Picha kutoka http://www.kikweteshein.com/
kwa kumtetea Chitalilo!
na Mwandishi Wetu
VYAMA viwili vya upinzani vimeeleza kushangazwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete inayotoa mwelekeo wa kumtetea Mbunge wa Buchosa, Samwel Chitalilo (CCM), anayekabiliwa na kesi ya jinai ya kudanganya kuhusu elimu yake wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Kikubwa kinachoonekana kuvigusa vyama hivyo viwili ni kauli aliyoitoa Rais Kikwete juzi wakati akiwa katika ziara yake wilayani Sengerema.
Kikwete katika kauli yake hiyo, aliyafananisha malalamiko ya baadhi ya wapiga kura wa Buchosa dhidi ya mbunge wao kuwa sawa na kelele za mlango ambazo, aghalabu hazina uwezo wa kumzuia mwenye nyumba kulala. Viongozi wa kwanza kupinga kauli hiyo ya Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Mwanza, Ibrahim Lyimo na Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbaralah Maharagande. Viongozi hao walisema kuwa, hatua ya Rais Kikwete kumkingia kifua mbunge huyo ni kudumaza taaluma ya Watanzania na kupotosha suala zima la elimu inayotolewa nchini kwa mataifa mengine ya nje.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Mwanza jana, Lyimo aliielezea hatua hiyo ya Rais kuwa inapunguza nguvu na bidii ya kujituma katika masomo kwa baadhi ya wanafunzi walioko katika vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi. “Basi kama ni hivyo, kutakuwa hakuna umuhimu wa wanafunzi kuhudhuria darasani, ili mradi kuna kompyuta ambayo inaweza kutengeneza cheti, na muhuri na sahihi ya kughushi kwa shule au chuo husika na mhitimu kuanza kazi hata kama hajasoma,” alisema Lyimo.
Lyimo alisema kauli hiyo ya juzi ya Kikwete, imeipunguza kama si kuimaliza nguvu azima iliyotangazwa na serikali hivi karibuni ya kuwasaka wale wote wanaotumia vyeti bandia. Kwa upande mwingine, Maharagande alisema chama chake (CUF) kimehuzunishwa na kauli ya Rais Kikwete kwani imeonyesha dharau kwa kazi iliyofanywa na taasisi nyingine za serikali kuhusiana na jambo hilo. Alisema uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi nchini ilithibitisha kuwa Chitalilo aliwadanganya wapiga kura wa Buchosa kuhusu elimu yake, hatua ambayo hivi karibuni ilisababisha baadhi ya wananchi wa huko kwenda mahakamani kufungua kesi dhidi ya mbunge huyo.
“Inashangaza kumsikia rais akitoa kauli ambazo zinapingana na Jeshi lake la Polisi. CUF tunamtaka aache kumlinda Chitalilo, angeiachia mahakama itoe uamuzi,” alisema Maharagande katika taarifa yake ya maandishi kwa vyombo vya habari.
Akiwa katika ziara yake hiyo wilayani Sengerema, Rais Kikwete alisikika akiwaambia wananchi wa jimbo hilo katika Kijiji cha Nyakalilo kuwa wapinzani wamekuwa wakimpigia kelele Chitalilo kwa madai ya kughushi vyeti. Rais Kikwete anakuwa kiongozi wa kwanza wa juu serikalini na kutoka CCM kujitokeza hadharani kumtetea Chitalilo, hatua ambayo inaweza ikafungua utata mkubwa. Kwa upande mmoja, watu kadhaa waliowasiliana na gazeti hili jana, walikielezea kitendo hicho cha Rais kuwa kililenga zaidi kulinda masilahi ya CCM zaidi, badala ya kulinda na kuheshimu haja ya lazima ya wagombea uongozi kuwa wa kweli.
Spika wa Bunge, Samuel Sitta, amewahi kukaririwa akisema kuwa, asingekuwa na uwezo wa kuchukua hatua zozote kwani suala hilo halijapata kufikishwa kwake rasmi.
Imepostiwa na Tausi A. Makame: tausi@online.no
Chanzo cha habari: Tanzania Daima mtandaoni, Jumanne 08.05.2007
No comments:
Post a Comment