipya lililojengeka kwa misingi ya haki, insaaf na kioo cha uadilifu kwa pande mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano.

Tunazungumza nawe moja kwa moja sio tu kama kiongozi wa taifa, bali pia kama mtu tuliyempa matumaini hayo. Wewe ni mtu wa mwisho kwetu kuamini kuwa anaweza kujenga khofu badala ya matumaini, batili badala ya halali, kitisho badala ya nasaha na mgawanyiko badala ya utangamano.

Mheshimiwa Rais,

Ulichokifanya siku ya tarehe 21 Machi 2013 ni kuzua taharuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano hasa kwa ndugu zetu wa Kizanzibari waishio upande wa pili wa Muungano huo. Ulichofanya ni kulihusisha jeshi letu linalothaminiwa dunia nzima kwa misingi ya heshima kwa kusaidia pakubwa kuifanya Jamhuri yetu kuwa ndio kisiwa cha amani kwa takribani miaka yote 50 ya Muungano wetu. Hakujawahi katika historia ya Tanzania kwa rais kuzuwa hisia za mapinduzi ya kijeshi kama hoja mbadala ya kuviza maoni ya walio wengi katika kiwango ambacho wewe umefanya.

Mheshimiwa Rais,

Ulikuwa umejizolea sifa kwa kuwa mmoja wa viongozi wachache wa Tanzania ambao hawakuonea haya mtafaruku wa kisiasa visiwani Zanzibar na ukaamua kuuvalia njuga ili kuhakikisha kuwa unatulizwa kwa amani. Kwa Wazanzibari wengi walio ndani na nje ya nchi, matarajio yao yalikuwa ni kwamba wewe ungelisimimia haki yao ndani ya Muungano kwa uadilifu mkubwa haidhuru maoni waliyonayo kuhusu muundo wa Muungano yanatafautiana na yako.

Tulikutegemea kuwa msimamizi wa haki uliyejizatiti kuhakikisha chembechembe za ubaguzi zinakufa katika kipindi chako cha utawala. Tulikutegemea usimame imara kusimamia hilo maana ndiyo misingi ya kiuongozi. Hatukutegemea hata kidogo uyumbe na uyumbishwe na kundi la wahafidhina ndani na nje ya Chama chako cha Mapinduzi (CCM), kwani maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu zaidi kuliko maslahi finyu ya makundi hayo ya kihafidhina. Lakini leo hii umekwenda kinyume hata na imani yako kwa kuwabeza Wazanzibari waishio Tanganyika bila ya kuthamini mchango wao mkubwa katika ukuwaji wa uchumi katika Muungano huu.

Tukukumbushe Mheshimiwa Rais, ikiwa umesahau, kuwa ni Zanzibar ndiyo iliyoungana na Tanganyika. Si Wapemba wala Waunguja. Sawa na sisi kusema kwamba hatukuungana na Wadengereko au Wanyamwezi waishio visiwani Zanzibar, bali ni Tanganyika kwa jumla kama nchi iliyo na makabila zaidi ya 100 ambayo tokea awali tumekuwa pamoja kwa misingi ya udugu kabla hata ya Muungano wa nchi zetu.

Pili tukukumbushe Mheshimiwa Rais kwamba suala la kuuvunja Muungano halijawahi kuwa sehemu ya mjadala mkuu kwenye Rasimu ya Katiba. Ni wewe na wenzako ndio ambao munalizusha kila mara kwa mintarafu hiyo hiyo ya kutisha. Lakini hata kama hayo yatakuwa ndio matokeo ya munayoyataka, basi tukukumbushe kuwa Waunguja na Wapemba waishio Tanganyika wataathirika sawa sawa na mtetemeko wa Muungano kama ilivyo kwa Watanganyika waishio visiwani. Si walima vitunguu tu ambao husaidia katika ulipaji wa kodi inayotumika kuijenga Tanganyika watakaoathirika na uvunjwaji wa Muungano, bali kila mmoja wetu.

Inashutsha sana kwa rais wa nchi mwenye heshima duniani kukiuka misingi ya usawa kwa kuwalenga jamii ya watu anaowaongoza kwa vitisho badala ya kuwahakikishia ulinzi hasa kwa vile ndie jemedari mkuu wa jeshi aliyeapa kuwalinda wananchi wote wa Muungano huu kwa nguvu zote alizopewa kikatiba.

Hatukuzuii kutetea na kulinda mfumo wa serikali mbili hasa ukiwa mwenyekiti wa chama chako kilichojizatiti katika mfumo huu wa sasa. Lakini ukiwa kama ni rais wa nchi inakupasa kuzitafautisha sehemu hizi mbili za kimamlaka ili kuwe na ufanisi wa demokrasia iliyokuchaguwa na kukupa hadhi ya rais wa Muungano huu.

Hivi kweli hakukuwa na hoja nzito za kuulinda mfumo wa sasa bila ya kuwaingiza wananchi katika mzozo mkubwa utaoleta nyufa katika taasisi tunayotarajia kuilinda na kuiimarisha?

Umeamsha hisia kwamba ni Wapemba pekee – kama ulivyotuita – tunaofaidika na Muungano huu na kuendeleza kampeni ya chuki juu yetu, badala ya kuwazindua wananchi michango ya pande zote mbili katika ukuwaji wa uchumi na pia misingi ya amani tunayojivunia. Umekiuka maadili ya uongozi uliotukuka ulioapa kuitekeleza ukiwa ni mkuu wa Muungano huu na kudharau michango yetu Wazanzibari katika sekta zote za maendeleo ya Tanganyika.

Tukukumbushe tena Mheshimiwa Rais kwamba huna uhalali wa kuunganisha mfumo wa Serikali Tatu na uwezekano wa kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi. Umekuwa mmoja wa wapatanishi wa mzozo wa Madagascar, kwa mfano, na unajuwa kwamba mapinduzi ni zao la wapenda madaraka, wasiopenda kuwasikiliza wananchi walio wengi pamoja na uendeshwaji wa nchi kwa misingi isiyoendana na haki, uadilifu na ihsani.

Mfumo wa muungano unahitaji ithibati nzito kutoka kwa wananchi wa pande zote mbili. Haiwi sawa kuendeleza hamasa za kisiasa kwa kuzidharau hisia na matakwa ya walio wengi kwa kisingizio cha kuendeleza siasa za kuwaridhisha Wazanzibari pekee.

Hiyo ni sawa na rushwa ya upande mmoja, na ulaghai wa hali ya juu kwa upande mwengine, kwa vile kero za Muungano hazipo kwa Wazanzibari pekee. Tunahitaji mfumo utaokuwa na nguvu ya matakwa ya pande zote mbili, utakaoweza kudumu na kuwa tunu kwa Afrika nzima.

Miaka 50 ya Muungano huu wetu mbali ya kwamba hakuna aliyejaribu kujiunga nasi kwa kutokuwa na manufaa, bali hata wengine walioungana hawakuwahi kuutazama huu wetu kama kigezo cha kuungana.

Kwa kuendeleza mfumo wa sasa katika jitihada za kutiatia viraka, zipo ishara nzito kwamba sio tu kwamba Muungano hautadumu, bali pia utazua machafuko makubwa na kuzitia nchi zetu katika giza la historia chafu na dowa litaanza kwako kwa kuogopa kivuli chako mwenyewe. Ni vigumu kwa wakuu wa nchi kupima hali halisi ya nchi kwa kusikiliza wapambe waliojipenyeza kwa fitna na kukisema kile ambacho wakuu hupenda kukisikia.

Kwa sasa angalizo kwako ni kuangalia mazingira yalivyo hasa katika Muungano na muamko wa wananchi katika mabadiliko waliyoyategemea zaidi kutoka kwako.

Mheshimiwa Rais,

Tunakuusia tena kama tunavyoziusia nafsi zetu, wasikilize wananchi walio wengi na matakwa yao katika ujenzi wa Muungano mpya utakaokuwa madhubuti na utakaoacha jina lako kuwa kwenye kumbukumbu njema kwa vizazi vijavyo. Haki, usawa na heshima baina ya pande hizi mbili ndio ziwe dira kwako katika kuleta mustakbali wa mabadiliko yatayotuweka katika Muungano utakaothaminiwa na kutunzwa na kila mdau.

Matarajio yetu katika kipindi chako ni mageuzi ya kweli yanayoendana na wakati, yatakayoangalia matakwa ya wananchi na kuhakikisha hekima zako na busara zitaweza kuzaa matunda makubwa yatayoweza kuwa neema kwa vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Rais,

Khofu ni adui mkubwa wa mabadiliko ya kweli na yaliyo thabiti. Ulichaguliwa kwa matarajio makubwa kwa vile ulionyesha wazi kuwa miongoni mwa wachache walio na dira ya mapatano, ukuwaji wa amani na mapambazuko ya demokrasia nchini.

Tanzania iliweza kubadili mfumo wa vyama vingi na kubeza waliokuwa na khofu ya mabadiliko. Zanzibar iliweza kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo kwa upande mkubwa imerejesha imani kwa wananchi na hata wawekezaji na kuwa ni chombezo kwa wengine majirani kufuatia.

Na kwa hili la mabadiliko ya mfumo wa Muungano tuna hakika ndio nafasi pekee ya Muungano mpya utakaobeba haki, usawa na heshima kwa kila mwananchi wa nchi zetu hizi.

Mheshimiwa Rais,

Tumekuandikia haya yote kwa kuwa tunaamini kuwa ukitaka unaweza kurekebisha pale ulipoteleza. Wewe ni mwanaadamu licha ya kuwa kiongozi mkuu wa nchi. Una nafasi ya kufanya makosa, lakini una nafasi kubwa zaidi ya kusahihisha makosa yako, maana makosa yako yana uzito mkubwa na wa kipekee kwa hatima ya taifa.

Tunakunasihi uipitie tena hotuba yako, weka sawa ulimopinda, safisha ulimochafua. Nchi inataka uongozi wako kukwamuka na kusonga mbele. Haitaki vitisho wala khofu zako. Ukihisi ni maamuzi magumu zaidi, rudi kwa wananchi na uwaulize tena kwa uwazi matakwa yao juu ya mfumo wa Muungano wa nchi zetu. Sote tunataka Tanzania kwanza pia hapana shaka, lakini kwa maana gani ya Tanzania kwanza?


Tanzania kwanza isiyobebwa na shengesha za mfumo butu wa sasa.

Tanzania kwanza isiyoviza ukweli wa kuwepo kwa Zanzibar na Tanganyika zinazojiendesha kwa ufanisi.

Tanzania kwanza iliyojidhatiti katika Muungano wa heshima, usawa na haki. Tanzania kwanza iliyobebwa na matashi na matakwa ya wananchi.

Tanzania kwanza ya Serikali Tatu sio moja ya kuimeza Zanzibar na isiyotenda haki kwa Tanganyika.

Ahsante.

Hassan M Khamis
Mwenyekiti ZAWA UK

1 comment:

Tende said...

Hii dondoo ni ndefu kweli lakini nimeshindwa kupata maneno kamili yaliyotamkwa na Rais kuonyesha madai ya mwandishi. Ni vizuri kama mwandishi angeonyesha ni jinsi gani matamshi ya Rais na yanavyotishia usalama au kubomoa muungano.