Monday, October 01, 2007

Simulizi toka London: Masudi kagoma kublogu au kublogiwa

na Freddy Macha.

BRADHA vipi siku hizi? Hatusalimiani. Hatuonani. Hatupigiani simu. Hatujuani? Ah...mi nipo tu.

Upo vipi bradha Masudi; umenuna, unaanza kunona kinamna siku hizi; unakula peke yako watusahau tuliokukaribisha mjini?

Ah si kweri blaza, miye nipo najali famiria yangu na watoto. Una mtoto mmoja tu tayari umevimba kichwa Bradha Masudi? Wawiri. Tayari Halima mimba ya pili? Tayali. Sasa, mbona hatuonani na mambo yako freshi?

Naogopa. Unaogopa nini Masudi? Woga una sababu blaza? Woga ni woga tu. Umenitega kweli na kitendawili. Kinachokutisha nini? Mi naogopa Mbongo yeyote anayepita kando yangu; awe wewe, mamako, babu yako, lafiki yako, nyanya yake lafiki yako, mpwa wake, hawala yake, kira Mbongo kwangu nuhusi tu. Hamfai wote.

Kila Mbongo kwako nuksi? Tena sana. Masudi katuna, kavimba, macho yamemtoka. Siku hizi Masudi hachezi mpira, siku hizi Masudi hafanyi mazoezi, kaanza kuvimbiana. Amenona. Nyumbani wakimwona watasema amenawiri. Uzunguni watasema afya yake mbaya. Unene ni ugonjwa.

Tena umenenepa vizuri kweli kweli siku hizi. Nakura supu za Kituluki na nyama choma. Nyama choma gani na mimi sikuoni baa za Watanzania hapa London.

Baa za Watanzania mi siendi blaza Freddy...mi nawaogopeni. Hiyo Kirabu Afulika...wala sifiki. Mara ya mwisho kwenda mwaka 2003. Nakumbuka tulipokwenda pale Club Afrique na wewe ukasifia nyama choma nzuri, ukaopoa kimwana toka Zimbabwe. Yuko wapi siku hizi Sofia?

Yure Sofia kaorewa na Mnaijelia, ana katoto kamoja. Kaolewa na Mnaijeria? Nasikia jamaa anakachalaza kweri kweri afadhari angeorewa tu na mimi. Mi sipigi mwanamke wala sichapi kofi, sana sana nafinya tu. Unafinya?

Nnafinya tu. Unafinya wapi?

Hapa. Masudi anaelekeza mkono wake nyuma ya tako anajifinya. Anaangua kicheko kikali, kinatoka hwa hwa hwa na kukatika chaaa! Utadhani mtoto mtundu aliyekuwa akiiba sukari kabatini akafumaniwa ghafla.

Kumbe kaingia Simpson. Simpson ni Mjamaika. Muuza bangi. Wote tunamjua lakini mimi nimemzoea zaidi. Hey, Simpson wazzzap?

Cool. Anajibu salamu Mjamaika akitucheki cheki na kutupa ngumi. Kugongeshana ngumi ndo mtindo wa salamu za weusi London. Anamkagua Masudi, macho ya kitemi, akimnusa nusa ka mbwa. Simpson fisi.

Have I seen you somewhere, mate? Simpson siku zote hutafuta wateja wa kuuza bangi. Yeye ni karagosi tu wa wapambe wa mji; msafirishaji na mtafuta wanunuzi mitaani. Ukitaka chochote cha wizi na nishai anacho.

Bunduki, visu, magari, baiskeli za wizi, laptopu, simu za mkononi...walkman za muziki aina ya I-pod. Kifupi Simpson theluthi moja jambazi koko, nyingine mkono wa wauaji, theluthi ya tatu mlevi wa madawa ya kulevya.

Zamani sana niliwahi kumtambulisha Masudi kwake, wakati ndiyo anaingia London, hawakuelewana Kiswahili wala Kiingereza wala sura wala maneno wala kope wala nahau.

Masudi msomi, kaja kutafuta shahada yake ya Masters enzi hizo, anachopenda watoto wa Kitasha, mpira, vitabu na kitanda cha kulala mapema asichelewe kuamkia Chuoni.

Enzi hizo wengine wala hamkumjua Masudi vizuri. Labda wale wanaomfahamu. Maana kujua na kufahamu ni kama paja na goti. Je, mnakumbuka? Masudi mkorofi vile vile. Mnakumbuka Masudi alivyokuwa anamwania totoz wa Kibrazili? Mnakumbuka?

Nikakutana naye katika basi kavimbiana uso mzima umejaa mapunye na majipu na madonda. Mnakumbuka Masudi alivyopigwa masumbwi na Mbrazili?

Akakubali kunyukwa maana alijua alikuwa anaiba mali ya mtu baadaye alipomaizi akalipa kisasi. Akamtafuta Mbrazili akamnyuka. Masudi mtoto wa Mwananyamala. Kwa vichwa anafaa kuitwa balozi wa Tanzania. Lakini ndugu msomaji wee si mpumbavu. Nikuulize.

Mtanzania gani asiyejua vichwa? Hiyo silaha ataikumbuka Mbrazili, na Mjamaika asipoangalia yatamfika maana hapa tunapopiga domo mi na Masudi huenda yakaokotwa meno saizi Ithnaashara (wanavyosema Waarabu, saa kumi na mbili jioni).

Masudi leo kakasirika, mi mwenyewe rafiki yake bado sijang´amua siri ya sifuri. Bado sijaelewa nini kinamguguna mwana wa Msele toka Mwanyamyala.

Mwambie asinijue. Ntamnyuka na bangi zake. Ntakuona wapi muza bangi mkubwa weee... You hot, bro?He is cool, Simps; just leave him alone, all his parents were killed in Burundi, he is full of grief.

Naongopa na Masudi kajua anazuia kicheko. Tangu lini Masudi Pashamoto Msele akawa mkimbizi toka Burundi? Mjamaika ananivuta kando. Kweli eti huyu bradha hataki widi? Nasema kweli hataki.

Wala kununua simu ya mkono modeli mpya iliyotoka mwezi jana? Hataki bwana wewe. Walevi wa bangi na madawa ya kulevya si walevi wa kawaida.

Labda wapo siku hizi kiasi Bongo lakini si desturi kama huku nchi zilizoendelea. Nyumbani ulevi mkubwa bado ni wa pombe na gongo na vitu kama hivyo, lakini Majuu ulevi mkubwa ni wa madawa, unga na bangi za kila namna. Walevi wa namna hii wako kama vichaa.

Wako tayari kuua, kunajis, kubaka, kupigana, kuongopa ili mradi wakipate kitu hata kama cha senti hamsini. Namwambia Mjamaika kuwa Masudi ni msomi, anachokitafuta hapa Ulaya masomo na ajira. Simpson anaona pengo ananiponyoka kiwizi wizi. Anamchapukia Masudi wa watu.

Brother i got a new laptop for you, Brand new. Only 200 pounds. Sony. 1000 Megabytes. Masudi anatingisha kichwa. Sina hela nyoko wee...Wha is SINA HELE mean?

Mi na Masudi tunacheka. Mjamaika anapandisha. Anapoingiza mikono mfukoni tunajua kitatoka kisu, mi najitayarisha kubingirishana maana hapa Uingereza visu ndiyo fedheha na desturi. Inachopoka bangi ya msokoto imepinda pinda kama jongoo. Jongoo mweupe lakini. Ishasokotwa, inavutwa, baada ya dakika mbili, Simpson anaona kila kitu kidogo.

Wanapita wanawake watatu, wawili wazungu mmoja mweusi, wanapiga makelele, hata kutuzidi. Utadhani mabata.

Hey you snakes and ladders; come over here, sweethearts! Simpson anawaendea. Wanawake kimyaaaa...Hakuna watu wanaoheshimiwa nchi hii kama wanaume wa Kijamaika. Kila mwanamke anamjua Mjamaika magirini, (labda aliyesoma) lakini hawawachezei.

Waafrika wote tunaokuja nchi hizi na kujigamba na magari na midomo tunavuna matunda ya harakati za Wajamaika dhidi ya kila aina ya ubaguzi wa nguruwe na ukaburu. Wajamaika wakorofi. Wale wanawake kumbe wanahitaji vitu.

Pochi zinafunguliwa. Meno yake Simpson yenye mapengo yaliyozibwa kwa dhahabu alipokuwa jela yanamerita meta gizani. Tunaachana nao.

Mi na Masudi tunaingia mgahawa mmoja wa Mturuki, tunaagizia vinywaji maana saa za futari zishawadia. Masudi anafungua kwa juisi ya maji ya machungwa.

Unaendeleaje mwezi Ramadhani Masudi?

Mwezi Mtukufu hapa Majuu dhiki tu ndugu yangu Macha. Nasikia malalamishi kila kona.

Nyumbani ni utamaduni. Hapa kero tupu. Saa ya futulu uko peke yako, afadhali mi nimeoa Mwisramu kuna jamaa wameoa wanawake wa huku Waklisto; inabidi ajipikie futali peke yake, saa ya daku ikifika kiramtu keshakura, kesharara; si unajua Wazungu hura chakura mapema, hawali usiku tena. Ziki tupu.

Lakini Masudi si bado uko na Halima? Bado niko naye ndiyo; ataenda wapi?

Nataka kusema atarudi kwa Rama naminya. Mliofuatilia habari za Masudi mmesikia alimwiba mke wa mtu. Rama siku hizi sijui anaishi wapi na Halima ukimwona utajua kwanini hata kama we si jambazi itabidi uwe.

Mazungumzo yamestawi. Tumeongelea habari ya swaumu hadi tukakosa la kusema sasa kimya. Naona umefika wakati wangu. Masudi. Naam.

Bado Kiswahili chako kimepwaya babu. Kwa vipi?

Bado huwezi kutofautisha ra na la ; au li na ri. Wewe ni wale Watanzania wanaoita televisheni luninga badala ya runinga na kusema kura badala ya kula.

Masudi anacheka. Unajua blaza mi sijijui mpaka unavyoniambia. Wee tu ndiyo huwa unanisahihisha. Hata shemeji yako Harima mwenyewe huwa ...

Halima. Si Harima. Ah unaona? Yanakwisha.

Lakini tulichokuwa tukikiongea kabla hajaja Simpson hatujakimaliza. Kipi?

Cha blogu.

Macho ya Masudi kama yamepakwa pilipili. Uso unamfura. Midomo inafutika, ana harara.

Miye burogu sitaki. Una nini na blogu Masudi?

Sina kitu lakini burogging sipendi. Hata pale kazini kwetu watu chungu nzima wana hii burogu. Nyumbani kuna jamaa mmoja lafiki yake sana huyu ndugu yako Ndesanjo ana bulogu lake huwa ananitumia nisome, mie hupitia tu rakini sina habali naro.

Je, unajua saivi karibu kila mtu nyumbani anataka kuanzisha blogu, wengine wanashindwa shauri ya lugha tu?

Najua, najua...tena kuna jamaa wanasema wameusoma huo Mwongozo wa Ndesanjo aliouandika wa kutengeneza burogu lakini bado hawawezi shauri Kiingeleza kinawapiga chenga. Mi sitaki. Basi Masudi nakuomba nikublogu wewe. Si unaona leo nimekuja na kamera kabisa nikutoe?

Ah, umetumwa Macha? Unapendwa nyumbani. Una mashabiki. Kuna watu wako tayari hata kukuozesha dada au binti zao, wapo jamaa wakikuona watakupeleka baa wakakupe bia. Mi na blogu mbarimbari blaza Macha. Maana picha yangu ikitoka tu, nimekufa. Picha yako ikitoka tu umekufa vipi? Ntapigwa Albadili...

Al badir hupigwa kwa mwenye kosa. Wee una kosa gani, kila mtu anakuhusudu. Wee mtu wa mfano. Mamako akapata mimba akiwa shule, Kilakala; akafukuzwa, akajitahidi akakuzaa, akakusomesha, akatafuta kazi, akakuleta Ulaya kwa pesa zake bila kuiba au kufanya umalaya. Sasa umesoma umemaliza, unafanya kazi, umeoa una watoto wangapi vile?

Wawiri; kulwa na doto.

Unaona sasa? Tungekuweka katika blogu ukaonekana kama mtu wa mfano. Mchapa kazi. Shujaa. Ah wapi, usinijue. Musinijue Wabongo. Wambea sana nyinyi. Mnasengenyana. Mnarogana. Mnaoneana wivu. Mi msinijue. Ah na tumwache Masudi wa watu.

Siku njema msomaji.

Barua pepe: kitoto2004@yahoo.co.uk

Blogu: http://kitoto.wordpress.com


No comments: