Monday, October 22, 2007



Kikwete shughulikia tuhuma hizi.

TANGU viongozi wa kambi ya upinzani walipotangaza orodha ya viongozi wanaodaiwa kwa namna moja au nyingine kuhusika na ufisadi, mengi yametokea na kusemwa.

Jambo moja li -wazi hata hivyo; kuwa wote waliotajwa katika orodha hiyo wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kujisafisha na tuhuma zinazowaandama pasipo mafanikio.

Na wakati mambo haya yakiendelea, kile tulichokisema awali, kuwa mwenendo wa mambo nchini unaashiria kuwepo mapinduzi ya lazima katika uongozi wa sasa, umeanza kuonekana.

Tuliwahi kuandika, tukimuonya Rais Jakaya Kikwete kuhusu ukimya wake dhidi ya tuhuma zinazomwandama yeye mwenyewe pamoja na wasaidizi wake, kuwa zinaichafua serikali yake na kuifanya isiaminike kwa wananchi.

Rais Jakaya Kikwete.
Picha na Carolyn Sithembiso Matenge Chikwenga
Februari 28, 2007, Oslo - Norway.

__________________________

Tukatahadharisha kuwa, iwapo Rais Kikwete atapuuza kuchukua hatua za kujisafisha yeye mwenyewe na serikali yake, basi uwezekano wa serikali yake kupinduliwa kupitia sanduku la kura ni mkubwa.

Lakini Rais Kikwete hakutusikia, aliendelea kukaa kimya mpaka hivi karibuni alipoibuka na kueleza kuwa tuhuma zote za rushwa zitafanyiwa kazi na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote bila kujali wadhifa wake punde akipatikana na hatia.

Rais Kikwete aliwaonya wanasiasa kuacha kujichukulia mamlaka yote mikononi mwao, wakijiona wao ndio wapelelezi, waendesha mashitaka na mahakimu dhidi ya wale wanaowatuhumu kwa ufisadi.

Kwa hakika, sisi hatukutegemea kama Rais Kikwete angetoa majibu ya aina hiyo kulingana na uzito wa tuhuma zilizoelekezwa kwake pamoja na wasaidizi wake.

La kwanza tulilotegemea kulisikia kutoka kwa rais ni ufafanuzi dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake, tulitegemea kumsikia akikanusha ama akikubali kuhusika katika madai hayo ya ufisadi. Pili, tulitarajia kusikia kauli yake dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwa wasaidizi wake. Lakini haikuwa hivyo.

Baada ya kauli hiyo ya Rais Kikwete, baadhi ya watu mashuhuri hapa nchini wametoa kauli nzito ambazo kwa ujumla zinaelekea kutofautiana na msimamo wa Kikwete.

Wa kwanza ni Joseph Bituku, mmoja wa wasaidizi wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa muda mrefu na mwanachama wa TANU na sasa CCM, ambaye aliwataka viongozi wote wa Serikali ya Awamu ya Nne waliotajwa kwa tuhuma mbalimbali za rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma, kujiuzulu.

Kauli hii ya Butiku inadhihirisha kuwa, madai yaliyotolewa na viongozi wa kambi ya upinzani yamemgusa na amebaini kuwa yana ukweli. Kwa kauli hii, Butiku anatofautiana na Rais Kikwete katika mlolongo mzima wa tuhuma hizi dhidi ya viongozi wa serikali.

Wa pili, alikuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye alitamka kuwa tuhuma dhidi ya ufisadi, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma hazipaswi kudharauliwa na viongozi. Kwamba madai hayo yametolewa na watu wenye akili na wameamua kufanya hivyo kutokana na hali ya mambo wanayoishuhudia.

Kama Butiku, mzee Mwinyi naye ametofautiana na Rais Kikwete jinsi anavyozichukulia tuhuma hizi zinazomwandama yeye mwenyewe na serikali yake.

Wengine waliotoa kauli zinazoonyesha kukerwa na jinsi tuhuma zinavyochukuliwa na viongozi walioko madarakani ni pamoja na Jenerali Ulimwengu, na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, John Malecela. Mbunge wa CHADEMA, Philemon Ndesamburo, naye ameungana na kina Butiku, Malecela, Ulimwengu na wengine.

Kauli hizi ni tahadhari kwa Rais Kikwete kuwa viongozi wenzake, wakiwemo waliomtangulia kukaa Ikulu hawakubaliani na staili yake ya kushughulikia kashfa hizi.

Na sisi wa Tanzania Daima kwa mara nyingine tunaungana na hawa kumuasa Rais Kikwete kuwa staili yake ya kushughulikia kashfa hizi hatukubaliani nayo. Tunamshauri achukue hatua zinazostahili katika kukabiliana na kashfa hizi.

Kutoka Tanzania Daima.

No comments: