Sunday, September 09, 2007


WATU 31 wamefariki dunia na wengine 76 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizotokea katika mikoa ya Mbeya na Morogoro.

Ajali iliyotokea Mbeya ilihusisha basi la Kampuni ya Sabco, lililogongana uso kwa uso na lori katika kijiji cha Majenje Igurusi, Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya.
Waliokufa na kutambuliwa majina yao ni; Maramilanji Sinkala, Mtoto Omary na mama yake aliyefahamika kwa jina la mama
Omary. Wengine ni, Lutangiro Nyagawa, Dereva wa basi la Sabco Idi Simba, Jane Sheredi, Mohamed Bagasheni, Mama

Farida, Lupona Agustino na watoto wa familia moja Stella George na Telesia George.
Orodha hiyo ya waliofariki inajumuisha wanawake 14 na wanaume 13 ambapo kati ya marehemu wote, wawili walikuwa ni watembea kwa miguu, watatu ni kutoka katika Lori na 22 ni abiria wa basi la Sabco.

Akielezea tukio hilo Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kiwanjani kata ya Igurusi, Pilu Ibrahimu alisema kuwa, ajali hiyo ilitokea majira ya saa mbili na nusu asubuhi,baada ya basi la Kampuni ya Sabco lililokuwa likitokea Tunduma kuelekea jijini Dar es Salaam, kugongana uso kwa uso na Lori na kichwa cha gari hilo kuharibika vibaya.

Alisema kuwa, basi hilo lilikuwa katika mwendo mkali huku pia likitaka kulipita gari lingine hali iliyoshindikana maana lilikutana uso kwa uso na roli lililokuwa limebeba mawe likitokea Tanga kuelekea kiwanda cha Saruji Mkoani Mbeya.

Ajali hiyo pia ilisababisha wafanyakazi watano wa Halmashauri ya Mbarali waliokuwa katika gari lingine kujeruhiwa akiwamo Afisa Elimu wa Wilaya ya Mbarali, Kezia Juakali.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Steven Mwinamila alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na akaeleza kuwa, chanzo cha ajali ni mwendo kasi na dereva wa basi kutaka kulipita gari lililokuwa mbele yake.

Majeruhi wa ajali hiyo wapatao 33 wamelazwa katika hospitali ya Misheni ya Chimala kati yao wawili wako katika chumba cha upasuaji, kumi wamelazwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya na hali zao zinaelezwa kuwa ni mbaya.

Mmoja wa Majeruhi Marko Matuta ambaye alikuwa na familia yake ya jumla ya watu sita alisema kuwa, tukio hilo alilisikia kama bomu na kujikuta yuko nje na aliweza kupata fahamu baadaye na kwamba mpaka wakati anazungumza na gazeti hili alikuwa hajui watoto wake watatu aliokuwa nao kama wako hai au wamefariki dunia, ila amepata taarifa kuwa mke wake Doto Lunguja amejeruhiwa vibaya.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya John Mwakipesile alisema kuwa, mfululizo wa ajali za kampuni ya mabasi ya Sabco unatokana na utovu wa nidhamu na uzembe unaofanywa na madereva wa mabasi hayo.

Taarifa ya Mkuu huyo, ilieleza pia kuwa, Waziri Mkuu Edward Lowassa alikuwa amepata taarifa ya ajali hiyo na akatoa pole kwa waliokutwa na ajali hiyo.

Katika tukio jingine Ashton Balaigwa anaripoti kuwa watu wanne wamefariki dunia na wengine 33 kujeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Mkoani Mwanza kuelekea mjini Dar es Salaam kugongana na lori.

Basi hilo linalojulikana kwa jina la Super Najmunisa liligongana na lori lililokuwa limepaki katika eneo la ajali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye alisema kuwa, ajali hiyo imetokea Septemba 7 mwaka huu majira ya saa 2.30 usiku katika eneo la kijiji cha Meseyu barabara kuu ya Morogoro na Dar es salaam.

Alisema kuwa, katika ajali hiyo watu wawili walifariki katika eneo la ajali ambao mpaka sasa hawajatambuliwa majina yao na miili yao imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva aliyekuwa akiendesha basi hilo
ambaye alitambuliwa kwa jina moja la Bernad alikimbia mara baada ya ajali hiyo kutokea.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya mkoa wa Morogoro, Dk Meshack Massi aliwataja waliofariki baada ya kufikishwa hospitalini hapo kuwa ni pamoja na mtu anayedaiwa kuwa utingo wa basi hilo, Said Chande na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Minja ambaye alivuja damu nyingi.

Dk Massi alisema kuwa, majeruhi wa ajali hiyo wengi wao wamevunjika miguu na wengine wameumia sehemu mbalimbali za usoni na kuwaomba wananchi wajitokeze kujitolea damu kutokana na hospitali hiyo kuwa na upungufu wa damu ambapo kabla ya ajali kutokea walikuwa na uniti 5 tu.

Hata hivyo Dk Massi alisema majeruhi waliopokelewa na baadhi yao kulazwa ni pamoja na Wendelini Mfaume,

Juma Amri,
Vendelini,
Joseph John,
Yohana Musa,
Saida Nassoro,
Hassan Hussen,
Magreth Samson,
Samson Zefania,
Mwajuma Said, na Michael Mweta.
Wengine ni pamoja na
Hamad Hanji,
Moris Mlaponi,
Robert Rajabu,
Musa Seleli,
Joseph Mazigo,
Maduhe (kondakta) wa basi hilo,
Wilson Mzaba,
Kaduma Nyomola,
Mlava Mathias,
Chemu Musa,
Daniel Idd na watu wawili wa familia moja ambao ni Elinaza Israel na Elisna Julius.

Majeruhi wengine waliopokelewa na kulazwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro ni pamoja na;
Yassin Bweyula,
Shaufa Ligamke,
Robert Kingu,
Peter Godfrey,
Monica Magoli,
Rabia Magoli,
Fatuma Said,
Amina Hama Omari,
Omari Midika na Anthon Bathalomeo.

Habari na picha kutoka: http://haki-hakingowi.blogspot.com/


No comments: