Jambo moja muhimu ambalo sote hatuna budi kukubaliana nalo ni kwamba Richa Adhia ndiye atakayetuwakilisha watanzania wote katika mashindano ya urembo ya dunia (Miss World) tarehe mosi(1) Desemba mwaka huu huko Sanya nchini China.
Hivi sasa anapojiandaa kuiwakilisha Tanzania huko nchini China, tulipata fursa ya kufanya naye mahojiano mafupi kuhusiana na maandalizi yake na ujumbe alionao kwa watanzania na wadau wote wa masuala ya ulimbwende. Yafuatayo ni mahojiano kamili;
BC: Richa kwanza hongera sana kwa ushindi wako wa Miss Tanzania 2007. Ulijisikiaje baada ya kutangazwa mshindi siku ile pale Leaders Club?
RICHA: Asante nashukuru. Nilipotangazwa kuwa mshindi nilishikwa na butwaa na kwa sekunde chache niliona kama ni ndoto.
BC: Watu wengi wametuandikia wakiomba tukuulize swali hili. Kwa maoni yako unadhani ni kwanini majaji wa Miss Tanzania 2007 walikupa wewe ushindi na si wenzako mliokuwa mkichuana? Nini kilikusaidia?
RICHA : Jibu la swali hili wanalo majaji. Kilichonisaidia mimi ni kujiamini na kufuata maelekezo yote tuliyopewa na waandaaji.
BC: Unapojiandaa kuelekea China kama mwakilishi wa taifa letu la Tanzania ni mambo gani matano (5 ) mazuri kuhusu nchi yako ambayo ikitokea ukaulizwa huko China hutofikiria kwa zaidi ya nusu dakika kuyataja?
RICHA: Mazuri ni mengi lakini nayataja 5 kama ulivyo uliza.
(1)Amani na Upendo: Nchi yetu ina makabila mengi na kila kabila lina utamaduni wake. Lakini tunaishi pamoja kwa amani na upendo pia tuna uhuru wa kuabudu.
(2)Tanzanite: Ni nchi pekee duniani yenye madini ya Tanzanite.
(3)Ngorongoro crater: Hii ni maajabu ya nane ya dunia na ipo Tanzania.
(4)Mlima Kilimanjaro: Ni mlima mrefu kuliko yote Afrika. Ni kivutio kikubwa kwa watalii.
(5)Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika: Ziwa Victoria ni ziwa kubwa kuliko yote Afrika, na Ziwa Tanganyika ni ziwa lenye kina kirefu kuliko yote Afrika.
BC: Tangu tulipoandika kuhusu ushindi wako katika blog yetu, kumekuwepo na ‘mvua” ya maoni juu ya ushindi wako. Wako wanaounga mkono ushindi wako na wapo pia wanaoupinga. Wanaoupinga wanatoa sababu kama vile; kwa sababu wewe ni mtanzania mwenye asili ya Asia basi kwa ujumla utamaduni wako ni wa kihindi zaidi ya kitanzania. Unawaambia nini watu wa kundi hilo linalokupinga?
RICHA: Nashukuru sana, mimi ni Mtanzania mwenye asili ya kiasia, lakini nimezaliwa Tanzania na wazazi wangu wamezaliwa Tanzania, mama yangu anatoka Pemba na baba yangu anatoka Morogoro. Nimekulia katika utamaduni wa kitanzania, ni utamaduni pekee ninao ufahamu, ninaouthamini, na ninao upenda kwa dhati.
Nawaomba watu wa kundi hilo wanaonipinga, waungane na mimi wanipe sapoti kwa sababu ninawakilisha Watanzania wenzangu wote.
BC: Hii itakuwa sio mara yako ya kwanza kuiwakilisha Tanzania katika medani za kimataifa za masuala ya urembo. Uliwahi kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss Earth yaliyofanyikia huko Philipines mwaka jana. Hukushinda. Una mategemeo gani katika mashindano ya Miss World mwaka huu? Unategemea kujiandaa vipi kuwania taji la Miss World tofauti na ulivyojiandaa ulipokwenda kushiriki Miss Earth mwaka jana?
RICHA: Ni kweli nilishiriki shindano la Miss Earth mwaka jana [2006] na sikushinda. Lakini katika shindano kuna kushinda na kushindwa. Na asiyekubali kushindwa si mshindani.
Isitoshe nimejifunza mengi kwenye shindano la Miss Earth na nataraji nitayatumia mafunzo hayo kwenye mashindano ya Miss world mwaka huu. Nimeshaanza kujiandaa na nitajitahidi kwa uwezo wangu wote kupeperusha bendera ya taifa vizuri.
BC: Umejifunza mambo gani ya msingi mpaka sasa hivi baada ya kuwa Mtanzania wa kwanza mwenye asili ya kihindi [Asia] kushinda taji la Miss Tanzania ?
RICHA: Kwa ujumla, nimejifunza kuwa Tanzania ni nchi yenye haki sawa kwa kila Mtanzania bila ya kujali rangi, kabila au dini yake.
BC: Una lolote ungependa kuongezea?
RICHA : Nashukuru sana kwa maswali yako na ninawaomba Watanzania wenzangu waniunge mkono na waniombee dua niweze kuiletea sifa nchi yetu nzuri ya Tanzania.
BC : Asante sana Richa kwa muda wako.Tunakutakia kila la kheri.
Mahojiano haya kutoka Bongo celebrity.
No comments:
Post a Comment