Sunday, April 01, 2007

Waliomjenga Rais Kikwete ndio wanaombomoa


Ansbert Ngurumo.

JUMAPILI iliyopita, nilijadili ajabu ya Rais Jakaya Kikwete kusifiwa mno na vyombo vya habari hata kabla hajaanza kazi, huku baadhi ya wapambe wakimlinganisha na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, na kusisitiza kwamba ‘Kikwete zaidi,’ na wengine wakidai kwamba Kikwete ni ‘Nyerere mpya.’

Nilihitimisha kwamba sifa nyingi hizi za vyombo vya habari zilizua hisia kwamba ‘waandishi wamehongwa’ ili kuunda mazuri ya Kikwete na kumpamba, wanajikomba kupata vyeo, huku wengine wakisema ‘wapambaji’ hawa hawajui kufanya vizuri kazi waliyopewa, kwani kila mmoja anaona kwamba mengi wanayoandika yanaundwa na yanatiwa chumvi.

Hizi ndizo hoja ambazo niliahidi kuziendeleza kuanzia leo. Labda ni vema niseme mapema kwamba, kwa kutazama mwenendo wa mambo sasa, idadi ya waliokuwa wakimsifu Rais Kikwete katika wiki zake za kwanza madarakani, imepungua. Si kwamba wapambe wamemkimbia, bali wameanza kuondokewa na ulevi uliowakumba wakati wa kampeni, wameanza kutazama mambo kwa macho yao wenyewe na kufikiri kwa akili zao wenyewe.

Wamejikuta wana mambo mawili, na kati ya hayo wanachagua mojawapo: Kumsifu kama wana mambo ya kusifia au kunyamaza pale wanapogundua kwamba waliyokuwa nayo yameisha na hawawezi kuyarudiarudia; huku wakishuhudia wakosoaji wa Kikwete wakiongezeka makali kwa kutaja udhaifu huu na ule, na kasoro moja baada ya nyingine katika mwaka mmoja na ushehi wa utawala wake.

Kinachoongeza makali ya wakosoaji sasa ni taarifa za baadhi ya vyombo vya nje, zikiwamo za majuzi zilizoandikwa katika jarida la Economist. Kwamba baadhi ya watu waliokuwa mstari wa mbele kummwagia sifa Rais Mkapa sasa wanakuwa wepesi kumkosoa Rais Kikwete, ni jambo linalowafadhaisha wapambe wa Kikwete na washauri wao. Lakini huo ndio ukweli wa maisha, kwamba kuna sehemu mbili za shilingi.

Ni vema niseme pia kwamba kinachomponza Rais Kikwete na wapambe wake, wanataka wananchi waonyeshwe sura moja tu ya Kikwete - uzuri na uwezo wake! Na kinachowaponza zaidi sasa, ni sifa alizopewa kabla hajawa rais. Zilikuwa nyingi na hazionekani akiwa ofisini.

Maana Kikwete hakuwa mgeni kwetu. Amekuwa serikalini kwa zaidi ya miaka 10. Amekuwa mbunge wa Chalinze kwa muda mrefu. Alikuwa mtu wa kawaida, akiwa na sifa za ucheshi na utanashati.

Lakini ghafla kampeni zilipoanza, watu walijengwa kuwa sasa nchi imepata nabii na mkombozi. Mbwembwe zilizoandikwa na kutangazwa vilionyesha kwamba dawa ya matatizo ya Tanzania imepatikana. Wengine walifika mahali pa kuandika hata kuwa Kikwete ni ‘Tumaini Lililorejea.’ Yote haya yaliwapa wananchi matumaini makubwa mno, na kumfanya Rais Kikwete kuwa mtu ‘spesho’; wakamfanya kuwa na uwezo asiokuwa nao.

Ajabu ni kwamba, sasa hivi yanapoanza kutokea yasiyotarajiwa yanayosemwa sana na wakosoaji wa Serikali ya Kikwete, maisha ya wananchi yanapoanza kuwa magumu na ya dhiki kuliko kuwa bora kama walivyoahidiwa na kuaminishwa, tuhuma za rushwa ndani ya mikataba (tena inayowahusu wakubwa na rafiki zao) zinapochomoza mapema hivi, huku Kikwete mwenyewe akihusika moja kwa moja na kuruhusu au kuzuia baadhi ya mikataba inayolalamikiwa na akijaribu kulinda waziwazi makosa yaliyotendwa na watangulizi wake, wanapoanza kuikimbia kaulimbiu ya ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania;’ watu wale wale ndio sasa wanaolalamika kwamba si vema kumlaumu rais sasa hivi; kwamba ni mapema mno.

Ni watu wale wale waliokuwa wanaambiwa kuwa ilikuwa mapema mno kuanza kumwaga sifa kemkem kwa rais mwanzoni mwa utawala wake. Naye kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari, sasa anasema asihukumiwe sasa, bali apimwe baada ya miaka mitano ya uongozi wake. Mbona hakusema hivyo alipokuwa anasifiwa? Kwa nini hakuwaambia waliomsifu kuwa wasubiri baada ya kuona kazi yake ya miaka mitano?

Habari zinasema kwamba, baadhi ya wasaidizi na washauri wake wameshaanza mkakati wa kusambaa tena kwa vyombo vya habari vinavyomkosoa Kikwete ‘kupoza makali’ kwa kubembeleza hata kutoa kauli za vitisho, huku wakionya kuwa ‘wakosoaji wasisahau kwamba rais ni mwanajeshi.’ Kumbe!

Si huyu ndiye alinukuliwa akiwaambia wabunge wa chama chake kwamba anataka akosolewe? Haikuwa kauli ya dhati? Na kama wapambe wake wana mazuri yake, si wayaandike kuweka sawa takwimu na vielelezo vya wakosoaji? Au si waiache jamii ione na kusikia alichofanya na alichoshindwa?

Si wajinga. Wanajua wanachofanya, maana wanakumbuka walichofanya kwa zaidi ya miaka 10 kumsimika Kikwete katika mioyo ya Watanzania. Mkakati wao (wanamtandao) wa kwanza ulikuwa kuwabomoa watu waliodhaniwa kuwa wanautaka urais, ili kupunguza washindani wa Kikwete wakati utakapowadia.

Bahati mbaya hata walioshughulikiwa hawakujua kinachoendelea, na walipojua hawakuwa na mbinu; na walipojaribu walikuwa wamechelewa.

Miongoni mwa waathirika wakubwa wa awali wa mkakati huu ni Waziri Mkuu wa wakati huo, Frederick Sumaye. Miongoni mwa habari chafu za mwanzo dhidi ya Sumaye ni kile kilichosemekana kwamba ziara yake moja katika nchi za Marekani na Ulaya ilitumia pesa za Watanzania shilingi milioni 500.

Ikafuata nyingine kwamba alikopa shilingi milioni 50 kutoka PPF. Ikaja nyingine ya Sumaye kukodishwa eneo kubwa la ardhi Kibaigwa mkoani Dodoma; mara Kibaha, mkoani Pwani. Sumaye akaonekana kiongozi asiyejali Watanzania; mroho wa mali za wananchi. Akahusishwa na udanganyifu, rushwa na uchafu mwingi.

Ukweli ni kwamba habari hizi ziliandikwa na vyombo vya habari, lakini hazikuchunguzwa na waandishi wa habari. Zilichunguzwa na kusambazwa na wanamtandao. Na zilitimiza azma ya kumfanya Sumaye aonekane mchafu, dhaifu, mroho wa mali na mla rushwa! Nina hakika kamba baadhi ya walioandika na waliosoma habari za Sumaye, hawakujua kwamba nyuma yake kulikuwa na kundi la watu wanaoshindania urais wa Tanzania.

Hizi zilikuwa zinapenyezwa na kundi la wanamtandao zikiwa na taarifa muhimu bila makosa na zikiongezwa chumvi inayostahili kutimia lengo la wahusika – kwa ajili ya Kikwete. Katika hili, na katika mengi ya aina hiyo, waandishi walitumika; wala hawakuhongwa na mtu kufanya kazi hiyo.

Jambo ambalo wengi hatukujiuliza ni kwa nini iliandikwa habari moja ya safari ya Sumaye nje ya nchi, ilhali viongozi wengine wakiwamo Rais Mkapa na Waziri Kikwete walikuwa ‘wanaishi kwenye ndege’? Mbona hadi sasa hatuelezwi wao walitumia kiasi gani kwa kila safari?

Lakini zaidi ya hayo, pesa hizo zilimhusuje Sumaye, mtu ambaye hajipangii safari wala kujipangia kiasi cha pesa zinazopaswa kutumika au kujilipa posho? Si Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, iliyokuwa chini ya Kikwete, ndiyo ilimpangia safari hiyo? Si ndiyo inayoratibu ziara za wakubwa na wote wenye pasipoti za kidiplomasia? Je, ndiyo ilivujisha habari kwa vyombo vya habari ili kummaliza Sumaye?

Niliwahi kuandika na kuhoji wakati fulani: ‘Kashfa za Sumaye zina harufu ya urais?’ Wasambazaji wakuu na washinikizaji wa habari hizo kwa waandishi wanafahamika. Nasikia baadhi yao ndio hao vinara wa mtandao, ambao sasa baadhi yao wanahusishwa na miradi mibovu na minono yenye utata, ukiwamo wa Richmond.

Hofu yao sasa ni kwamba, kile walichowatendea wenzao wakati ule, kwa kuvipelekea vyombo vya habari taarifa za kashfa za wakubwa, kinaweza kutumiwa sasa na wenzao ndani au nje ya mtandao kuwamaliza walio madarakani. Wanajua kuwa mtandao ulishagawanyika; hawaaminiani tena. Wanajua pia kwamba majeruhi wa mtandao ndani ya CCM ni wengi, na wanajua kilichofanyika dhidi yao, na labda wangependa kulipiza kisasi cha njia ile ile kujaribu bahati tena, au kuwapitisha watu wao.

Kwa kujua mazingira haya, ndiyo maana baadhi ya watu wanasema serikali ya sasa inajitahidi kuvifuga vyombo vya habari kwa sababu inaviogopa. Inataka iviongoze viandike nini, viache nini, vimwandame nani na vimkwepe nani.

Ndiyo maana tumeshuhudia baadhi ya watu wasio wanamtandao, ambao baadhi yao wamo serikalini (yawezekana na John Magufuli anaangukia katika kundi hili), wamechimbwa mno na kuanikwa hadharani kwa staili le ile iliyommaliza Sumaye. La Magufuli linahitaji makala inayojitegemea.

Watanzania hawajasahau yaliyowatokea washindani wa Kikwete, kama walivyoorodheshwa na Absalom Kibanda, katika moja ya makala zake kwenye safu ya TUENDAKO. Aliwataja wengi kwa majina, kwamba mbali na Sumaye, wamo kina John Malecela, Iddi Simba, Dk. Salim Ahmed Salim, Prof. Mark Mwandosya, Dk. Gharib Bilali na Pius Msekwa.

Waliguswa na kuumizwa mmoja mmoja, kwa hoja za kweli na za kutungwa, zilizosambazwa na watu wale wale kutoka kwa vyanzo mbalimbali na kurushwa katika vyombo vya habari. ‘Waathirika’ hawa walichelewa kujua maumivu yao yanatoka wapi; na hata walipojua, hawakuwa na mbinu za kuwapiku wanamtandao.

Silaha moja ambayo wanamtandao walimiliki, ambayo washindani wao hawakuwa nayo ni ‘urafiki na vyombo vya habari.’ Wanamtandao walikuwa karibu na waandishi, hasa wahariri, ambao ndio waamuzi wakuu wa habari zinazoandikwa, zinazotangazwa na zinazoachwa.

Udhaifu mkubwa wa washindani wao ni ‘kuwa mbali na waandishi,’ na kwa kuona wanashambuliwa, wakajenga ukuta dhidi ya waandishi wa habari. Ukuta huu ulizaa mazingira ya chuki na woga miongoni mwa waandishi na watu hawa. Habari zao chafu zikavuja na kutumika kirahisi; huku habari mbaya za wanamtandao zikimezwa na urafiki na kuoneana aibu.

Sikumbuki idadi ya waandishi walioalikwa kwenye safari za kikazi (kwenda popote) na kina Sumaye, Simba, Malecela, Dk. Bilali, Mwandosya na Dk. Salim tangu mwaka 1995. Sikumbuki kuambiwa na mtu yeyote au kuona kundi hili likiwaalika waandishi kwa mazungumzo ya kawaida ya kufurahia jambo mbele ya ‘kikombe cha chai au bia.’ Lakini nazikumbuka safari nyingi (na mialiko ya kawaida) za waandishi wakiambatana na wanamtandao, wakiwamo Kikwete mwenyewe, na Edward Lowassa, hasa alipokuwa Waziri wa Maji.

Kina Kikwete walifungua mlango kwa wanahabari, kina Sumaye hawakuwapa nafasi hiyo, ama kwa kuwaogopa, au kwa kuheshimu maadili ya taaluma yao, wakawaacha wafanye kazi objectively. Kina Kikwete walijifanya ‘watu wa watu,’ washindani wao wakawa watu wasiojichanganya na watu wadogo. Kina Kikwete na Lowassa walifichua baadhi ya makucha yao kwa rafiki zao (wanahabari); kina Sumaye, kwa kuzingatia utamaduni wa CCM wa kushtukizana, wakawa na mitandao ya chini chini ndani ya chama na serikali, lakini hawakuwa na kiunganishi kwa wananchi.

Sumaye, kwa mfano, licha ya kuwa msiri kuhusu azma yake, na kuwa mbali na wanahabari waliokuwa tayari wametekwa na kundi la Kikwete, alichangia kusimika udhaifu wake kwa wananchi kwa sababu ya kukaa kimya bila kujibu mapigo ila alipoandikwa magazetini.

Alijitetea kwa hoja nzito mbele yao siku alipochukua fomu kugombea urais, katika Ukumbi wa NEC, Dodoma; na akahitimisha kwa kuonya kwamba mtu anayewachafua ili kujisafishia njia kwa kutumia kalamu (akimaanisha Kikwete) atajisafishia njia kwa kutumia risasi akiwa madarakani.

Hatuwezi kusahau kauli hii ya Sumaye. Na itatusaidia kupima mwenendo na reaction ya Kikwete kwa wakosoaji wake kadiri siku zinavyoendelea na anavyozidi kunogewa na madaraka.

Kikwete na wenzake, hasa Lowassa, wanajua uzembe alioufanya Sumaye kwa kukaa kimya kila kashfa zake zilipoibuliwa. Ndiyo maana kila wakiguswa kidogo wanakimbilia kukanusha au kulazimisha yafanyike masahihisho kwenye vyombo vya habari, hata ikibidi wanunue nafasi na wailipie kwa gharama ya kodi za wananchi.

Na sasa wanadhani kila kinachoandikwa au kutangazwa kwenye vyombo vya habari, kina msukumo kutoka nje ya vyombo vya habari. Kwa kuwa waliwatumia waandishi kwa kuwaletea ‘mabomu ya kulipua,’ sasa hawawaamini hata wakiibua suala lolote zito dhidi ya serikali au kiongozi yeyote. Dalili zimeanza kujionyesha kwamba, fikra zao zinarudi kule kule walikotoka wao, kwamba waandishi hawa wametumwa, na wanatumiwa na washindani wao.

Wanakumbuka kwamba, sumu waliyoimwaga kwa Sumaye ilimwandama, hata alipojitokeza kugombea urais ndani ya CCM, akapokewa kwa hisia zilizopandikizwa na wanamtandao miongoni mwa wananchi kuhusu ‘uchafu’ wake.

Baadhi ya watu walidiriki kuhoji ‘hata Sumaye anataka urais?’ Tayari walikuwa wameshiba ‘mabaya’ yake, na walikuwa na mtu wao vichwani. Lakini aliingiaje vichwani mwao? Alijengwa. Na je, hawa waliojengwa dhidi ya wachafu hao, ni wasafi kuliko nani?

Itaendelea Jumapili ijayo.

Kiselula: +447828696142
Baruapepe: ansbertn@yahoo.com
blogu: http://ngurumo.blogspot.com

No comments: