Tuesday, April 03, 2007

Heri Kulamba Miguu ya Kikwete Kuliko ya Mabeberu


By Salehe Mmoro

Mwanahabari wa HabariTanzania.com, Dar-es-salaam

Habari ilichapishwa kwenye Habari Tanzania, Oktoba 2006.

JUMAPILI, Oktoba Mosi mwaka huu, Gazeti la Sunday Nation la Kenya liliwakejeli waandishi wa habari wa Tanzania kwamba walikuwa wakikalia ‘kumlamba miguu’ Rais Jakaya Kikwete, na kukariri kila akisemacho, kama kasuku!

Kejeli hiyo kupitia katuni iliyochapwa ukurasa wa nane wa gazeti hilo, iliwaonyesha Waandishi wa TZ ( Tanzania) waliokuwa wakishangilia, na wengine wakiwa wamemsujudia Kikwete, huku wakimlamba miguu, kuonyesha kuwa waandishi wa nchi hii ni mbumbumbu wasioweza kufanya tafakuri tunduizi dhidi ya kauli za watawala, isipokuwa, kufagilia tu!

Naam, licha ya kumsujudia Kikwete, kumlamba miguu na kushangilia kila alichokuwa akisema, katuni hiyo ya mwaka, iliwaonyesha baadhi yao wakionyesha unyenyekevu kwa rais aliyeketi katika kiti cha enzi, huku akiwa kavalia kanzu, suruali na ‘mabuti’.

Japo ni ujumbe uliotumwa kwa njia ya kejeli kupitia katuni, lakini maudhui ya katuni hiyo yamebeba ukweli uliotiwa chumvi nyingi, dhana iliyowahi kupingwa na hata Yesu wa Nazareti; ya kutoa kibanzi jichoni mwa mwenzako, wakati kwako kuna boriti.

Ukweli mwanana uliomo katika katuni hiyo ni juu ya vyombo vya habari kuacha wajibu wa kuutumikia umma, na kugeuka kasuku; ili kuwasifia watawala.

Tatizo hili halipo Tanzania peke yake, limeota mizizi tangu Kenya, ambako hadi majuzi tu, kila sentensi katika kila Taarifa ya Habari ya Sauti ya Kenya (VOK) na baadaye KBC, ilikuwa ikianza na “Mtukufu!!”Binadamu atakuwaje mtukufu, kama si kulamba dole gumba la watawala? Mtukufu ni Mungu ambaye wengine hudai hayupo.

Mtukufu Rais husika alikuwa akiimbwa kwa takriban asilimia 80 ya muda wa taarifa ya habari, wakati habari zinazohusu maendeleo ya watu, kero zao na hata habari za wanaharakati wa Haki za Binadamu na zile za wapinzani ,zikibezwa!

Sijafahamu; kama habari hizo za kumwita mwanadamu mmoja, “Mtukufu !” kama Mungu, zilikuwa zikikusanywa, zikiandikwa na kuhaririwa na kina nani, kama si waandishi wa habari wa Kenya?

‘Mtukufu, Baba Moi’ alikuwa akiimbwa redioni tangu alfajiri KBC ilipokuwa ikifunguliwa hadi wakati wa kufungwa usiku wa manane.

Haki za wananchi kuzungumza kupitia vyombo huru vya habari, haukuwepo. Badala yake jamii isiyo huru ilikuwa ikichaguliwa wimbo gani waimbe; bila shaka kusifia harakati za serikali ya NYAYO katika kuwaletea watu wake Demokrasia na Maendeleo!

Si Kenya tu. Hata waandishi wa Marekani ambako kunadaiwa Demokrasia imekomaa, na vyombo vya habari viko huru hata kuandika habari za Hugo Chavez kumtukana Bush shetani, vimekuwa vikisambaza pumba na propaganda kwamba Iraq ilikuwa na silaha za maangamizi.

Waandishi wa habari wa Marekani waliokuwa wakiandamana na majeshi ya nchi hiyo Iraq na Afghanistan, hawakuacha kuandika habari za uongo, za upande mmoja, kwamba majeshi ya Washirika yalikuwa yakisonga mbele kwa kasi, huku yakishangiliwa, hata kama walikuwa wakipigwa na maiti za askari wao kuburuzwa mabarabarani na wenyeji.

Hata leo, vyombo vya habari vya Magharibi haviachi kumsifia Bush na Tony Blair na mikakati yao ya kutaka kuzivamia Korea Kaskazini, Iran na Syria, kwa sababu zozote za uongo. Wala hawajakoma kuudanganya umma kwamba Bush anapendwa ulimwengu mzima, wakati Chavez akimtukana Ibilisi, katika mkutano wa mataifa yote, mjini New York! Vipi kuhusu kipigo cha Israeli dhidi ya Hizibollah? Wanasema nani shetani, kati ya Israeli na Lebanon…ni politiki tu.

Kwa kusema hivi, sipendi kutetea uandishi wa upande mmoja; wala sipendi kuunga mkono ‘ukasuku’ wa vyombo vya habari vya ulimwengu mzima, ikiwemo Tanzania.

Ningeridhika, kama gazeti la Nation lingetoa mada kuhusu waandishi wote wa habari wa nchi zetu hizi, ili wafuate maadili ya uandishi na kukosoa watawala wanapokwenda kinyume cha matakwa ya watu.

Ni kichekesho magazeti ya Uingereza kumkosoa Robert Mugabe wa Zimbabwe, kwa kunyang’anya mashamba ya Wazungu na kuwapa Waafrika, wakati waki ‘mfagilia’ Tony Blair kushirikiana na Bush kutesa watu na kuwafunga jela bila kuwafikisha mahakamani huko Guantanamo Bay, Abu-Ghraib na jela za siri Ulaya! Wakati huo huo wakibomoa makazi ya mamilioni ya watu kwa mabomu Iraq, Afghanistan na Lebanon…na sasa wanatishia kwenda Syria, Iran na Korea Kaskazini.

Huku ni kutetea haki za binadamu wapi? Au ndio kama walivyosema wahenga, “nyani haoni nonino?” Tazama CNN, BBC, ABC,CBS,NBC au hata SKY NEWS, n.k. hutakosa kuona habari hasi kuhusu Bara la Afrika na Waafrika…makamasi, mapanki, ukimwi, njaa, vita na kila uchafu!

Hii ni kuonyesha kuwa si lazima sana vyombo vya habari vya kizalendo kupiga kelele nyingi zinazoweza kuivunjia hadhi nchi hiyo miongoni mwa mataifa. Vitakosoa watawala kwa namna ambayo haileti migogoro ya kisiasa inayosababisha “kelele nyingi” hadi masikioni mwa akina Bush, Marekani kiasi cha kutilia shaka ‘Political stability’ katika nchi hizo!

Ulimwengu haujasahau Desemba 30; dakika chache rais Mwai Kibaki wa Kenya akikaribia kuapishwa kuwa rais wa tatu wa Kenya. Katika uwanja wa Uhuru Park, Mtangazaji maarufu wa nchi hiyo (simtaji) ali ‘katwa mtama’ na wananchi waliokuwa wakimshangilia kwa nguvu rais Mpya, wakampokonya chombo cha kutangazia!

Sababu za Mtangazaji huyo wa siku nyingi VOK na KBC kupigwa mtama na wananchi, ni kutangaza habari za kujikomba sana kwa utawala uliopita, na kuwabeza wapinzani, ambao muda mfupi tu waliapishwa kuchukua dola. Hao ni waandishi wa Kenya.
Enzi ya Nyayo wasingethubutu kuwabeza ndugu zao wa Tanzania kuwa wanawafagilia watawala. Vipo vyombo vya habari katika nchi zote vinavyofanya kazi bila upendeleo, wala kujikomba.

Hapa nchini, Kikwete amekosolewa sana; hata sasa Mama Salma anakosolewa kwa kwenda kuhudhuria sherehe za Kimila huko Swaziland, ambako kila mwaka Mfalme Mswati II huchagua kigoli na kuoa.

Wala hatuhitaji kupiga kelele sana hadi akina Bush wasikie huko Washington hadi wafadhili wafikiri tutatoana ngeu! Kenya, katika Uchaguzi mkuu uliopita, watazamaji wa uchaguzi wakiwemo wa Umoja wa Ulaya (EU) walisema KBC ilikipendelea chama cha Kanu, hususan mgombea wake, Uhuru Kenyatta, kwa asilimia kati ya 32 na 33; wakati wapinzani hususan Narc wakitangazwa kwa asilimia 25 tu katika televisheni ya KBC.

KTN walimtangaza Kibaki kwa asilimia 45, Kanu wakatangazwa kwa asilimia38. Televisheni ya Nation ilimpa Kibaki ‘coverage’ ya asilimia 44, wakati Uhuru Kenyatta na Moi walitangazwa kwa asilimia 34 tu. Je, kuipinga serikali iliyoko madarakani na kuwapendelea wapinzani kwa jinsi hiyo, ndio kulinda maadili ya uandishi? Sio kuwa bias?

Wapi impatiality?
Umoja wa Ulaya walisema,ingawa Tume ya Uchaguzi ya Kenya ilitoa mwaongozo kwa vyombo vya habari, vyombo vya habari vya Kenya, likiwemo gazeti la Nation, walishindwa kuwapa wapiga kura habari sahihi.

Kwa upande mwingine vyombo vya habari vya Kenya, vilikuwepo wakati wa Utawala wa Moi. Lakini vilishindwa kufichua vyumba vya vya siri vya mateso dhidi ya wapinzani wa Kanu, katika jengo la makao Makuu, ya Kanu, Jogoo House, hadi utawala mpya wa Narc ulipoingia madarakani.

Vilishindwa kusema ukweli juu ya watu waliokufa katika mazingira ya kutatanisha enzi za Nyayo. Hawa ni pamoja na Dk. Robert Ouko, na mpiga picha wa Kiingereza, Julie Ward (28) aliyeuawa katika mbuga za wanyama za Masai Mara. Mauaji ya Julie yaliifanya serikali ya Kenya kuwa lawamani, kufuatia Uingereza kuwatuma Scotland Yard kupeleleza chanzo cha mauaji hayo, kufuatia serikali kusema aliuawa na wanyama wakali!

Kwanini Scotland Yard walikuja kufanya upelelezi wa mauaji ya msichana huyo Kenya, wakati wapo polisi wa nchi hiyo? Rushwa? Kwa nini vyombo vya habari vya nchi hiyo vimeacha nchi kufika huko, kama vyatenda kazi yao barabara?

Vyombo vya habari vya Kenya havikusema muuaji, hadi utawala wa Kibaki ulipoingia madarakani ndipo wakaanza kuandika haja ya kuchunguza vifo vya akina Julie, Dk. Ouko, J.M. Kariuki, Pio Gama Pinto, Tom Mboya na wengine ambao vifo vyao vilikuwa utata mtupu. Je, huu ni Uungwana?!

Na kwanini mahali ambapo vyombo vya habari haviwalambi miguu watawala, kuwe na mauaji ya siri na mawingu ya mashaka , jinsi mfumo mzima unavyofanya kazi… hadi waje Scotland Yard?

Nation waliandika nini kuhusu kifo cha Julie Ward?Waliikosoa serikali kwa asilimia mgapi?

Moi aliiongoza Kenya kwa miaka 24, tangu kifo cha mwasisi wa Taifa hilo, Jomo Kenyatta, 1978.Lakini hadi Kibaki alipoingia madarakani 2002 ndipo ‘siri’ za mauaji ya akina Dk.Ouko ya Feburuari 1990 na siri ya vita vya kikabila vya miaka ya 90 zikaanza kuvuja.

Nation walikuwepo Kenya, walifanya nini badala ya ‘kuulamba miguu’ utawala wa Moi? Kuhusu kashfa za Goldenberg na Anglo Leasing; vyombo vya habari vya Kenya havipaswi kujitazama kuwa viko juu katika kufichua ‘skandali’.Kinachoufikia umma wa Kimataifa, wakiwemo akina George W. Bush, ni fujo na makelele, kana kwamba nchi hiyo haina ‘political stability?’

Mtindo unaotumiwa na waandishi wa habari wa nchi hiyo, na ambao wanataka waandishi wa Tanzania wauige, ni kushambuliana kila kukicha. Vyombo hivyo na waandishi wake hawajapona majeraha ya kikabila, kimajimbo na hata kidini. Bila shaka waandishi wa kabila fulani huwatetea wanasiasa wa kabila lao hata kama wanaleta mgawanyiko.

Waandishi wa itikadi fulani hudumu kuipinga serikali hata kama haijafanya makosa, mradi tu watu wao washinde uchaguzi. Huu si uhuru wa vyombo vya habari wala kufuata maadili; bali fujo tu zinazo dunda kwa fujo masikioni mwa akina Bush, Washington.

Kuhusu udini, katuni ya Nation imekosa hoja kutaka kuwaambia Watanzania waliokwisha sahahu ukabila na udini, kwamba Kikwete aliyekalia kiti cha enzi ni Muumini wa Madhehebu fulani, ambao hutambulishwa kwa vazi la kanzu!

Kikwete, awe Muislamu, Mkristo, Budha, Baniani, Mpagani au hata asiye na dini yoyote, Watanzania hawajali!

Nijadili kidogo waandishi wa nchi hii kumfagilia Kikwete. Kama udhaifu huu upo hapa Tanzania kama Kenya na Marekani, si wajibu wa waandishi wa Kenya kutufundisha maadili ya kazi. Zaidi sana kila nchi ina maadili yake ambayo hata vyombo vya habari huyafuata.

Kwanza Watanzania hawajazoea fujo; hawajawahi kupigana; wa kabila moja dhidi ya lingine kiasi cha kuathiri nyanja mbalimbali hadi kuanza kushambuliana kwa ukali na kuzua mtafaruku.

Tatizo la vyombo vyetu vya habari kumfagilia Kikwete halina tofauti na vyombo vya Magharibi kutoona uvunjaji wa Haki za Binadamu wa Marekani na washirika wake Iraq na Afghanistan, na badala yake kukalia kumlaani Osama bin Laden, Wataleban, Magaidi, Mullah Muhammad Omar na wengineo wanaopinga ubeberu kwa staili ya kujitoa mhanga.

Pengine, kuipinga serikali iliyoko madarakani na kuwaunga mkono wapinzani bila kujiondoa katika upendeleo wa upande mmoja, si kipimo sahihi cha utendaji kazi au kutimiza wajibu.

Nani asiyejua kuwa kelele za vyombo vya habari vya nchi hiyo juu ya harakati za wanasiasa wa nchi hiyo kupendelea ukabila na migawanyiko ndizo zinazoifanya Kenya kuonekana haijatulia?

Katika nchi ambayo vyombo vya habari hufanya kazi vizuri hakuna rushwa ya kutikisa kama Goldenberg na Anglo Leasing; na wananchi wananeemeka kwa amani inayowaletea uchumi mzuri, potelea mbali utulivu usiwepo.

Ubora wa vyombo vya habari haupimwi kwa picha nzuri za televisheni na magazeti, na mbwembwe za watangazaji wa redio,bali hupimwa kwa amani na ustawi walionao wananchi au jamii inayotumikiwa na vyombo hivyo.

Kipimo cha uandishi bora hakiji kupitia mashambulizi yasiyo na sababu dhidi ya serikali, bali kuutafuta ukweli mkamilifu, bila mashaka, wala shinikizo la wanasiasa wa upande fulani kwa maslahi yao…uandishi bora uliotukuka huwatumikia wananchi wanyonge, makabwela; wala siyo wanasiasa wa upinzani tu.

Bob Woodward na Carl Bernstein au kama walivyokuja kujulikana, “ The Woodstein” ni waandishi wa gazeti la Washington Post, waliofichua kashfa ya Watergate, iliyomfanya Rais Richard Milhouse Nixon kujiuzulu Agosti mwaka 1974.

Waandishi hao wa kitabu maarufu cha All The President’s Men, waliweka bayana matumizi ya fedha haramu kwa maharamia waliovunja makao makuu ya kampeni ya chama cha Democrat, (wapinzani wa Nixon), yaliyoitwa Watergate.

Nixon alikabiliwa na mashitaka ya uhaini kutoka Baraza la Congress, baada ya waandishi hao kulipua skandali la Watergate.Akajiuzulu, na makamu wake wa Rais Gerald Ford, akachukua mahali pake. Ushahidi ulikuwepo, na ungeweza kutolewa mahakamani dhidi yake.

Naam, kuandika habari nzito hakujitengi na ushahidi wa dhati; na wala siyo dhana na kusingizia kusikowanusuru waandishi na mashitaka,kama waandishi wa Kenya wanavyotaka tuanze kumfanyia rais wetu!

Hatuna ugomvi mkubwa na serikali ya Kikwete. Wala Mama Salma hajawahi kuvamia chombo chochote cha habari na kuwapiga bakora waandishi, kubomoa makompyuta na kutupa magazeti.

Kwa kusema hivyo, hatuna maana kuwa tunamlamba miguu au kutowajibika kwa umma, kulingana na wajibu na maadili na uhuru wa vyombo vya habari. Umma wa Tanzania unawajibika kuwa mashahidi, na wala si waandishi wa Kenya.

Tunatambua kuwa serikali na vyombo vya habari ni maadui wa tangu enzi, lakini wenye majukumu tofauti, lakini kila mmoja apaswa kumheshimu mwenzake na majukumu yake.

Kwa misingi hii waandishi wa Tanzania hawaachi kuiheshimu serikali yao hata kama watafichua uoza, rushwa na kutowajibika dhidi yake. Kuheshimu si kulamba miguu. Na kusababisha vita si kufuata maadili yoyote. Ni ushenzi, uchochezi na unyama mkubwa.

Tunakiri; vipo vyombo vya habari au mwandishi mmoja-mmoja waliojibatiza ukasuku. Lakini si wote. Hata Kenya na Marekani wapo kama tulivyoona, wala hatuhitaji nyapara toka Kenya kuwapigia kelele! Sisi wenyewe twatosha.

Nani aliwachagua waandishi wa Kenya kuwa nyapara na walimu wetu? Wanalipwa na nani kwa kazi hiyo? Kwa kujitia mafundi, wanaipa nguvu serikali yao au ugoigoi? Wanapata faida gani kwa kuidhoofisha serikali ya Narc, ili ODM iingie madaearani?

Tunaingia katika Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC) tunahitaji upendo na utulivu kwa nchi zetu na si chokochoko na uchochezi toka upande mmoja. Ule umoja uliokuwepo ulivunjika kwa sababu za ubinafsi toka hukohuko; na sasa dalili zimeanza kuonekana hata kabla ya wakati!

Tunarudia, tunathamini maoni ya kila mtu, yakiwemo ya waandishi wa Kenya, lakini kamwe si kudhalilishwa na mtu kwa sababu tu ya kusigana kwa mawazo na mtindo wa kuendesha mambo yetu.

Biblia inasema, “u-mimi” ni chanzo cha vita, bali tunda la roho ni upendo, utu wema, upole, uvumilivu na tafakuri tunduizi isiyo na vita na kuwapenda maadui hata kuwashangilia kwa mema wanayofanya. Wala hatuhitaji nyapara toka Kenya kwa hili la upendo, umoja, amani na utulivu.`

Baruapepe: omybabu@yahoo.com

Chanzo cha habari, HabariTanzania, Jumanne 03.04.2007:

http://www.habaritanzania.com/articles/1231/1/
Heri-Kulamba-Miguu-ya-Kikwete-Kuliko-ya-Mabeberu


No comments: