Upelelezi wa kesi ya kula njama na kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Euro 2,065,827.60 inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Rick Mahalu na wenzake wawili, umekamilika.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mtunza Fedha, Steward Prosper Migwano na Ofisa Utawala, Grace Alfred Martin.
Kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi Bw. Sivangilwa Mwangesi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Akiwasilisha madai hayo, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU), Bw Joseph Molle, alidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
`Mheshimiwa, uchunguzi wa shauri hili umekamilika kwa hiyo naomba tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali,` alisema Bw. Molle.
Mahakama iliridhia ombi la upande wa mashtaka na kupanga shauri hilo kusikiliza maelezo ya awali Aprili 23, mwaka huu.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wote kwa pamoja kutokana na nyadhifa zao mbalimbali wanadaiwa kula njama ya kuiba fedha za serikali katika maeneo mbalimbali ya jiji la Rome, nchini Italia.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa, washtakiwa wakiwa wafanyakazi wa serikali, waliiba vocha yenye namba D2/9 ya Septemba 2, mwaka 2002, wakiwa na lengo la kuipotosha serikali kuhusu bei halisi ya jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.
Ilidaiwa kuwa vocha hiyo ilikuwa imejazwa taarifa za uongo, ikionyesha kuwa bei ya jengo hilo ni Euro 3,098,741.58.
Katika shtaka la tatu ilidaiwa kuwa washtakiwa wakiwa na lengo la udanganyifu, walitumia mkataba wa mauzo ya Oktoba Mosi mwaka 2002, kuonyesha gharama za jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia ni Euro 3,098,741.58.
Pia, washtakiwa wanadaiwa kuwa, Oktoba 2002, katika Ubalozi huo, wakiwa na lengo la udanganyifu, walitumia mkataba huo wa uongo kuonyesha kuwa muuzaji wa jengo hilo amepokea Euro 3,098,741.58 kama malipo ya jengo hilo huku wakijua kuwa sio kweli.
Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa, Oktoba Mosi, 2002 washtakiwa waliiba Euro 2,065,827.60 mali ya Serikali ya Tanzania.
Washtakiwa walikana shtaka hilo na wako nje kwa dhamana, ambapo kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 23, mwaka huu maelezo ya awali yatakaposikilizwa.
- SOURCE: Nipashe 21st. March 2007
1 comment:
nahitaji kufahamu case registration number kwani nimejaribu kwa kila hali nimeshindwa kuipata. tafadhali ni muhimu katika research yangu.
Post a Comment