Monday, April 09, 2007

Askofu adai orodha ya vigogo wa unga

MIEZI kadha baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwepo kwa orodha ya wanaodaiwa kuwa ni wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya, kiongozi mmoja wa kidini nchini, ameitaka serikali kuiweka wazi orodha hiyo. Ombi hilo lilitolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa, kupitia mahubiri yake katika Ibada ya Ijumaa Kuu, iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Mtakatifu Albano jijini Dar es Salaam, jana.

Askofu huyo alisema vita dhidi ya dawa za kulevya inapaswa kutiliwa mkazo kwa sababu ina madhara makubwa, si tu kwa watu binafsi, bali hata kwa uchumi wa nchi. Alisema taarifa za vyombo vya habari za kuwepo kwa orodha hiyo, ya watu wanaodaiwa kuwa ni vigogo wa biashara ya dawa za kulevya, ilikuwa ni sehemu nzuri ya kuanzia vita dhidi ya dawa hizo. Alisema kwa mujibu wa vyombo vya habari, orodha hiyo ilihusisha baadhi ya wabunge, maaskofu na wachungaji na ilidhaniwa kuwa mwisho wa siku itawekwa hadharani, lakini hadi leo majina hayo hayajawekwa hadharani.

“Vita ile imeishia wapi? Ina maana hatuwapendi wanaokufa na madawa hayo? Ina maana na sisi viongozi wa dini tunahusika? Mbona majina hayo hayatangazwi? Lakini imekuwa ni kawaida kutangaziwa kila dawa hizo zinapokamatwa viwanja vya ndege au katika maeneo mengine bila kuwataja wahusika wakuu,” alisema Askofu Mokiwa.

Askofu huyo alisema athari ya dawa hizo ni kubwa kwa watu wanaopata matatizo ya akili, ambao aliwaita ‘mazezeta’ wanaongezeka, familia zinaathirika. Alisema yeye kama kiongozi wa kidini, angefurahi iwapo taarifa hiyo ingeanikwa hadharani kabla hajafa. “Athari ya madawa haya ni kubwa kwa kuwa mazezeta wanaongezeka na aibu ni kubwa katika familia, hivyo nitafurahi kabla mimi sijafa nikaipata hiyo orodha. Hata ikiwa kesho nitafurahi,” alisisitiza Askofu Mokiwa.

Alisema Tanzania hakuna viwanda vya kutengeneza dawa za kulevya, hivyo ni dhahiri kuwa zinaingizwa kwa wingi hapa nchini kutoka nje. Askofu huyo alisema kwa kuwa serikali ina jicho kubwa na mikono mirefu, alidhani kuwa ingechukua hatua zinazofaa kisheria kulimaliza tatizo hilo kabisa bila hofu. Aidha, askofu huyo alizungumzia pia tatizo la ujambazi na uvunjaji wa sheria, ambalo alisema ni eneo linaloacha majeraha mengi kwa Watanzania.

Katika mahubiri yake, Askofu Mokiwa aligusia kuhusu taratibu za umilikaji silaha, akionyesha wasiwasi kuwa huenda silaha nyingi zinazotumika katika ujambazi, ni zile zinazomilikiwa kihalali. “Serikali ifikirie upya umiliki wa silaha hizo, ikiwezekana tunaiomba ifunge kabisa maduka yanayouza silaha,” alisema Askofu Mokiwa. Alizungumzia pia vurugu katika taasisi za kidini na kubainisha kuwa, kumekuwepo na vurugu katika jamii ya Wakristo nchini, jambo ambalo limekuwa likisababisha uvunjaji wa amani makanisani.

“Wakristo mara zote wametafuta punda wa lawama kwa kutaja dini fulani ndiyo chanzo cha migogoro. Wakristo tumekuwa tukijidanganya kwa hali ya sasa, viburi vya kiroho vimeongezeka, kugombea uongozi, uinjilisti wa kuibiana Wakristo, siasa chafu kanisani, kupiga viongozi wa kiroho hata kuvunja fimbo ya uchungaji,” alisema Askofu Mokiwa.

Awali, alisema kuwa kizazi cha sasa kimejaa ukaidi kwani katika historia ya uumbaji, kizazi cha sasa ndicho kinachojulikana kwa vituko na uasi. “Kinachotafuna kanisa hivi sasa ni roho ya unafiki ndani ya kanisa. Kanisa limejaa idadi kubwa ya mapadri, wachungaji na maaskofu ambao ndio chanzo kikubwa cha kuharibu kanisa,” alisema. Alibainisha kuwa, hali hiyo ndiyo inayorudisha nyuma maendeleo ya injili.

na Lucy Ngowi

By Habari Tanzania | Published 07/04/2007


No comments: