Saturday, April 07, 2007

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 31 MACHI, 2007


Picha kutoka http://www.kikweteshein.com

Utangulizi

Ndugu Wananchi;

Leo katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi huu wa Machi, nitazungumzia mambo mawili. Nayo ni: Utoaji mikopo ya wajasiriamali wadogo wadogo na hali ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa na jitihada tunazozifanya kukabiliana nao.

Ndugu Wananchi;

Kabla ya kufanya hivyo, napenda kuitumia nafasi hii kutoa mkono wa heri na pongezi kwa ndugu zetu Waislamu na Wakristo hapa nchini. Kwa Waislamu nawatakia heri na fanaka tele katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W. Na kwa ndugu zao Wakristo nao nawatakia heri na fanaka tele katika sikukuu ya Pasaka ambayo ni kumbukumbu ya mateso, kifo na kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo.

Wakati nikiwatakia heri katika sikukuu hizi muhimu kwetu sote Watanzania, napenda kusema kuwa naungana nanyi katika sherehe hizo। Ni matumaini yangu kuwa sherehe hizo zitakuwa tulivu na salama. Napenda kuwahakikishia kuwa vyombo vyetu vya usalama vitafanya kila linalowezekana kulinda usalama wa Watanzania na mali zao wakati wote wa sherehe hizi.

Mikopo ya Uwezeshaji Wajasiriamali

Ndugu Wananchi;

Mwezi Januari mwaka huu Serikali ilianza kutekeleza mpango wake wa mikopo ya uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo wadogo nchini. Mpango huo unalenga kuwasaidia wananchi wa kawaida waweze kupata mikopo kwa masharti nafuu.

Shabaha yetu ni kuwa, kupitia mikopo hiyo wakopaji wataweza kuanzisha au kuendeleza shughuli za uzalishaji mali na huduma ambazo zitawapatia kipato zaidi na hivyo kuinua hali zao za maisha na kupunguza umaskini. Mikopo hiyo itawasaidia wananchi vijana na wanawake waweze kupata ajira kwa njia ya kujiajiri wenyewe.

Ndugu Wananchi;

Katika utekelezaji wa mpango huu, tuliamua kuwa kazi ya kutoa mikopo kwa niaba ya Serikali itafanywa na Mabenki ya Biashara, Benki za Wananchi na Asasi zinazotoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo. Kwa ajili hiyo Benki za Biashara za NMB na CRDB ziliteuliwa pamoja na Benki za Wananchi za Dar es Salaam, Mwanga na Mufindi na Benki ya Posta. Kadhalika asasi zinazotoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali wadogo wadogo nazo zitahusishwa. Mpaka sasa shilingi bilioni 10.5 zimekwishatolewa kwa mabenki ya NMB na CRDB, kila moja ikipata shilingi bilioni 5.25. Shilingi bilioni 10.5 zilizosalia za kupewa Benki za Wananchi, Benki ya Posta na asasi zinazotoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali wadogo bado hazijatolewa. Benki Kuu inaendelea kushughulikia suala hilo.

Kwa upande wa fedha zilizopokelewa benki za NMB na CRDB maelewano yalikuwa kwamba benki hizo zitatoa na kukopesha fedha yao ambayo itakuwa mara tatu ya zile walizopewa na Serikali। Kwa ajili hiyo basi benki hizo zitakopesha shilingi bilioni 31 badala ya zile shilingi bilioni 10.5 tu zilizotolewa na Serikali. Zile fedha za Serikali zitabakia kama dhamana kwa mikopo itakayotolewa na mabenki hayo.

Mafanikio Yameanza Kupatikana

Ndugu Wananchi;

Tayari Benki za NMB na CRDB zimeanza kutoa mikopo kwa wananchi mmoja mmoja na vyama vya kuweka na kukopa. Kwa mfano, hadi kufikia tarehe 23 Machi, 2007 benki ya NMB ilikwishatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.419 kwa mikoa yote ya Tanzania Bara isipokuwa Ruvuma na Rukwa. Katika zoezi hilo waombaji 2,013 nchini kote wamepatiwa mikopo.

Kwa upande wa Benki ya CRDB kiasi cha shilingi 397,660,000 kilikuwa kimeshakopeshwa kwa SACCOS nane zenye wajasiriamali 1,160. Wakati huo huo shilingi 725,660,000 za kukopeshwa SACCOS tatu zenye wajasiriamali 1,441 zilikuwa zinasubiri kibali cha Makao Makuu ya Benki hiyo.

Ndugu Wananchi;

Watu wengi binafsi, vikundi vingi na SACCOS nyingi zimejitokeza kuomba mikopo. Benki ya NMB imepokea jumla ya maombi 59,974 yenye thamani ya shilingi bilioni 105.2. Benki ya CRDB nayo imepokea maombi yenye thamani ya shilingi 8,070,382,,000 kutoka SACCOS 42 zenye wajasiriamali 17,454.

Ni wazi kuwa thamani ya maombi yaliyopokelewa na Benki ya NMB ni kubwa zaidi, kwa takriban mara saba, ikilinganishwa na shilingi bilioni 15 zilizotengwa na benki hiyo kwa ajili ya mikopo ya uwezeshaji katika awamu ya kwanza ya utekelezaji.

Ndugu Wananchi;

Kutokana na maombi kuwa makubwa kuliko uwezo uliopo Benki hiyo imeamua kusitisha upokeaji wa maombi mapya ya mikopo. Wameamua kuwa kwa sasa wafanye kazi ya kushughulikia maombi yaliyokwishapokelewa ambayo nayo hawataweza kuyatosheleza yote.

Naamini sababu zao ni za msingi kabisa kwani hakuna maana kuendelea kupokea maombi mapya wakati hata yale waliyonayo yamekwishazidi uwezo wao. Benki ya CRDB ndiyo bado ina uwezo wa kuendelea kupokea mikopo. Wao hawajafikia ukomo wa fungu lao walilotenga.

Ndugu Wananchi;

Taarifa zinaonyesha kwamba baadhi ya mikoa imeweza kuwasilisha maombi mengi na kuna baadhi ya wilaya hakuna maombi yaliyowasilishwa kabisa. Wakati mabenki yanaendelea kupitia maombi waliyopokea Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu zoezi hili ili kuhakikisha kuwa malengo yetu kwa kila mkoa kupata mgao wake wa mikopo yanatimizwa.

Vile vile, tutazungumza na mabenki ili kutafuta njia za kuhakikisha kuwa wananchi wa zile wilaya ambazo wanachelewa kuwasilisha maombi hawapotezi kabisa fursa hii। Serikali pia, itajaribu kuzungumza na mabenki ili kuona namna ya kuhudumia SACCOS katika wilaya ambazo benki ya CRDB haipo na NMB haitakuwa tayari kufanya hivyo.

Malalamiko na Matatizo

.Ndugu Wananchi;

Natambua kuwepo malalamiko na matatizo kadhaa kuhusu mikopo ya wajasiriamali ambayo ningependa kuyazungumzia leo. Kwa mfano, nilipokuwa wilayani Ngorongoro wiki chache zilizopita wananchi wa wilaya hiyo walitaka kujua hatima yao itakuwaje kwani watu wote wamechelewa kuwasilisha maombi ya mikopo wakati Benki ya NMB inasimamisha kupokea maombi mapya. Nilitoa majibu ambayo ningependa kuyarudia tena leo kwa manufaa ya wilaya zenye matatizo kama haya.

Ni makusudio ya Serikali kuona kuwa watu wa kila mkoa na kila wilaya nchini wanapata mikopo hiyo. Hivyo basi, pamoja na Benki ya NMB kusimamisha kupokea maombi kwa sasa, hapana budi utaratibu ufanywe ili, wilaya ambazo wananchi wake hawakuwahi kuwasilisha maombi ya mikopo nao wapate fursa hiyo.

Haiwezekani na wala haikubaliki kuwepo wilaya hata moja nchini ambayo watu wake hawatapata fursa ya kupata mikopo hii. Ikitokea hivyo dhamira ya kuanzisha mpango wa mikopo hii nchini itakuwa haikufikiwa.

Ndugu Wananchi;

Kumekuwepo pia malalamiko kuhusu utaratibu wa kupokea maombi, kuyashughulikia na kutoa mikopo. Zipo hisia kuwa utaratibu ni mgumu mno, mlolongo ni mrefu na kwa sababu hiyo kuna usumbufu na inachukua muda mrefu mno kwa mtu kupata mkopo.

Ni jambo jema kuwa na utaratibu wa kufanya mambo lakini ni vyema utaratibu ukawa rahisi na kwamba haichukui muda mrefu kutekeleza jambo. Hatuna budi basi kuuangalia upya utaratibu wetu wa sasa na kufanya marekebisho pale panapostahili ili mambo yaende vizuri. Yaani, iwe rahisi kwa waombaji kuomba na ichukue muda mfupi kwa waombaji kupata majibu na kupewa mikopo kwa wale watakaokubaliwa.

Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;

Pamoja na kusema hayo sina budi kusisitiza kuwa baadhi ya taratibu zilizowekwa ni muhimu kuwepo. Zina manufaa yake. Kwanza, zinasaidia kuhakikisha kuwa mikopo inawafikia walengwa. Hii ni mikopo ya raia Watanzania na ni mikopo ya maskini ili kuwawezesha wainue hali yao ya maisha. Si mikopo ya matajiri, wao mabenki yapo, tena yamejaa mabilioni ya fedha zinazosubiri wakopaji kama wao wawapatie.

Pili, taratibu hizo zinasaidia kuhakikisha kuwa fedha zilizokopeshwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na mikopo inalipwa। Mathalan, itasaidia kuhakikisha kuwa mtu aliyeomba mkopo wa kulima bustani ya nyanya hatatumia pesa hizo kumalizia nyumba yake au kulipia ada ya mwanae. Ni mambo ya maana, lakini siyo makusudio ya mkopo. Kama watu wataachwa wafanye hivyo mikopo haitalipwa na mtaji huu wote utakufa. Tukifikia hali hiyo dhamira yetu ya kuwa na utaratibu endelevu haitafikiwa. Itakuwa ni hasara kubwa ambayo ni lazima tuhakikishe kuwa hatufiki hapo.

Utaratibu Uzingatiwe

Ndugu Wananchi;

Utaratibu wa kuomba na kutoa mikopo unasisitiza mambo makuu yafuatayo: Kwanza, sharti muombaji awe na mradi unaokopesheka. Mwombaji awe na shughuli ya uzalishaji mali au utoaji huduma anayoiombea mkopo. Shughuli hiyo lazima ithibitike kuwa inafaa kupewa mkopo kwa kupitia taratibu zilizowekwa.

Pili, muombaji apitishe fomu zake za maombi kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa au Kijiji atakapofanya hiyo shughuli ili wamtambue na wautambue mradi.

Tatu, maombi yachambuliwe na Kamati ya Maendeleo ya Kata. Kamati hiyo itatoa maombi yake kabla maombi hayo hayajawasilishwa Benki kwa uamuzi wa mwisho.

Kwa upande wa SACCOS wanachama wanatakiwa kuwasilisha maombi yao kwa uongozi wa SACCOS yao kwa uchambuzi. Uongozi wa SACCOS ukiridhika huwasilisha maombi hayo kwa Afisa Ushirika wa Wilaya ambaye huthibitisha uhai wa SACCOS hiyo. Baada ya hapo uongozi wa SACCOS huwasilisha maombi hayo benki kwa uamuzi.

Ndugu Wananchi;

Wamekuwepo pia watu wanaolalamika kuwa kiasi cha fedha kinachotolewa katika mikopo hii ni kidogo mno na kwamba riba ya silimia 10 ni kubwa mno. Ni kweli kiasi kinachokopeshwa, yaani kati ya shilingi 50,000 na 5,000,000 si kikubwa lakini imefanywa hivyo kwa makusudi. Hii ni mikopo ya watu wenye kipato cha chini ambao katika hali ya kawaida benki haziwakopeshi. Maskini hakopesheki benki. Hana dhamana ya kukubalika na benki na wala hana uwezo wa kulipia gharama za kuombea mkopo.

Ndugu Wananchi;

Kwa kutambua ukweli huo na kwa nia ya kutaka kuwawezesha wananchi wenye vipato vya chini kupata mikopo ili na wao waanze safari ya kuelekea kwenye maisha bora, ndipo Serikali ilipoamua kuanzisha mpango huu wa mikopo. Hakuna sharti la kuwa na dhamana kwa wakopaji na wala hawalipi ada ya kuomba mkopo. Serikali imebeba mzigo huo. Fedha iliyotolewa na Serikali kwa benki ndiyo dhamana, na ndiyo inayofidia gharama za kuchukua fomu za maombi na za kushughulikia maombi.

Ndugu zangu;

Ni kweli kabisa kwamba ingekuwa vizuri kama mikopo hii ingekuwa haina riba yoyote. Tena lingefurahisha wengi na hususan wale ambao kiimani riba ni jambo haramu. Suala la kutokuwepo riba, lilizungumzwa kwa kina lakini lilikuwa gumu kulitekeleza. Sababu ya msingi ni gharama nyingine za kibenki zilizobaki hata baada ya Serikali kubeba mzigo wa dhamana na gharama za kuomba mkopo.

Ndiyo maana mikopo hii ina riba. Hata hivyo, ndugu zangu, ukilinganisha na riba ambazo kwa kawaida huwa zinatozwa na mabenki haya kwa mikopo ya namna hiyo riba inayotozwa kwa mikopo hii bado ya chini.

Vile vile unapolinganisha na riba inayotozwa na asasi za fedha zinazotoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo, riba inayotozwa kwa mikopo hii bado ni nafuu sana. Nyingi ya asasi hizo hutoza riba ya zaidi ya asilimia 30 na nyingine hufikia hata asilimia 40 au zaidi.

Ndugu Wananchi;

Nimeyaeleza haya kujaribu kufafanua baadhi ya mambo yanayoleta utata katika utaratibu mzima wa mikopo ya wajasiriamali wadogo wadogo. Sikuyamaliza maswali yote waliyokuwa nayo wananchi, naamini tutapata fursa siku zijazo kuyafafanua. Lakini pia, viongozi wenzangu taifani, mikoani na wilayani watasaidia kuyafafanua. Waendeeni, waambieni. Watafurahi kuwasaidia kwani ni wajibu wao.

Ndugu Wananchi;

Nauona mpango wa mikopo ya wajasiriamali kuwa ukombozi wa wanyonge. Kila kitu kina changamoto zake. Kuwepo kwa changamoto kusitukatishe tamaa bali kutuongezee ari ya kutafuta mbinu na maarifa ya kuzishinda. Maombi yangu kwa wadau wote ni kuwepo na ushirikiano miongoni mwetu. Pawepo na mawasiliano ya urahisi miongoni mwa wadau ili tatizo linapotokea habari ziwafikie wahusika kwa wakati. Naomba sote tushirikiane na tushikamane kwa dhati katika kuhakikisha kuwa mpango huu unafanikiwa kutimiza malengo yake.

Tuhakikishe kuwa taratibu zilizowekwa zinafuatwa lakini urasimu na ucheleweshaji usiokuwa wa lazima unaepukwa. Pia tuhakikishe kuwa mikopo inatumika kwa shughuli iliyokusudiwa na inarejeshwa kwa wakati ili na wengine nao waweze kukopeshwa. Tukiyazingatia na kuyafanya haya tutakuwa tumejenga msingi mzuri wa kuwapatia Watanzania wa kawaida fursa ya kubadili maisha yao kuwa mazuri zaidi kuliko yalivyo hivi sasa.

Ndugu Wananchi;

Naomba nimalizie mazungumzo yangu kuhusu mikopo kwa kutoa wito kwa Watanzania wenzangu tunaotaka mikopo kuwa na moyo wa subira. Muda utahitajika tangu mtu awasilishe maombi mpaka atakapopata. Hatuna budi kulitambua hilo na kuwa na subira nalo.

Lakini, kubwa zaidi ni ule ukweli kwamba si kila mmoja aliyeomba mkopo atapata wakati huo huo. Kama tulivyoona maombi ni makubwa kuliko fedha iliyopo. Kwa vyovyote vile, wapo watakaopata mwanzo na wapo watakaopata baadaye baada ya wale wa mwanzo kuanza kulipa.

Nawasihi Watanzania wenzangu tuutambue ukweli huo na kuukubali, ndiyo maana nawasihi tuwe na moyo wa subira। Kutaka wewe uwe wa mwanzo ndiyo ubinadamu, lakini ni vyema kutambua kuwa kwa hali ilivyo unaweza usiwe wa mwanzo. Ikitokea hivyo kubali na endelea kusubiri. Utaratibu huu ni endelevu. Si wa mara moja.

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa

Ndugu Wananchi;

Nchi yetu hivi sasa imekumbwa na tatizo la ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa yaani kwa Kiingereza Rift Valley Fever au kwa kifupi RVF. Ni ugonjwa hatari unaoua wanyama na binadamu pia.

Homa ya Bonde la Ufa ni ugonjwa wa mifugo na mwanadamu hupata maradhi hayo kwa kula nyama ya mnyama aliyeathirika.

Vile vile mnyama na mwanadamu wanaweza kupata maradhi kwa kuumwa na mbu wa aina ya Aedes mwenye wadudu wa maradhi hayo.

Mbali ya kuua mifugo mingi ugonjwa huu pia umesababisha vifo vya wananchi wenzetu katika baadhi ya mikoa hapa nchini. Hadi kufikia tarehe 28 mwezi huu watu 33 walikuwa wamepoteza maisha yao na wengine 119 walikuwa wameambukizwa.

Kwa upande wa mifugo mikoa ambayo imekumbwa na ugonjwa huu ni Dodoma, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Iringa, Singida na Mbeya. Mikoa ambayo watu wameathirika na hata baadhi yao kufariki dunia ni pamoja na Manyara, Tanga, Dodoma na Morogoro. Mikoa ya Dar es Salaam na Singida pia inao wagonjwa wachache wenye kuonyesha dalili za ugonjwa huo ambao wanaendelea kuchunguzwa.

Ndugu Wananchi;

Napenda kuchukua fursa hii kuwapa pole Watanzania wenzetu wote walioathirika na ugonjwa huu hatari. Kwa wale waliotangulia mbele ya haki, tunawaomba ndugu na jamaa zao wapokee mkono wetu wa rambirambi na pole zetu nyingi. Tunaelewa machungu ya kupotelewa na wapenzi wao. Tunajumuika nao na kuomboleza nao katika wakati huu mgumu wa machungu mengi na majonzi tele. Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu awape marehemu wetu hao rehema na azilaze roho zao mahali pema peponi.

Kwa wagonjwa wanaoendelea kupata matibabu tunawaombea wapone haraka ili wajiunge tena na familia zao na jamii nzima ya Watanzania katika ujenzi wa Taifa। Kwa wenzetu waliopoteza mifugo tunawapa pole kwa kupoteza rasilimali muhimu. Wasivunjike moyo, ndiyo mitihani ya dunia. Kuteleza si kuanguka.

Hatua Zinazochukuliwa na Serikali

Ndugu Wananchi;

Serikali inatambua uzito wa tatizo linalotukabili na inafanya kila iwezalo kutokomeza ugonjwa huu. Katika mkakati tuliouandaa hadi sasa tumechukua hatua zifuatazo:

Kwanza, tumezuia kufanyika kwa minada ya mifugo kote nchini. Hatua hii ni ya muda inayolenga katika kudhibiti kuenea kwa ugonjwa. Minada itaruhusiwa tena kufanya kazi pindi hali itakaporejea kuwa nzuri.

Pili, tumeimarisha utoaji wa chanjo za mifugo dhidi ya ugonjwa huu kwenye maeneo yote yenye mifugo. Hadi sasa tumeshatumia kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kununulia chanjo na vifaa vingine vya kukabiliana na ugonjwa. Tayari tumeagiza dozi milioni mbili za chanjo ya RVF. Kati ya hizo, dozi 736,600 zimeshapokelewa na kusambazwa kwenye wilaya zilizoathirika na zile zilizo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa.

Tatu, tumeandaa chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, mpango wa dharura wa kitaifa wa kudhibiti ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa। Mpango huu utagharimu dola za Kimarekani takribani milini 12.3. Tunaendelea kuwasiliana na marafiki zetu wa nje kuhusu uwezekano wa kutusaidia kugharamia mpango huu mapema iwezekanavyo ili kunusuru mifugo yetu na maisha ya watu.

Wajibu wa Kila Mmoja Wetu

Ndugu Wananchi;

Jukumu la kupambana na ugonjwa huu ni letu sote. Kila mmoja wetu pale alipo anao wajibu wa kuhakikisha kuwa anachukua tahadhari zote muhimu zitakazosaidia katika kukabiliana na ugonjwa huu. Hivyo nawaomba tuzingatie mambo yafuatayo:

Kwanza, tuhakikishe kwamba mifugo yote inapata chanjo. Hii ndiyo kinga yetu ya kwanza ya kupambana na ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa. Serikali inafanya jitihada ili kuhakikisha kwamba dozi za kutosha za chanjo zinapatikana. Hivyo nawaomba watu wote wapeleke mifugo yao ikachanjwe mapema iwezekanavyo.

Pili, tuache tabia ya kuhamisha mifugo kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kiholela. Uhamishaji holela wa mifugo unachangia katika kueneza ugonjwa. Aidha, unarudisha nyuma jitihada zetu za kudhibiti ugonjwa huu hatari.

Tatu, tuepuke kuchinja wanyama na kuchuna ngozi bila kuchukua tahadhari za kujikinga. Vile vile tujiepushe na kushika damu, majimaji na nyama ya mnyama anayehofiwa kuwa na ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa.

Nne, tusile nyama ya mnyama aliyekufa kwa ugonjwa huu. Inashangaza sana kusikia kuwa baadhi ya wenzetu wanadiriki kufukua mizoga iliyozikwa na kula nyama yake. Ndugu zangu, ni uchu wa kiasi gani huo unaotufanya hata tupuuze tishio kubwa kwa maisha ya mwanadamu kama hili la ugonjwa huu. Nawasihi tusikilize ushauri. Wahenga wamesema “asiyesikia la mkuu huvunjika guu”.

Tano, tuepuke kunywa maziwa yasiyochemshwa vizuri. Siku zote tuchemshe maziwa vizuri kabla ya kuyanywa.

Sita, wataalam na watendaji kwenye ngazi ya wilaya na vijiji wasimamie kwa ukamilifu utekelezaji wa Sheria ya Magonjwa ya Mifugo ili kudhibiti kuenea zaidi kwa ugonjwa huu.

Saba, wananchi watumie vyandarua hasa vile vilivyowekwa dawa ili kujikinga na mbu. Ndugu zangu, tukumbuke kuwa ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa unaenezwa pia na mbu aina ya Aedes. Hivyo kinga dhidi ya mbu ni jambo muhimu sana.

Na nane, tuongeze juhudi za kudhibiti mbu ili tupunguze kushamiri kwa mbu kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Watu wafukie mazalia ya mbu na pale inapowezekana wanyunyizie dawa.

Ndugu Wananchi;

Katika mapambano yetu dhidi ya ugonjwa huu, vyombo vya habari vinalo jukumu kubwa la kusaidia kuelimisha umma kuujua ugonjwa na jinsi ya kujikinga nao। Nawaomba mtimize wajibu wenu huo wa msingi kwa ukamilifu. Nawashukuru kwa hatua tuliofikia sasa naomba waendelee kufanya vizuri zaidi. Nawaomba wawe na ushirikiano na mawasiliano ya karibu na mamlaka husika na hasa wataalamu husika ili kuepuka kuandika au kutangaza habari ambazo hazijathibitika.

Hitimisho

Ndugu Wananchi;

Ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wetu atazingatia mambo ya msingi katika mapambano yetu dhidi ya ugonjwa huu. Hususan naomba tuzingatie ushauri wa wataalam utakaoendelea kutolewa mara kwa mara. Mimi naamini kuwa kama tukiyazingatia hayo tutaweza kuzuia kuenea na hatimaye kuutokomeza ugonjwa huu hatari mapema iwezekanavyo.

Watanzania tunayo sifa moja kubwa. Nayo ni kuwa pale tunapokabiliwa na adui siku zote huwa wepesi sana katika kuunganisha nguvu zetu na kupambana nae.

Ndugu zangu, ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa ni adui hatari anayetaka kutudhalilisha na hata kutuangamiza. Naamini kama ilivyo kawaida yetu tutaunganisha nguvu zetu ili tuweze kumtokomeza adui huyu mapema iwezekanavyo.

Na, katika vita hii kila mmoja wetu analo jukumu lake la kufanya. Naomba basi kila mmoja wetu atekeleze jukumu lake ipasavyo ili tuweze kuushinda na kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Homa ya Bonde la ufa. Inawezekana Timiza Wajibu Wako!

Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania!

Asanteni kwa Kunisikiliza!

Chanzo cha habari: Tanzanet mailing list (list@tanzanet.org), Ijumaa Aprili 6, 2007.

No comments: