Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Amina, alisema anamuomba Mwenyezi Mungu amuamshe salama, ili aweze kuzungumzia suala hilo ambalo anafahamu kuwa linaweza kumuweka katika wakati mgumu kabisa. “Nafahamu ninapambana na watu hatari, lakini kesho (leo) namuomba Mwenyezi Mungu aniamshe salama, ili niweze kuliweka bayana suala hili mbele ya waandishi wa habari MAELEZO. Nimekusudia kusema ukweli wote kuhusu suala langu,” alisema Amina.
“Daima nasimamia ukweli na sababu ya dhamira yangu. Nipo tayari kufungwa au kuchukuliwa hatua yoyote iwapo nitaonekana sina nidhamu… hata ikibidi kupoteza ubunge na uanachama wangu wa CCM. Mimi si mwanasiasa wa ‘ndiyo mzee’,” alisema Amina baada ya kuulizwa iwapo ukweli anaotaka kusema hautamgharimu.
Amina ambaye ameihakikishia Tanzania Daima kuwa alipewa talaka na mumewe, Mei 3 mwaka huu, anasema tukio hilo lilikuja baada ya kiongozi huyo wa CCM ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho kumuita mumewe ofisini kwake. “Nilipewa talaka siku ile ile baada ya Mpakanjia kutoka ofisini kwa kiongozi huyo. Kwa kweli (anamtaja) ndiye aliyevunja ndoa yangu kwa kumuambia mume wangu mambo ya uongo,” alisema.
Habari zaidi ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kwamba, Amina anaamini kwamba kikubwa kilichosababisha akutwe na masahibu hayo, ni kile kinachoelezwa kuwa uamuzi wake wa kutaka kugombea uenyekiti wa taifa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), hatua ambayo inaonekana kuwashtua na kuwakera baadhi ya viongozi wa sasa wa umoja huo. Hivi sasa Mwenyekiti wa UVCCM ni Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana anayetarajiwa kumaliza kipindi chake mwakani.
Hata hivyo, Amina alipotakiwa kueleza iwapo alikuwa akikusudia kugombea nafasi hiyo, hakuwa tayari kusema lolote zaidi ya kumtaka mwandishi kusubiri hadi wakati utakapofika kwani kuna muda mrefu bado, kabla ya yeye kufikia uamuzi huo. Mbali ya hilo, Amina alielezwa kushangazwa kwake kuona masuala yake ya ndoa, yakipelekwa bungeni, wakati mahusiano yake ya nyumbani hayana uhusiano wowote na ubunge wake au uanasiasa wake.
Habari ambazo zilithibitishwa zinaonyesha kuwa, Amina amekuwa akihusishwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mbunge kijana wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ambaye alipopigiwa simu na gazeti hili jana, aliyapuuza madai hayo ambayo alisema; “hayana ukweli.”
Zitto mmoja wa wabunge machachari wa upinzani, alisema anafahamu kwamba suala hilo limeandaliwa na kundi la watu wenye sababu za kisiasa, ambao wamekuwa wakimtafuta yeye na Chifupa kwa muda mrefu.
“Ukaribu wangu na Amina ni wa kikazi tu… na ukaribu huo ulianza siku Spika wa Bunge alipotuteua tuhesabu kura za wabunge zilizomuidhinisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa. “Siku hiyo tulipokuwa tukihesabu kura, afisa mmoja wa bunge alitufuata katika chumba cha kuhesabu kura na akatutaka kutozitaja kura mbili zilizokuwa zimeharibika, jambo ambalo mimi na Amina tulilikataa. Tangu hapo nilianza kumheshimu Chifupa baada ya kubaini kuwa alikuwa mtu makini na mwenye msimamo. Tangu wakati huo tumekuwa na uhusiano wa karibu kikazi,” alisema Zitto, alipohojiwa kwa njia ya simu. Alisema, siku zote amekuwa na uhusiano mzuri na wabunge wote vijana kwa wazee, lakini anashangazwa na uvumi juu ya uhusiano wake na Amina kuonekana vinginevyo.
Gazeti moja la kila siku, (si Tanzania Daima), jana lilimkariri Mpakanjia, akithibitisha kumtaliki mkewe baada ya kubaini ndoa yake ikiingiliwa na mbunge wa CHADEMA ambaye hata hivyo hakumtaja. Habari zaidi ambazo gazeti hili linazo zinaeleza kwamba, ushahidi mkubwa unaoonekana kuwaunganisha kimapenzi wabunge hao vijana, ni tukio la siku moja jioni, ambalo Amina alionekana akiwa amevaa koti la Zitto, wakiwa wameketi pamoja katika Hoteli ya Dodoma.
Chanzo cha habari: Gazeti la Tanzania Daima mtandaoni, Jumatatu 07.05.2007.
Imepostiwa na Pwagu na Pwaguzi: pwagu.na.pwaguzi@oslo.online.no
No comments:
Post a Comment