Tuesday, June 05, 2007

Lugha kuendelea kuwa kielelezo cha utamaduni wa Mtanzania?

Lugha ni njia kuu ya mawasiliano na hubadilika kadiri jamii inavyobadilika. Ni sehemu ya utamaduni, ni amali ya jamii inayoizungumza na ina alama ya umoja wa kitaifa.

Lugha ni utambulisho wa jamii na kwa kutumia lugha watu hupashana habari, hujenga uhusiano kwa kufahamiana, kuelimishana na kupatana au kufarakana.

Kwa njia ya lugha, maisha ya jamii yanaakisiwa na kuifanya kuwa kioo cha jamii,bila lugha ingekuwa vigumu kuurithisha utamaduni wa kizazi kimoja hadi kingine.

Mastidia Kailembo Mbeo wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) akijadili lugha kama inaendelea kuwa kielelezo cha utamaduni wa mtanzania hivi karibuni alisema kuwa Kiswahili ni njia kuu ya mawasiliano ya wanajamii wa Tanzania.

'Ilitumika kuanzia enzi za utawala wa kikoloni hadi leo. Imekuwa ni njia muhimu ya mawasiliano baina ya watawala na watawaliwa ili kuharakisha maendeleo ya taifa.' Alisema na kuendelea.

'Kiswahili ni lugha ambayo ni kielelezo cha ndani cha jamii ya watanzania. Imekuwa ikitumika kuelezea mila na desturi ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania'

Kwa mujibu wa Mazrui na Mazrui (1995) Kiswahili ni lugha ya pwani na pia lugha ya Kibantu ambayo kwa karne nyingi imekuwa na mwingiliano mkubwa na lugha nyingi za kigeni.

Kutokana na hali hiyo nguvu za kuenea kwake zimetokana hasa na mambo makuu matatu ambayo ni biashara, utawala na dini.

Akichambua kuhusu utamaduni, Mastidia alisema kuwa utamaduni ni hali ya ustaarabu iliyofikia jamii ya watu kutokana na mafunzo au uzoefu wa kutenda kazi.

Ni hali inyaojumuisha imani, mila, mafunzo, desturi za jamii ambazo hutumika kama kitambulisho cha jamii husika zikilinganishwa au kutofautishwa na za jamii nyingine.

Utamaduni ni kielelezo cha uhai na utashi wa taifa na ni mama na baba wa sekta nyingine za jamii, siasa na uchumi.

Kwa hiyo utamaduni ni jumla ya mamabo yote yaliyobuniwa na jamii ili kukidhi utashi na maendeleo yake (sera ya utamaduni,1997), inaelezea Dhima ya utamaduni kuwa ni utambulisho wa taifa na watu wake.

Lugha ni nyenzo muhimu sana katika kuuelezea utamaduni wa Taifa kwani haiwezi kuwa utambulisho wa taifa bila kuelezea utamaduni wake.

Kwa upande wa lugha ya Kiswahili ni kielelezo cha utamaduni wetu kwa sababu huhifadhi taarifa zake kwa njia mbalimbali kama maandishi, kanda zilizorikodiwa, katika mitandao kama intaneti na tovuti ambazo hurejewa na wanajamii.

Matumizi ya Kiswahili katika shughuli za utamaduni yamechochea maendeleo ya jamii kwa namna nyingi.

Lugha ya Kiswahili hutumiwa na vikundi vya sanaa au vyama mbalimbali vya utamaduni kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa.

Mathalani, maarifa, itikadi, maadili na ufundi anuwai umekuwa ukiwasilishwa kwa kutimia lugha ya Kiswahili.

Aidha sanaa za kuchonga kama vinyago pamoja na kwamba zinahitaji kujieleza kwa kuzitazama tu, pale yanapohitajika maelezo, lugha ya Kiswahili hutumika kutolea ufafanuzi wa fikra mficho katika sanaa hizo.

Matumizi ya Kiswahili huduhirika katika nyimbo ambazo huwa na mafunzo na maadili fulani kwa mfano, maadili ya kuwaelimisha wana jamii kuhusu madhara ya kutoa mimba, madhara ya zinaa na mengineyo.

Umahiri wa wasanii wa muziki katika kutumia Kiswahili unajidhirisha katika muziki wa kizazi kipya au muziki wa kufokafoka, mziki wa ngonjera (Bongo Flava) .

Ijapokuwa baadhi ya watu wanauponda kuwa una maadili au utamaduni wa kigeni lakini unawasilishwa kwa lugha ya Kiswahili na unaelezea matukio yaliyomo kwenye mandhari ya Tanzania.

Katika magazeti na vyombo vingine vya habari, lugha ya Kiswahili ni mojawapo ya lugha zinazotumika kuelezea, kuelimisha na kuburudisha wana jamii kuhusu mambo kadhaa wa kadhaa yakiwemo ya utamaduni.

Michoro ya vikatuni huambatana na maelezo yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili ili kutoa mafunzo mbalimbali ya kitanzania kwa walengwa.

Lugha ya Kiswahili hutumika katika sala, dua kuomba na hata kuabudu.

Viongozi wa dini hutumia lugha ya Kiswahili katika kutunga sheria na kanuni pamoja na kuandika vitabu vyenye mambo bora ya kuelimisha jamii.

Lugha ya Kiswahili hutumika katika sherehe na ibada za jadi kwa mfano, katika jando na unyago, wakati wa kutoa, wakati wa kukabidhiwa madaraka au majukumu mapya, wakati wa kuamiri majengo na mengineyo.

Kwa kutumia lugha ya Kiswahili, wazee huwaingiza wahusika katika hali mpya ya maisha.

Huwafunza namna ya kuishi na kutenda mambo kulingana na majukumu yao.

Huwaarifu wahenga kuwa vijana wao wameamiri na kuwaombea kwa Mungu au miungu na wahenga wawaongoze, wawalinde na kuwafanikisha maishani.

Lugha ya Kiswahili hutumika katika kusimulia hadithi ambapo lugha ya nathari hutumika kutoa mafunzo na maadili mbalimbali.

Mtamba hadithi ana uwezo wa kutumbukiza hapa na pale semi zenye maana maalum ambazo ina mafunzo kwa wanajamii.

Kwa upande wa changamoto iliyopo kwa lugha hii ili iwe kielelezo cha utamaduni wa Mtanzania ni kwamba baadhi ya watumiaji wa lugha hii hususan vijana na baadhi ya watu wazima wanaidhalilisha kwa kuzungumza lugha isiyo ya heshima au staha, huko mitaani, katika daladala, vijiweni na katika mazingira anuwai.

Ieleweke kuwa maendeleo ya sekta zote, yawe ni maendeleo ya kiuchumi,kisiasa, kijamii na kitamaduni yanahusisha lugha katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.

Ni muhimu kufahamu utamaduni ni sekta mtambuka ambayo inahusiana na maeneo mengine.

Hivyo sekta zote zinapaswa kuhimiza matuimzi ya kiswahili, iwe ni kwa mazungumzo au kwa maandishi.

Vyombo vya habari ambavyo ni sekta muhimu ya utamaduni wa jamii na vyenye nguvu kubwa katika kuutanagaza, kuutetea na kuueneza utamaduni, kwa makusudi au bila kujua vinatumika kuudhoofisha utamaduni wa jamii, kuibua mitafaruku ya kiutamaduni au kueneza utamaduni wa kigeni usioifaa jamii yetu.

Ukiukaji wa maadili katika matumzi ya lugha,picha na michoro ni hali ambayo inalalamikiwa kila siku hasa katika TV na magazeti.

Hivyo, zifanyike jitihada za kujenga uwezo wa wanahabari, wasanii na wana lugha kwa ujumla kwa kuwapatia mafunzo kuhusu utamaduni kwa kupitia semina, warsha, makongamano na matamasha mbalimbali ili hatimaye watumie lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuikuza badala ya kuitumia kibiashara tu kama ilivyo sasa.

Pia vyombo vya habari vishiriki kikamilifu katika kuelimisha umma kuhusu matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili.

Kutoka China Radio International.

No comments: