Monday, June 04, 2007

Kicheni Pati

na Stella Nyemenohi

HabariLeo
; Friday, June 01, 2007 @00:02

“Kicheni pati” ni maneno ambayo nalazimika kuyatohoa kutoka katika maneno ‘kitchen party’. Ili kutengeneza tafsiri ya moja kwa moja, maneno haya yanamaanisha ‘tafrija ya jikoni’.

Haya ni maneno ya kiingereza yanayotumika kuelezea utamaduni ulioshamiri katika maeneo mengi hususan mijini. Ukienda mitaani, sehemu za kazi (maofisini) na hata katika maduka mbalimbal dhana, hutakosa kusikia maneno haya yakitamkwa.

Katika sehemu za kazi, utashuhudia kadi zilizochapishwa kwa mitindo mbalimbali zikiwaalika wanawake kuchangia na kuhudhuria sherehe hizo.

Ukiamua kutembelea saluni katika Jiji la Dar es Salaam, hususan siku za mwisho wa wiki, hutakosa kukutana na watu wanaojiremba na kujipamba kwa lengo la kuhudhuria tafrija hiyo.

Bado katika maduka mbalimbali, hususan ya vyombo vya ndani na yale ya kuuza khanga, utashuhudia wanawake wanaofanya manunuzi kwa ajili ya kicheni pati.

Ukiingia mitaani katika siku za mwisho wa wiki, wanawake waliovalia sare za khanga au vitenge, huwa ni kitambulisho kimojawapo cha wanaokwenda kuhudhuria sherehe hizi.

Mirindimo ya muziki katika kumbi za starehe pia hutoa sura nzima ya kicheni pati. Lakini utambulisho halisi wa tafrija hii, ni sherehe hizi kuhudhuriwa na wanawake pekee.

Kama utawakuta wanaume, basi hawatazidi watatu. Nao huwa ni kwa ajili ya kuratibu vyombo vya muziki au wapiga picha. Hata hivyo katika kicheni pati nyingi, wanawake wamejizatiti kuendesha shughuli zote wenyewe.

Kwa ujumla, utamaduni huu wa kicheni pati unaelezwa katika mtazamo tofauti. Mathalan, mmiliki wa saluni moja eneo la River Side, Hasnath Masoud anaona kicheni pati ni utaratibu waliojiwekea wanawake kumwezesha bibi arusi mtarajiwa kupata vyombo vya kumsaidia katika maisha yake ya ndoa.

Ester Juma, mkazi wa Kimara Kona, anaichukulia kicheni pati kama sehemu muhimu ya kuwakutanisha wanawake kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya uhusiano wao na wanaume.

Mganga na Mtafiti wa tiba asilia, Elias Musingi, anavutiwa pia kuchangia juu ya dhana ya kicheni pati. Ingawa anakiri kwamba tafrija hizo ni kwa ajili ya wanawake, lakini anasema:

“Ingawa mimi ni mwanaume, lakini naiona kicheni pati kuwa ni mtindo mpya ambao mila na desturi za Watanzania zimeingizwa ndani ya mfumo wa kigeni na hatimaye kupotoshwa.”

Musingi mwenye ofisi zake eneo la Buguruni Malapa, anaona kwamba ingelikuwa vema kama kicheni pati ingetamkwa wazi kuwa ni sherehe za kutoa zawadi za vyombo kuliko kuziita kuwa ni za kufunda.

Anasema katika Tanzania zipo mila na desturi tofauti za makabila. Hivyo kumchukua mfundaji mwenye mila na desturi tofauti na bibi arusi mtarajiwa, na kumtaka amfunde, anaona ni sawa na usanii.

“ Matokeo yake, huyo mtu atapewa mchanganyiko wa mawazo yanayoweza kumchanganya. ” anasema na kuongeza kuwa hata kama kuna kufanana kwa mila na desturi za makabila, lakini bado baadhi ya mafundo hupingana.

Ukimuuliza Musingi, ni namna gani ameweza kufahamu yanayojiri katika sherehe hizi, anasema, “Zinafanyika kwenye kumbi na kunakuwapo vipaza sauti kiasi kwamba kila mtu anasikia. Sasa kweli hizo ndizo mila na desturi tunazotaka kuziendeleza?.”

Anakosoa zaidi kwamba, endapo sherehe hizi zinazingatia utamaduni wa Mtanzania, basi hakuna haja ya kuzifanyia kwenye kumbi na kwa vipaza sauti kiasi cha kila mtu kufahamu kinachoendelea.

Ingawa upande mmoja unapingana na dhana ya kicheni pati kwa madai kwamba haina chembe ya mila na desturi za Kitanzania, lakini upande mwingine unatetea sherehe hizi kwa nguvu zote.

Wale wanaounga mkono, wanasema kinachofanyika ni kuboresha utamaduni usiendelee kuwa wa kijima. “Muziki katika kicheni ni muhimu. Hii ni karne ya sayansi na teknolojia,” anasema mmoja wa washereheshi (MC) katika kicheni pati, maarufu kama Fat Lady.

Anasema sherehe hizi ni nzuri na muhimu kwa wasichana wanaotarijia kuanza maisha ya ndoa. Anasema ingawa kuna usasa mwingi katika kufanya shughuli hizi, lakini bado usasa huo hauondoi mantiki nzima ya kuzingatia mila na desturi za Kitanzania.

Anataja baadhi ya mambo ambayo mabibi arusi watarajiwa hufaidika katika kicheni pati, ni pamoja na kupata mawaidha na uzoefu wa maisha ya ndoa kutoka kwa wanawake walio katika eneo hilo kwa muda mrefu.

Mshereheshi huyu anasema kasoro zinazojitokeza katika sherehe hizi ni za binafsi zisizopaswa kuchukuliwa kwa ujumla wake kuwa sherehe hizi hazifai.

Hata hivyo Fat Lady ambaye jina halisi ni Rose, anaweka bayana baadhi ya mambo yanayostahili kurekebishwa ili kuifanya kicheni ikubalike na ichukuliwe kuwa ni utamaduni muhimu.

Anasema yapo masuala nyeti ambayo hayastahili kuwekwa hadharani. “Mambo mazito yasiwekwe hadharani; inabidi yatafutiwe sehemu na muda wa kumweleza bibi arusi mtarajiwa,” anasema.

Jambo lingine analokosoa ni kitendo cha kufanya sherehe hizi usiku. Anashauri utaratibu wa kufanya sherehe hizi mchana uendelezwe ili inapofika majira ya saa 12, zimalizike na kutoa nafasi kwa akina mama kurudi mapema nyumbani.

Chausiku Salim, maarufu kama Bi Chau, ni miongoni mwa wanawake maarufu jijini Dar es Salaam wanaotumika kufunda mabibi arusi watarajiwa.

Bi Chau (49) anasema karibu kila wiki lazima aitwe kwenda kutoa huduma ya ufundaji. Yeye anatoa tafsiri ya kicheni pati na kusema huu ni utaratibu mzuri unaomwandaa bibi arusi mtarajiwa kwa kumwelimisha njia bora za kuishi katika ndoa.

Lakini anasema, dhana ya kicheni pati, haina budi kugawanywa sehemu mbili. Anasema sehemu ya kwanza, ni kumfunda bibi arusi mtarajiwa katika sehemu maalum na kwa faragha. “Hii inamwezesha bibi arusi kuuliza maswali na kujibiwa juu ya mambo anayohisi hayaelewi,” anasema.

Sehemu ya pili, anaitaja kuwa ni ile ya hadharani ambayo imezoeleka kwa wengi ambapo bi arusi mtarajiwa hupelekwa ukumbini na kukabidhiwa zawadi mbalimbali hususan vyombo vya ndani.

“Kwanza nawalaumu baadhi ya ma-MC, hawajui wanalolifanya. Unakuta wanatoa maneno ya ajabu ukumbini. Kawaida mimi huwa siendi ukumbini kuanika mambo hadharani, nawafunda sehemu ya faragha,” anasisitiza Bi Chau.

Bi Chau ambaye pia ni msanii wa maigizo, anasema kicheni pati haina budi kudumu katika sehemu hizi mbili. Anasisitiza kwamba ni vema sherehe za ukumbini zibaki kuwa za kupeana zawadi na kuburudika wakati mafundo, yapewe faragha.

“Kufunda sharti kuwe sehemu ya faragha; lakini utashangaa siku hizi, utakuta kicheni pati zinatumia vipaza sauti,” anasema na kukosoa pia kitendo cha kuwapa nafasi watu ambao hawajawahi kuolewa ili watoe mawaidha.

Mwanamke huyu anaunga mkono baadhi ya sherehe hizi ambazo huendeshwa ukumbini katika misingi ya dini na kusema nyingi, hazikiuki maadili ya mila na desturi za Kitanzania.

Anatoa mfano wa baadhi ambazo huendeshwa kwa misingi ya dini ya Kikristo na kusema watoa mada hutoa maneno mazuri yasiyo na matusi ndani mwake kiasi kwamba hayawezi kuwakwaza wasiohusika hususan wanaume.

Hata hivyo Bi Chau ambaye ni mwenyeji wa Dar es Salaam, anasema mara nyingi hualikwa na watu mbalimbali bila kujali kabila. Anasema, “Mila na desturi za makabila mengi hazitofautiani sana. Hivyo hakuna tatizo kwake kumfunda mtu wa kabila lingine.”

Kwa ujumla, kicheni pati ni utamaduni unaoelezewa kwa mitazamo tofauti. Wakati wengine wanauchukulia kama unyago, bado upo upande unaoona kuwa sherehe hizi ni hazikidhi mila hizo za unyago.

Umekuwa ukionekana kuwa ni unyago ulioingizwa ndani ya mfumo wa kigeni chini ya mwavuli wa utandawazi na kutengeneza kitu kiitwacho kicheni pati. Lakini yote yanahitimishwa na Bi Chau anayesema kilichofanyika ni kuboresha kwa kuandaa sherehe lakini suala la kufunda chini ya mila na desturi liko pale pale.

Zaidi kuhusu UNYAGO bofya hapo chini:

http://findarticles.com/p/articles/mi_qa3687/is_199601/ai_n8733511/pg_4

http://findarticles.com/p/articles/mi_qa3687/is_199601/ai_n8733511/pg_5

http://findarticles.com/p/articles/mi_qa3687/is_199601/ai_n8733511/pg_6

Imetumwa na Tausi Usi Ame Makame: tausi@online.no

No comments: