`Ukibakwa ukaambukizwa VVU, wahi hospitali utapona`
2007-08-25 09:49:14
Na Gaudensia Mngumi.
Wanawake na watoto wanaobakwa na kuambukizwa virusi vya Ukimwi, wanaweza kutibiwa na kupona iwapo watawahi hospitalini ndani ya saa 72, imefahamika.
Wanawake na watoto hao watatibiwa na kupona kwa kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs).
Hata hivyo, aliyebakwa au kulawitiwa, atalazimika kwenda hospitalini katika kipindi kisichozidi saa 72 vinginevyo dawa hizo hazitafanya kazi.
Hayo yalisemwa na daktari wa magonjwa ya wanawake na mtaalamu wa masuala ya Ukimwi, Dk. Suleiman Muttani jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, aliyebakwa ama kulawitiwa na kuambukizwa na VVU, atatakiwa atumie dawa hizo kila siku kwa wiki nne mfululizo.
Alitoa ugunduzi huo kwenye mjadala wa namna ndoa za utotoni na vitendo vya ubakaji vinavyochangia maambukizi ya Ukimwi.
Mjadala huo ulindaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Nchini (TAMWA).
Dk. Muttani ambaye ni Mkuu wa Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam, aliitaka jamii kufahamu kuwa huo ni ukweli maambukizi ya Ukimwi yanaweza kuondolewa kama aliyebakwa na kuambukizwa atawahi hospitalini.
Alifafanua kuwa, mtu anapodhalilishwa kingono, atatakiwa kuwahi hospitalini, kufanyiwa mahojiano, kupewa ushauri nasaha na kuchunguzwa damu na iwapo ana VVU, ataanza dawa mara moja.
Hata hivyo, alisema iwapo hana VVU, dozi hiyo haitamsaidia kwani ameathirika na kwamba atapewa ushauri nasaha wa namna ya kuishi kwa matumaini na kuchunguzwa zaidi.
Aliongeza kuwa, aliyebakwa atapewa ARVs pale atakapokubali kupimwa VVU na iwapo atakataa hatapewa dawa hizo.
Lakini kwa watoto sharti hilo haliwahusu, kwani hawana ridhaa kutokana na umri wao mdogo, alifafanua.
Kwa upande mwingine, alisema wanaobakwa wanaweza kufika hospitalini kupewa matibabu bila kupitia polisi kuchukua fomu namba tatu, lakini wanapohudumiwa warudi polisi kwa ajili ya fomu hiyo kama taratibu zinavyotaka.
Kwa mujibu wa taarifa za ubakaji za Kituo cha Msaada wa Kisheria (WILAC) cha jijini, unyanyasaji wa watoto kingono ni mkubwa na nyakati hizi wazazi na jamaa wa karibu ndiyo watuhumiwa.
Mtoa mada wa asasi hiyo Bi. Scholastica Julu, alisema zipo kesi zinazofikishwa WILAC zikiwalalamikia wazazi wanaume kuwa, mbali na kuwanajisi watoto huwanyonyesha watoto wachanga uume wao.
Kadhalika, watu wanaojiita kaka wa hiari ambao ni wanaume marafiki wa familia, huwabaka watoto wa kike wa familia za marafiki zao.
Vikongwe nao ilielezwa kuwa hubakwa, kulawitiwa hata kuuawa kikatili na pia kuchukuliwa sehemu zao za siri.
``Kuanzia 1998 hadi sasa, kuna wafungwa 15,140 magerezani wa makosa ya kujamiana pamoja na mahabusu 2,687 wa kesi hizo wanaosubiri hukumu,`` alisema Bi. Julu.
- SOURCE: Nipashe, Jumamosi 25 Agosti 2007
No comments:
Post a Comment