Sunday, October 21, 2007




Waacheni wapinzani waikosoe Serikali - Jakaya Kikwete



Rais Jakaya Kikwete.
Picha na Carolyn Sithembiso Matenge Chikwenga
Februari 28, 2007, Oslo - Norway.
____________________________

Mkumbwa Ally, Rome.

HabariLeo; Sunday,October 21, 2007 @00:02

RAIS Jakaya Kikwete amezungumzia ukosoaji unaofanywa na wapinzani dhidi ya serikali yake, akisema unaonyesha mafanikio ya demokrasia nchini.

“Kelele zao hazinisumbui. Hazinikoseshi usingizi. Ni suala zuri kwa wapinzani kuzungumza, na zaidi hata kupaza sauti na kukosoa, hasa kama hawatasababisha kuleta vurugu kwa umma,” Rais Kikwete aliwaambia Watanzania wanaoishi Italia jana.

Wanasiasa wa upinzani hivi sasa wamekuwa wakiendesha kampeni ya madai ya rushwa dhidi ya baadhi ya mawaziri na maofisa waandamizi wa serikali, ambao baadhi yao wameeleza kusudio lao la kuchukua hatua za kisheria.

Rais Kikwete aliwahakikishia Watanzania hao kwamba hakuna mgogoro wa kisiasa nchini. “Kelele zao ni za kawaida katika siasa za vyama vingi,” alisema.

Alisisitiza kwamba mikataba mipya ya madini itakuwa na kipengele mahususi kwa ajili ya kulipa kodi kwa kampuni za madini zinazopata faida, ambacho awali hakikuwapo.

Kuondolewa kwa kipengele kilichokuwapo katika mikataba ya awali kutawawezesha wawekezaji kubaki na theluthi mbili ya faida na serikali theluthi moja, jambo ambalo ni haki kwa pande zote, alisema Rais Kikwete.

Alifafanua kuwa wafanyakazi wazalendo wataajiriwa ili kukagua uzalishaji wa madini badala ya tathmini hiyo ya madini kufanywa na wageni ambao walikuwa wakilipwa fedha nyingi.

Pia alisema kampuni za madini zitalazimishwa kununua bidhaa zinazozalishwa nchini badala ya kuagiza nje.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amesema pendekezo la kuruhusu Watanzania wanaoishi nje kuwa na uraia wa nchi mbili, limepokelewa vibaya na Watanzania nyumbani.

Alishauri kuwapo kwa subira wakati serikali inapotathmini faida za pendekezo hilo la uraia wa nchi mbili.

“Hii imekuwa ni nia ya kila Mtanzania anayeishi nje ambaye nimekutana naye, lakini mwitikio nyumbani ni tofauti, ninaogopa, pendekezo litakataliwa moja kwa moja kama tutashinikiza mno sasa,” alisema Rais na kuongeza kuwa, Tume ya Kurekebisha Sheria inalishughulikia suala hilo.

Alisema serikali pia inatafakari masuala ya gharama kuhusu ombi jingine lililotolewa hapa la kuwaruhusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi kupiga kura.

Rais aliwashauri Watanzania wanaoishi nje kuwa mabalozi wazuri na kurejesha rasilimali zao kusaidia ustawi wa familia na jamaa zao nyumbani.

Rais Kikwete jana usiku aliondoka kwenda mjini Napoli, ambalo anatarajiwa kuhutubia mkutano wa kimataifa wa dini kuhusu amani kabla ya kwenda Ufaransa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.




No comments: