Tuesday, October 30, 2007


Bank of Tanzania (BoT)
wakiri tuhuma mpya za Slaa.


*Yasema ni miongoni mwa mambo yanayochungwa

*Makamba asema madai hayo ni ya uongo

Ramadhan Semtawa na Kizitto Noya

WATUHUMIWA wawili kati ya sita waliohusishwa na Muungano wa vyama vinne vya upinzani katika ufisadi mpya wa mabilioni, wamejitokeza na kuzungumzia tuhuma hizo.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni taasisi za kwanza zinazohusishwa katika ufisadi huo ambazo jana kila upande umetoa majibu yake kuhusiana na tuhuma hizo.

BoT imeelaza kuwa tuhuma zote zinachunguzwa chini ya Ukaguzi wa Kampuni ya Ernest & Young katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Tamko hilo la BoT limekuja ikiwa ni siku moja baada ya vyama vinne vya upinzani kutoa tuhuma mpya za ufisadi wa Sh10 bilioni, ambazo vinadai zimechotwa kutoka benki hiyo na kutumiwa na CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Gavana wa BoT, Juma Reli, alisema uchunguzi katika akaunti ya EPA kwa sasa umefikia robo tatu.

Reli ambaye pia ni Naibu Gavana wa BoT, alisema madai hayo si mapya kwani yote yanahusu madeni ya nje ambayo yanafanyiwa uchunguzi.

"Nafikiri ni vema tukasubiri uchunguzi ndani ya EPA, kwa maana tuhuma zote zinahusu ulipaji fedha katika akaunti hiyo," alisema na kuongeza:

"Kwa sasa uchunguzi huo umeshafikia robo tatu na hivi karibuni ripoti kuhusu uchunguzi huo itatolewa."

Alipoulizwa iwapo ni kweli BoT inafahamu kuhusu malipo katika akaunti hiyo ambayo ilibadilishwa ghafla, alisema kwa kawaida benki huwa haiangalii pesa zilizolipwa zinahamishiwa katika akaunti gani.

Reli alifafanua kwamba, utaratibu ni kwamba BoT haingalii fedha ilizolipwa zinaenda katika akaunti ipi nyingine bali kusimami taratibu za malipo.

Kuhusu kama BoT inaifahamu kampuni moja ya Afrika Kusini ambayo inaelezwa imetumika kuchotea fedha hizo, alisema ni dhahiri fedha kama hizo hulipwa kwa kampuni, lakini hakuthibitisha kama ni kweli fedha hizo zimelipwa kwa kampuni hiyo.

"Fedha hulipwa kwa kampuni, lakini nafikiri huu si wakati wa kuanza kuzungumzia kwa undani jambo linalochunguzwa, maana itakuwa ni kuharibu uchunguzi, tusubiri uchunguzi wa EPA ndipo yote yatabainika," alisisitiza.

Kwa upande wake CCM, imesema hakiwezi kueleza chochote kuhusu tuhuma hizo kwa kuwa ni za uongo.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Yusuf Makamba aliliambia gazeti hili jana kuwa tuhuma kwamba CCM kiliiba fedha kwa ajili ya kufanikisha kampeni zake za uchaguzi hazina ukweli wowote.

"Siwezi kutoa ufafanuzi juu ya madai ya uongo. Uongo haujibiki unakaliwa kimya," alisema Makamba.

Alisema wapinzani waliotoa tuhuma hizo walipaswa kuzitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010 ili jamii iweze kuwaunga mkono, badala ya kuzitoa sasa na kumaliza uongo wote uliotakiwa kutolewa wakati wa uchaguzi huo.

"Uongo huo ungewasaidia kama wangetoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, sasa wanapoumaliza leo watasema nini kipindi hicho kikifika?" alihoji

Mbali na BoT na CCM, watuhumiwa wengine ambao umoja wa wapinzani umewahusisha na ufisadi huo mpya ni kampuni moja ya Afrika Kusini, Benki moja nchini na mawakili wawili wa kampuni moja ya uwakili nchini.

Juzi umoja wa vyama vya CUF, TLP, NCCR- Mageuzi na CHADEMA, ulitaja orodha nyingine ya watuhumiwa wa ufisadi ambao wamewahusisha na upotevu wa mabilioni mengine katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa Chama hicho Tundu Lissu, walisema kuwa watuhumiwa hao waliiba zaidi ya Sh10bilioni kutoka BoT wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Walisema fedha hiyo iliibwa kutoka BoT katika kipindi cha mchakato na kampeni za mgombea urais kupitia CCM Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 14 mwaka juzi kuanzia Agosti mosi hadi Desemba 10 mwaka 2005.

Katibu Mkuu wa Chadema Dk Slaa, alisema katika mkutano huo uliohudhuriwa na baadhi ya wakazi wa jijini Dar es Salaam, kuwa nyaraka zilizopatikana hivi karibuni zimeonyesha kuwa katika kipindi hicho makampuni mawili hewa ya Afrika Kusini yalianzishwa nchini kwa lengo la kupitishia fedha zilizoibwa kutoka BoT ili kusaidia kampeni za CCM.

No comments: