Tuesday, May 08, 2007

Amina Chifupa akwama

na Tamali Vullu

AZIMA ya Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Chifupa (CCM), kulipua bomu kwa kumtaja kiongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anayedai kuivuruga ndoa yake imekwama.
Chifupa, mbunge kijana ambaye juzi, alilihakikishia gazeti hili kwamba, angefichua siri hiyo mbele ya mkutano wa waandishi wa habari, alishindwa kufanya hivyo na badala yake akawakilishwa na baba yake mzazi, mwanasiasa mstaafu, Hamisi Chifupa.
Katika hali ambayo mzee Chifupa alishindwa kuifafanua, alisema walifikia uamuzi wa kumzuia binti yake kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kubaini kuwa, masuala yake yangeweza kumalizwa ama ndani ya familia au katika vikao rasmi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi waliokuwa wamefurika katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) kumsubiri mwanasiasa huyo kijana ambaye tangu aingie bungeni amekuwa akivuta hisia za wengi kisiasa, alisema:
“Nimekuja hapa kwa niaba ya Mheshimiwa Amina, kuwaomba radhi kwamba familia imesitisha mkutano na waandishi wa habari… ni kweli amepewa talaka moja.
“Sisi ndio wenye jukumu na mtoto wetu. Watoto ni pensheni zetu sisi wazee, hatutaki kuharibu. Tutashughulikia kichama. Kulinda pensheni ni muhimu,” alisema mzee Chifupa.
Pia alisema iwapo Amina anahitaji kuzungumzia suala hilo, atapaswa kufanya hivyo ndani ya vikao vya vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na si kuzungumza mbele ya umma.
Mzee Chifupa alieleza hayo alipoulizwa iwapo kusitisha mkutano huo ni kumnyima Amina uhuru wake wa kujieleza katika masuala yanayomhusu, hasa ikizingatiwa ni mbunge aliyetokana na vijana.
Mzee huyo aliyepata kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM, aliwachekesha waandishi wa habari alipozungumzia kufurahishwa kwake na habari ya serikali kuteketeza taa za umeme aina ya ‘tube light’ ambazo zimebainika kuwa ni feki za Kampuni ya Philips na uingizwaji wa mchele mbovu nchini, akijaribu kulimaliza suala la mwanawe.
Gazeti hili jana lilimkariri Amina akisema kuwa alikuwa akikusudia kusema ukweli wote kuhusu matatizo yake ya kifamilia ambayo yanahusishwa na dhamira yake ya kutaka kuwania nafasi ya uenyekiti wa vijana wa CCM Taifa, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Emmanuel Nchimbi, atakayemaliza muda wake mwakani.
Amina aliahidi kuwa katika mkutano wake wa jana angemtaja kiongozi huyo wa CCM ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho, aliyesema ndiye aliyevunja ndoa yake, baada ya kumweleza mumewe mambo yasiyo na ukweli.

Imepostiwa na Pwagu na Pwaguzi: pwagu.na.pwaguzi@oslo.online.no

Chanzo cha habari: Tanzania Daima mtandaoni, Jumanne 08.05.2007



No comments: