Sunday, September 09, 2007
Shenazi afariki.......................
Malkia wa kunengua miondoko ya Taarab na Mduara nchini, Shenazi Salum pichani ni miongoni mwa watu 27, waliokufa kwenye ajali ya basi, iliyotokea juzi kwenye Kijiji cha Majenje, Mbarali, Mbeya.
Kwa mujibu wa mdogo wa mwanamuziki huyo aitwaye Hanifa Salum, Shenazi alifariki dunia, muda mfupi baada ya kutokea ajali hiyo, iliyohusisha magari matatu....
alisema, Shenazi alipata ajali hiyo, alipokuwa akirejea nyumbani kwake Dar es Salaam na alikuwa akitoka Tunduma, Mbeya kwenye shughuli zake za muziki “Alituaga kwamba anakwenda Mbeya kufanya ‘shoo’, hatukujua kama ndiyo kifo kilikuwa kinamwita, lakini ndiyo hivyo Mungu kamchukua,” alisema Hanifa huku akitokwa na machozi.
Rafiki wa Shenazi ambaye naye ni mnenguaji maarufu, Mwajuma Thabit ‘Rose Jimama’, anasema kuwa marehemu alikwenda Mbeya na mwanamke aliyemtaja kwa jina moja la Tuki.
Rose alisema: “Nilipata taarifa kama Shenazi amepata ajali, nikapiga namba yake, ikapokelewa na polisi mmoja huko Mbeya, nikamuomba nataka kuongea na Shenazi, akanijibu, unataka kuongea na maiti? “Nilichanganyikiwa, yule polisi aliniambia rafiki yangu Shenazi amekufa na Tuki hali yake ni mbaya, nidhani utani, lakini yote ni mipango ya Mungu.”
Habari zaidi zilisema kuwa rafiki huyo wa Shenazi, Tuki, amevunjika miguu yote na alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Chimala, Mbarali. Shenazi alikuwa kwenye basi la SABCO aina ya Scania, T443 APF ambalo liligongana na lori pamoja na magari mawili yanayomilikiwa na Halmashauri ya Mbarali.
Ajali hiyo iliyoua watu 27, ilisababisha majeruhi 33. Shenazi alitarajiwa kuzikwa jana ambapo mwandishi wetu walifika nyumbani kwao, Ilala, Dar es Salaam na kukuta taratibu za mazishi zikiwa zimeshaanza kufanywa. Mbali na kunengua, malkia huyo atakumbukwa kama kungwi, aliyekuwa akiwafunda watu kabla ya ndoa, pia ni mwigizaji ambapo enzi za uhai wake aliwahi kucheza Filamu ya Kitchen Party ambayo ilipata umaarufu mkubwa.
Mungu Alaze Roho Za Marehemu Mahala Pema Peponi Amen...
Habari na picha kutoka: http://haki-hakingowi.blogspot.com/
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment