(Procolobus kirkii) Zanzibar Red Colobus
na Tina Mlonda
TUMEZOEA kuona wanyama jamii ya nyani wakizunguka kwenye mashamba yetu. Kwetu sisi wakulima, mara nyingi ni wanyama wanaoharibu mazao, hasa mahindi yakiwa shambani. Ndipo usemi wa “ukicheka na kima utavuna mabua” ulipoanza. Pamoja na yote mabaya, lakini kuna mengi ya kujivunia kuhusu wanyama hawa kwani ni urithi wetu. Pia kuna ambao hupatikana Tanzania ambapo watalii hulazimika kuja kwetu kuwaona. Wanyama hao jamii ya nyani ni pamoja na mbega mwekundu wa Iringa na kima punjuni au mbega mwekundu wa Zanzibar.Leo nitazungumzia kima punjuni au mbega mwekundu wa Zanzibar. Kwa Kiingereza hujulikana kama “Zanzibar Red Colobus” au “Kirk’s Red Colobus”. Jina la Kirk ni la Mzungu aliyewahi kuishi visiwani Zanzibar miaka ya enzi za ukoloni, ambaye alimtambua mnyama huyu na kufanya wanasayansi nao watake kumjua.
Mzungu huyo alikuwa akijulikana kama Sir John Kirk. Mnyama huyu ana manyoya ya rangi nyekundu iliyoiva na nyeusi sehemu za mgongoni. Uso wake mweusi una taji la manyoya meupe. Ana alama za rangi ya pinki kwenye midomo na pua. Ana mkia mrefu ambao una rangi nyeusi kwa juu na nyeupe kwa chini. Hupatikana kwenye hifadhi za misitu ya Jozani, Ngezi huko Zanzibar. Kima punjuni huishi kwenye kundi la wanyama kati ya thelathini mpaka hamsini. Humo huwa kuna madume wanne na majike mengi na pamoja na watoto. Ni wanyama ambao huishi kijamii zaidi. Hupenda kucheza na kutoana chawa wakati wa kupumzika.
Utafutaji wa chakula hufanywa na kundi zima. Madume hutoa mlio fulani ambao huutumia kuita wenge kwenda kutafuta chakula. Chakula chao mara nyingi ni majani mabichi, vikonyo vya majani, maua na matunda mabichi. Ni aina ya wanyama ambao hawali matunda mabivu. Hii ni kwa sababu matumbo yao ambayo yamegawanyika sehemu nne hayawezi kumeng’enya sukari. Hula pia mkaa, ambao huaminika kuwa husaidia kwenye mmeng’enyo wa chakula. Mkaa huu huondoa sumu itokanayo na majani waliyokula.
Hubeba mimba kwa muda wa miezi mitano ambapo kawaida huzaliwa mtoto mmoja. Mtoto huyo hukaa na mama yake akinyonyeshwa kwa miezi mitatu. Tabia moja ya ajabu kwa wanyama hawa ni kuwa unaweza kukuta dume mkubwa akiwa ananyonya kwenye matiti ya jike. Wanyama hawa wana uzito kati ya kilo 5 na gramu 200 na kilo 11 gramu 300.
Watu wa Zanzibar huamini kuwa mnyama huyu ana sumu hivyo humuhusisha na imani za kichawi. Pia huaminika kuwa mnyama huyu anapokuwa sehemu fulani, basi miti na mazao ya sehemu hiyo hufa. Na ikitokea kuwa akaliwa na mbwa, basi mbwa huyo hunyonyoka manyoa. Wana harufu kali (ndio mwanzo wa neno punju), hivyo wanyama hawa hawafugwi. Wanyama hawa wako kwenye hatari kubwa ya kupotea na tayari Shirika la Kuhufadhi Wanyamapori Duniani (IUCN) limewaweka kwenye mstari mwekundu. Hii ni kutokana na makazi yao ya asili ambayo ni misitu kuharibiwa. Tabia za binadamu ambazo ni hatari kwa makazi yao ni pamoja na uvunaji wa miti kwa ajili ya mbao, uchomaji wa misitu na usafishaji wa misitu kwa ajili ya mashamba.
Inasadikiwa kuwa idadi ya wanyama hawa iko chini ya 1,500 tu.
Mradi wa kuhifadhi msitu wa Jozani, yaani Jozani-Chwaka Bay Conservation Project, uliokuwa kati ya mwaka 1995 mpaka mwaka 2003, ulimchagua mnyama huyu kuwa kwenye nembo ya utunzaji mazingira Zanzibar. Huyo ndiye mnyama aitwaye kima punjuni, ambaye anapatikana Zanzibar peke yake. Jamani tuamke Watanzania tuache tabia mbaya ya uharibifu wa mazingira kwani tukiendekeza tutampoteza mnyama huyo. Pia nakukumbusha kutembelea hifadhi zetu ili kujionea urithi halali tulioachiwa na Mwenyezi Mungu.
tcharles82@yahoo.co.ukChanzo cha habari: http://www.freemedia.co.tz
1 comment:
Kwa habari zaidi juu ya huyu kima punjuni angalieni:
http://www.galenfrysinger.com/red_colobus.htm
Pwagu na Pwaguzi
Post a Comment