MBUNGE wa Kawe, Halima
Mdee (CHADEMA), amemlipua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka, kwamba anamiliki maelfu ya ekari za ardhi katika maeneo
mbalimbali nchini.
Mdee ambaye ni Msemaji wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alirusha kombora hilo jana bungeni wakati
akisoma maoni ya kambi hiyo kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Makombora hayo ya Mdee,
yalimfanya Waziri Tibaijuka, kutumia muda mrefu zaidi kujibu mashambulizi
badala ya hoja za wabunge wakati akihitimisha hoja yake.
Majibu hayo yalimfanya
Spika wa Bunge, Anne Makinda, kila mara kumtaka Waziri Tibaijuka ajibu hoja za
wabunge badala ya kujikita kumjibu Mdee, katika masuala yanayoonekana ni
binafsi.
Waziri Tibaijuka, alisema
kuwa Mdee amekuwa bingwa wa kuiba siri za serikali ikiwemo mwaka jana kuiba
andiko la chuo kikuu na mwaka huu ameiba barua zake za siri alizomuandikia
Waziri Mkuu.
Hoja za-Mdee
Mdee, alisema Waziri
Tibaijuka ana maslahi makubwa katika sekta ya ardhi ambapo anamiliki kiasi
kikubwa cha ardhi maeneo ya Kigamboni na Kagera Wilaya ya Muleba ambako katika
eneo la Kyamnyorwa ana hekta 800.
Kwa mujibu wa Mdee, mjini
Bukoba, waziri huyo mwenye dhamana ya ardhi, anadaiwa kumiliki ekari 100
alizozipata kiujanja.
Alisema eneo hilo
alilipata kwa kuwahamisha wamiliki halali kwa nafasi yake ya ukurugenzi wa
UN-Habitat na baadaye ya uwaziri wa ardhi.
“Mheshimiwa Spika,
linapokuja suala la migogoro ya ardhi, Waziri Tibaijuka anakosa “moral
authority” katika kuutafutia ufumbuzi wa haki. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka serikali kuliangalia upya suala lolote la ardhi ambalo waziri
atajiingiza kwani nyuma ya sakata hilo kuna maslahi binafsi yake kama hili la
Chasimba, na Kigamboni,” alisema Mdee.
Mbunge huyo alifichua siri
nyingine ya umiliki wa ardhi ya waziri huyo katika eneo la Kigamboni ambako
kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa mji mpya na wa kisasa.
Alisema katika eneo hilo,
Waziri Tibaijuka, kwenye ekari 50,934 zilizoongezwa kwa ajili ya mradi wa
ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni, amejimegea maelfu ya ekari.
Alisema Waziri Tibaijuka
aliongeza eneo la mradi kutoka hekta 6,494 zilizokuwepo awali hadi hekari
50,934.
“Hoja hapa ni je kati ya
hekta zilizoongezwa 44,440, zinazomilikiwa binafsi na waziri ni ngapi? Hii
haina siri, akikataa kusema wananchi wanaelewa ni ngapi, na hotuba ya mwaka
kesho zitatajwa hapa bungeni,” alisema Mdee.
Alisema anaitaka serikali
kuangalia upya mipango ambayo inatayarishwa na kusimamiwa na Waziri Tibaijuka
na jinsi gani inatekelezwa kwa madai kuwa haaminiki tena.
Mdee alisema katika
migogoro mingi ya ardhi, Waziri Tibaijuka amekuwa akitajwa kuhusika na katika
mazingira hayo ni dhahiri kuna jambo limejificha, hivyo ni wakati mwafaka
kuchukua hatua kabla ya majanga zaidi kutokea.
Mbunge huyo alimshambulia
Tibaijuka, kwamba hawezi kusimamia wizara hiyo kwani hata kwenye nafasi
aliyoachia Umoja wa Mataifa, aliondolewa kutokana na uwezo mdogo wa kufanya
kazi.
Akizungumzia sarakasi za
mradi wa Kigamboni, Mdee alisema mpango wa ujenzi wa mradi huo, umekuwa
ukilalamikiwa sana na kutiliwa shaka na- wananchi wa eneo hilo.
Mbunge huyo alisema mpango
huo ambao unaelezwa kuwa wa serikali, sio sahihi kwani umevalishwa koti tu la
serikali.
Kwa mujibu wa Mdee, ukweli
huo unathibitika kutokana na mvutano uliopo kati ya wananchi wa Kigamboni
wakiongozwa na mbunge, Dk. Faustine Ndungulile na Waziri Tibaijuka kuhusu
kukiukwa kwa sheria ya mipango miji.
“Huu ni udhaifu mkubwa kwa
upande wa utawala kwani ndio kinakuwa chanzo cha mgogoro usiokwisha na
kusababisha hata kama kuna nia njema basi dhamira ovu inaanza kujitokeza wazi
mbele ya uso wa jamii,” alisema.
Mbunge huyo alisema katika
kikao cha bajeti mwaka jana, Bunge lilitoa mwongozo wa kumaliza mgogoro kwa
kuitaka serikali kupitia kwa Waziri Tibaijuka, kukaa na mbunge na wananchi
kumaliza mtafaruku huo, lakini hadi sasa kikao hicho hakijawahi kufanyika.
Kibaya zaidi Mdee alisema
wizara imeandaa Master Plan bila kuwashirikisha wananchi kupata maoni yao kama
sheria ya mipango miji inavyotaka.
“Mheshimiwa Spika, kambi
rasmi inauliza je hayo maoni ya mwanzo yalikusanywa lini? Kama yalikusanywa
mbona wananchi wanalalamika? Tunamtaka waziri atoe majibu ya kueleweka,”
alisema Mdee.
Mbunge huyo ambaye jana
alikuwa mwiba kwa Waziri Tibaijuka, alihoji kama kuna uhalali wa kuendelea na
mpango huu kabambe pamoja na wakala wa kuendeleza mji wa Kigamboni.
Mgogoro wa ardhi Chasimba
Akizungumzia mgogoro wa
Chasimba, Mdee alisema kwa muda mrefu wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakiitwa
wavamizi.
Lakini alisema ukweli
unabaki kuwa kuna siri kubwa sana iliyojificha ya namna Kiwanda cha Wazo Hill
kwa kutumia viongozi wa kijiji wa kipindi kuuza ardhi ya wananchi wakiwa ndani,
kisha kubadilisha mipaka na hatimaye kiwanda hicho kupewa hati kinyemela.
Kwa mujibu Mdee, mahakama
iliamua- wananchi wahame, lakini pia iliiagiza serikali kwamba wajibu wake
katika mgogoro huu ni kuwapatia makazi mbadala.
Alisema amri hiyo
ilishindwa kutekelezwa kwa madai ya ukosefu wa fedha na eneo la kuwahamishia.
“Mheshimiwa Spika.
hatimaye ‘inasemekana’ wizara ilipata ‘eneo’ la ekari 1,000 ukilinganisha na
ekari 630 za eneo la Chasimba, mchakato ulisababisha kuitisha kikao cha
wananchi, waziri na timu yake na mthamini mkuu wa serikali na timu yake,
walifikia muafaka wa wananchi kufanya tahmini na kulipa fidia wote
waliotathminiwa ambao jumla yao ni 4096,” alisema.
Mdee alisema wananchi hao
waliahidiwa kulipwa sh 15,000 kwa mita moja ya mraba, pamoja na viwanja
mbadala.
“Mheshimiwa Spika, lakini
katika kile kilichoonekana kuna harufu ya wizi na rushwa, katika kikao
kilichofanyika baa kikiwahusisha Waziri Tibaijuka, Diwani wa Kata ya Bunju,
Mwenyekiti wa Mtaa wa Basihaya, pamoja na inayoitwa ‘Kamati ya Wananchi’, Waziri alisema wananchi hawatalipwa tena sh 15,000 kwa Square Metre, bali
watapewa 5,000 ya kifuta jasho,” alisema.
Mbunge huyo wa CHADEMA,
alisema kilichofanyika baadaye, waziri na timu yake walianza kutumia vitisho na
kuwataka wananchi wafungue akaunti na kujaza fomu zisizo hata na muhuri wala
nembo ya wizara, zikiwataka waandike namba zao za akaunti na kwamba wangekutana
na pesa zao huko huko.
Na zaidi ya hiyo, wananchi
hao waliambiwa asilimia 10 ya pesa watakayolipwa itakwenda kwenye Saccos,
ambayo haijulikani ni ya nani, imeundwa lini na kwa madhumuni gani.
“Mheshimiwa Spika, mpaka
sasa waziri akiulizwa tutajazaje fomu na kuandika akaunti ili tuingiziwe pesa
ambazo hata hatujui ni kiasi gani, anajibu utakachokikuta hata kama ni 200 ndio
halali yako,” alisema Mdee.
Dalili za wizi
Kwa mujibu wa nyaraka-
ambazo kambi ya upinzani inazo, Mdee alisema kaya 4,096 zilizofanyiwa tathmini,
kwa kiwango cha sh 15,000 kwa mita moja ya mraba, fedha iliyotakiwa kulipwa ni
sh 47,368,357,520/-.
Alisema hiyo
inathibitishwa kwa barua ya tarehe 8/11/2013, yenye kumbukumbu namba CBA
171/312/01 kutoka kwa Waziri Tibaijuka kwenda kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Alisema katika barua
husika, pamoja na mambo mengine anampa taarifa waziri mkuu juu ya uhitaji wa sh
69,051,215,426 kama hitaji la fedha kwa zoezi zima la kulipa fidia kutwaa eneo
la makazi mbadala, kulipanga eneo jipya kimipango miji, kupima viwanja na
kuweka miundombinu ya msingi hususan barabara, maji, shule ya msingi,
dispensari.
Mdee alisema kitendo
kinachofanywa na waziri pamoja na uongozi wa Kiwanda cha saruji cha Wazo
kumlazimisha Waziri Mkuu akubali deal hiyo ifanyike haraka, inatia shaka kwani
huenda Waziri Tibaijuka atafaidika na mpango huo.
Mdee alisema kwa mujibu wa
tathmini, kaya zilizofanyiwa tathmini, na kutakiwa kupewa viwanja mbadala ni
4,096, lakini wizara inataka kuvilipia viwanja 4,500 na vilivyosalia 404 vya
ziada havijulikani ni mali ya nani.
Taasisi
yenye mahusiano na Tibaijuka
Mdee,
alizidi kumkaba koo Waziri Tibaijuka kwamba ana mahusiano na taasisi ya
Tanzania Women Land Acces Trust- (TAWLAT) ambayo imo katika mchakato huu tata.
Alisema
kuwa ushahidi unaonyesha kuwa waziri alikishauri kiwanda kuingia mkataba na
taasisi hiyo ya TAWLAT kutoa elimu na kuendesha mazungumzo na viongozi na
wananchi wa Chasimba juu ya mgogoro wao.
Kutokana
na mazingira hayo, Mdee alisema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina shaka
juu ya ushiriki wa shirika hilo katika mgogoro wa Chasimba pamoja na kazi
nyingine za wizara.
Alisema
kwenye mgogoro huo wa Chasimba, taasisi hiyo ililipwa sh milioni 300 na milioni
nyingine 300 zilizotolewa na Halmashauri ya Kinondoni.
“Mheshimiwa
Spika, kwa maelezo ya Waziri Tibaijuka, katika kazi hiyo taasisi hiyo ililipwa
sh milioni 300 na katika mchanganuo niliouainisha hapo awali, wangelipwa sh
milioni 500 kwa kazi hiyo. Nikiwa kama mbunge wa jimbo husika, nikuhakikishie
kwamba hiyo taasisi haikufanya kazi yoyote,” alisema.
Mdee
alisema kazi ya uthamini ilifanikiwa baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Upimaji
na Ramani na timu toka Wizara ya Ardhi kuja ofisini kwake kumuomba awasaidie
kutuliza upepo kwani wananchi walikuwa wakiwarushia mawe.
“Mheshimiwa
Spika, ilituchukua mikutano mikubwa si pungufu ya sita mimi nikiwa msemaji mkuu
kuwaelimisha wananchi nia ya tathmini huku wakubwa hawa wakiwahahakikishia
kwamba watalipwa 15,000 kwa square metre na kupewa maeneo mbadala. Hakukuwa na
cha TAWLAT, wala Waziri Tibaijuka,” alisema.
Kutokana
na sarakasi hizo, Mdee alisema kambi ya upinzani inaitaka Takukuru kufanya
uchunguzi wa ushiriki wa TAWLAT kuhusu ushiriki wake wa shaka katika kazi
kadhaa za Wizara ya Ardhi na wasipofanya hivyo, watawasilisha hoja binafsi-
kuhusu sakata hili.
CCM
wakutana ghafla
Katika
hatua inayohusishwa na ugumu wa bajeti ya wizara hiyo, wabunge wa CCM
walikutana ghafla ambapo pamoja na mambo mengine walijadili mwelekeo wa bajeti
ya wizara hiyo.
Karibu
wabunge wote waliochangia bila kujali itikadi, waliishambulia bajeti ya wizara
hiyo na kutishia kuondoa shilingi.
Mbali
ya wabunge wa CCM kutishia kuondoa shilingi, mawaziri wengi hawakuwemo wakati
Waziri Tibaijuka anasoma bajeti yake na taarifa zinadai kuwa wamemsusia kwa
vile amekuwa hashiriki kwenye bajeti za wizara nyingine kwa namna yoyote ile.
Mmoja
wa wabunge wa CCM, alisema kuwa chama kimeweka msimamo wa
kumnusuru Waziri Tibaijuka.
No comments:
Post a Comment