Thursday, March 22, 2007

Ajikamatisha mwenyewe kwenye treni ya mjini - Wakili mwendesha mashtaka asikia yote.

Jamaa huyo Mnorwejiani mwenye miaka 25 alikamatwa Februari mwaka jana kwa kuhifadhi bangi na kukutwa na risasi 9 bila kibali cha kumiliki silaha. Alipokamatwa na polisi mwaka jana jamaa alikana katakata kuwa hajishughulishi na biashara ya midaharati. Na kuwa hivyo vitu havikuwa vyake na kuwa alibambikiziwa na wasiomtakia mema. Jana jamaa huyo alitubu madhambi yake akiwa ndani treni ya mjini (ya namna hii pichani) na rafikiye wa kike, kuwa anaenda mahakamani kwenye kesi yake ya kukutwa na bangi gram 1,3 na risasi 9.

Wakiwa ndani ya "trikk", akamwambia rafiki yake kwa sauti ya kusikika na watu wengi waliokuwemo ndani, kuwa polisi walikuta bangi na risasi nyumbani kwake mwaka jana. Ni zake na ana uhakika wa kushinda kesi yake inayomkabili mahakamani, kwani atakana na polisi hawana ushahidi wa kumfunga.
Alizungumza hivyo bila kujua kuwa aliyekaa mbele yake ni nani.

Mbele yake alikuwa dada mmoja amejikalia kimya huku alisikiliza, alikuwa Polisi mwendesha mashtaka, Anette Berger ambaye naye aliamua kupanda "trikk" siku hiyo. Mwendesha mashtaka huyo alisikia yote aliyosema huyo jamaa. Waliposhuka kituo kilicho karibu na mahakama na kuingia ndani, mwendesha mashtaka alimwendea na kumwambia kuwa ni yeye ataendesha kesi yake na kuwa amesikia yote aliyozungumza kwenye ”trikk” jamaa alipagawa, akaharakisha kwenda kwa wakili wake na kumwelezea yaliyotokea. Alipoulizwa kama anakiri kosa la kukutwa na bangi na risasi, alikataa licha ya kuwa alikiri mbele ya kadamnasi wa watu kuwa ana makosa.

Mahakama ilikubali ushahidi uliotolewa wa kuwa jamaa amekiri akiwa ndani ya trikk na kumhukumu kifungo cha siku 15 jela na kulipa kroner 2000,- gharama za kuendesha kesi hiyo.

Na Mwamedi Semboja, mahakamani Oslo, Alhamisi, 21. Machi 2007.


No comments: