Tuesday, September 18, 2007

Siri nzito yafichuka (Umbea wa Bongo?!)

"Mapokezi hayo yaliyofanyika Agosti 18, mwaka huu katika viwanja vya Jangwani na MC wa shughuli hiyo, Bw. Wilfred Lwakatare alimkaribisha shehe mmoja jukwaani, alipopanda alianza kuwaombea dua mbaya wale wote waliosababisha Zitto kusimamishwa Ubunge, ni dhahiri Mudhihir alikuwa mtu wa kwanza kumtia kitanzi Kabwe bungeni na ndio tunaoanisha tukio lile na ajali yake," alisema Juma Ally.

Akifafanua Bw. Juma alisema Mashehe wanapoomba dua mbaya kwa mtu wanayeamini kuwa kafanya kosa hutokea na akatoa mfano jinsi walivyofanya kwa Mwenyekiti wa TLP Bw. Augustine Mrema miaka ya nyuma.

Alisema Bw. Mrema aliombewa dua mbaya na Mashehe katika Msikiti wa Mtoro ili chama chake kisambaratike na asielewane na watu kisiasa na baada ya muda mfupi dua hiyo ikasikilizwa na Mungu.

"Dua ile ilisikilizwa, chama alichokuwa akikiongoza cha NCCR Mageuzi kikagawanyika mara mbili na viongozi wakuu wakamkimbia akiwemo Katibu Mkuu wake Mabere Marando na baadaye Prince Bagenda na Hamadi Tao," alisema Juma.

Akifafanua nguvu za dua za Mashehe, mwananchi huyo alisema licha ya kukimbiwa na watu hao, Mrema alitoswa pia na wasomi akiwemo Profesa Mwesiga Baregu, Dk. Ringo Tenga, Dk. Masumbuko Lamwai, Dk. Sengondo Mvungi na wanasiasa makini kama vile James Mbatia, Thomas Ngawaiya, Stevin Wassira na Daniel Nsanzigwanko.

Alisema kutokana na mfano huo, anaamini kuwa dua mbaya iliyosomwa mbele ya halaiki ya watu katika viwanja hivyo kwaajili ya wale wote waliohusika na kusimamishwa kwa Zitto ndiyo 'iliyomuumiza' Mudhihir.

Naye Frida Choda alisema alishuhudia dua mbaya ikiombwa na shehe huyo kwa wale wote waliosababisha Zitto kusimamishwa bunge na shehe huyo na baadaye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bi Ndorokinde Kessy naye alipandishwa jukwaani na Lwakatare kisha aliomba duwa akiwalaani mafisadi na akamuomba Mungu kuwapa moyo wa huruma (mafisadi) wawe kama walivyokuwa mitume wa zamani.

Baadhi ya wakazi jijini Dar es Salaam waliohojiwa kutokana na dhana hiyo, walisema kwamba inaweza kuwa ni moja ya sababu ya ajali ya Mudhihir jambo ambalo wengi hawalijui na kushauri kuwa wawatafute viongozi waliomuandaa shehe huyo ili dua yake igeuzwe, vinginevyo inaweza kuleta madhara makubwa zaidi.

Hata hivyo, Mudhihir alipohojiwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya Muhimbili alipolazwa kuhusiana na hoja hiyo, alisema kuwa hakukuwa na mkono wa mtu na kwamba ajali ilitokea katika mazingira ya kawaida yanayofanana na ajali nyinginezo na anaamini kwa rehema za Mungu atarejea katika afya njema ingawa amepoteza mkono mmoja.

Mudhihir alipata ajali ya gari eneo la Sido mkoani Lindi Alhamisi iliyopita na imesababishwa akatwe mkono wake wa kulia.Wakati huo huo, John Gagari kutoka Kibaha anaripoti kuwa mfanyabiashara maarufu George Thomas (50) amekatwa mkono kufuatia ajali iliyotokea hivi karibuni mjini hapo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani, Bw. Thomas alisema ajali hiyo imemfanya awe na ulemavu wa mkono wa kushoto hali inayomfanya aanze maisha mapya ya kutumia mkono mmoja wa kulia.

Akielezea juu ya tukio hilo, Thomas alisema kuwa alipanda basi la kampuni ya Hood aina ya Scania lenye namba za usajili T49 ARM likitoka Dar es Salaam kwenda Tunduma siku ya ajali.

"Basi letu lilikuwa kwenye mwendo wa kawaida na tulipofika eneo liitwalo kwa Mathias Kibaha, nyuma yetu likaja basi la kampuni ya Dar Express namba T273AHU lililokuwa likielekea Arusha, likawa linayapita magari mawili kwa wakati mmoja likiwemo letu, yakawa sambamba, mara likatokea lori mbele ya Dar Express hali iliyomfanya dereva wake atubane na kutugonga ubavuni, hivyo kupinduka," alisema.

Aliongeza kuwa baada ya basi lao kuanguka, mkono wake ulisagwa na ukabaki kiganja tu ndipo alipotolewa eneo la tukio na kupelekwa Hospitali ya Tumbi kwa ajili ya matibabu, "Namshurukuru Mungu kuninusuru na kifo na naendelea vizuri na matibabu ingawa nimepoteza mkono,"alisema Thomas kwa masikitiko.

No comments: