BALOZI wa Marekani nchini anayemaliza muda wake, Michael Retzer, ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Balozi Retzer, alisema mpaka sasa Takukuru na Mkurugenzi wa Mashitaka wameweza kukamata kile alichokiita ‘samaki wadogo wadogo’ wachache, lakini kuwaacha ‘samaki wakubwa’ wakiendelea kuogelea katika bahari ya rushwa.
“Napendekeza kwenu kwamba ‘samaki wakubwa’ si wachache na labda kuna hata papa kwenye dimbwi hili la rushwa. Napenda kumtia moyo Rais Jakaya Kikwete kurejesha ari na nguvu mpya aliyoionyesha alipoingia madarakani na kukabiliana na rushwa,” alisema Balozi huyo.
Balozi Retzer, alisema hayo jana wakati akiwaaga Watanzania katika hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, Dar es Salaam.
Alisema sasa wakati umefika kwa ‘papa’ wa rushwa kukamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Alisema hata nchini Marekani wanakabiliwa na tatizo la rushwa na alibainisha kuwa, nchi yake imewahi kuwachunguza magavana, maseneta na wabunge, na kwamba wengi wao wamejiuzulu na baadhi wamefungwa jela kutokana na visa vya rushwa.
Alisema dhana ya Takukuru ni nzuri, lakini itaweza kuchunguza rushwa mahali popote inapojitokeza iwapo tu itafanywa kuwa kweli taasisi huru isiyoingiliwa.
Aidha, balozi huyo alivipongeza vyombo vya habari nchini kwa kazi nzuri ya kuchunguza rushwa na akasema kuwa nchini Marekani kuna uhuru wa vyombo vya habari, unaolindwa na katiba yao, kwa kusaidia serikali iendee kuwa mwaminifu.
Katika kukabiliana na rushwa nchini, balozi huyo aliihimiza serikali kuacha kutumia mawakala wanapofanya manunuzi makubwa ya serikali.
“Kuhusu suala hili, ninaongelea juu ya madai yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu makampuni kama Richmond Development na BAE.
“Kama unanunua bomba la kusafirishia mafuta, ndege au mitambo ya kuzalisha umeme yenye thamani ya dola milioni 150, hauhitaji wakala au kampuni, ambaye kazi yake ni kuwa dalali tu. Unakaribisha rushwa,” alisema Balozi Retzer.
Alisema kila biashara halali, iwe kampuni ya General Electric, Pratt Whitney, Boeing au kampuni yoyote kubwa ya kimataifa inayozalisha bidhaa, itafurahi kuzungumza na serikali moja kwa moja.
Akizungumzia suala la muafaka kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), alisema anaamini vitafanikiwa kumaliza mazungumzo yao na yatapatikana makubaliano yanayoridhisha pande zote mbili.
Alisema wapiga kura wa vyama viwili huko Zanzibar wamegawanyika katikati na imekuwa hivyo kwa muda mrefu sasa. Alisema hali hiyo inaweza kurekebishwa kwa vyama husika kufikia muafaka na maelewano kati yao.
Alitoa mfano wa Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton, alimchagua seneta mashuhuri wa Chama cha Republican, William Cohen, kuwa Waziri Mwandamizi wa Ulinzi.
Hata hivyo, alisema anaamini juhudi za kupatikana kwa muafaka huo zitafanikiwa hivi karibuni na akawasihi viongozi wa vyama hivyo, wafanye jitihada za kupatikana muafaka ambao utakubaliwa na pande zote mbili.
Akizungumzia maendeleo ya kiuchumi, alisema Serikali ya Marekani iko mbioni kusaini mkataba wa mpango wa Millennium, ili kumsaidia Rais Kikwete kushughulikia vipaumbele vya taifa vitakavyogharamiwa na fedha kutokana na mradi huo.
“Msaada wa Millennium ambao hivi sasa bado unajadiliwa, huenda ukaingiza zaidi ya dola milioni 650 kutekeleza miradi mipya ya barabara, maji na nishati ya umeme katika miaka mitano ijayo.
“Lakini jambo la muhimu vilevile linalohitaji uharaka sana ni tathmini makini na urekebishaji wa sheria na vizuizi vya urasimu ambavyo vinazuia makampuni ya biashara kuanzisha miradi yao nchini Tanzania kwa urahisi na kuifanikisha,” alisema balozi huyo.
Alisema Benki ya Dunia hivi karibuni na Kampuni ya ushauri ya Booz Allen Consulting, ilifanya utafiti na kubaini kuwa Tanzania ilichukua nafasi ya 127 kati ya nchi 175 kwenye kundi la urahisi wa kufanya biashara.
Balozi huyo alisema kama ni vigumu kuanzisha biashara nchini Tanzania, Tanzania itakuwa na biashara chache za kusukuma mbele injini ya uchumi wake.
Aidha, alisema pamoja na mapendekezo yaliyotolewa katika tafiti hizo, majaji walipwe mishahara ya kutosha, ili wasishawishike kutafuta vyanzo vya mapato ambavyo si halali, badala yake waendelee kutoa haki kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia janga la ukimwi, alimpongeza Rais Kikwete kwa juhudi zake za kupambana na ugonjwa huo nchini na kwamba Marekani itaendelea kuisaidia Tanzania kupambana na ugonjwa huo.
Alisema kutokana na hali hiyo, wakati umefika kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuanza kutumia teknolojia mpya katika kupima ukimwi.
Alisema serikali ya nchi yake iko tayari kuisaidia Tanzania kutoa mafunzo kwa wapimaji damu 1,000 wa kawadia ambao wataweza kusaidia kuwapima Watanzania wote ili kufahamu hali za afya zao.
Alisema kipimo cha hivi sasa kinachukua hatua 127 na kinahitaji vifaa zaidi na damu zaidi, lakini kipimo kipya kinachukua hatua 10.
Balozi Retzer, alisema Serikali ya Marekani, kupitia mpango wa Rais Bush wa kupambana na malaria umepata mafanikio makubwa Zanzibar na Tanzania Bara na akatoa wito kwa Serikali ya Tanzania na nchi nyingine wahisani kuunga mkono juhudi hizo.
Sambamba na hayo, balozi huyo alizungumzia hatari ya chama chochote cha siasa hususan chama tawala kumiliki makampuni ambayo yanafanya biashara na serikali.
Chanzo cha habari Tanzania Daima, Alhamisi tarehe 30 Agosti 2007.
No comments:
Post a Comment